Monday, August 17, 2020

KASI YA USAMBAZAJI UMEME KWENYE TAASISI ZA UMMA YAONGEZEKA


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(wa kwanza kushoto) akiwasili kwenye kituo  cha Bukiriro, kilichopo kata ya Bukiriro,wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera,Agosti 16,2020, katikati Mkuu wa Wilaya ya Ngara Michael Mntenjele,(kulia) Mganga Mkuu wa kituo cha afya cha Bukiriro, Dkt Wilbroad Bukiriro.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Muyenzi kilichopo kata ya Lulenge, Wilaya ya Ngara, Mkoani Kagera, wakati alipokuwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi kazi ya usambazaji umeme vijijini

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akikata utepe kuashiri kwa kuwashwa kwa umeme katika shule  ya Sekondari Nyakahuru,iliyopo katika kijiji cha Mabale, kata ya Nyakahura, Wilaya ya Biharamulo

Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Muyenzi iliyopo kijiji cha Muyenzi, kata ya Lulenge,Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera wakimshangilia Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(hayupo pichani) mara baada ya kuwasili katika shule hiyo

Wananchi wa kijiji cha Bukiriro, kilichopo kata ya Bukiriro, wilaya ya Ngara Mkoa wa Kagera wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(hayupo pichani) wakati akiwa kwenye ziara ya kazi ya usambazaji umeme vijijini

………………………………………………………………………

Hafsa Omar-Kagera

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amesema Serikali inataendelea  kuzipa

kipaumbele  Taasisi za Umma nchini  katika usambazaji wa umeme vijijini ili siweze kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Ameyasema hayo , Agosti 16,2020 kwa nyakati tofauti  wakati akiwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini katika wilaya ya Ngara na Biharamulo,Mkoani Kagera.

Akiwa Mkoani humo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika Taasisi za Umma ambazo ni vituo vya afya na Pamoja Shule za Sekondari, vituo hivyo vya afya ni Pamoja na  kituo cha afya cha Bukiriro, kilichopo kata ya Bukiriro , Wilaya ya Ngara na kituo cha afya Nyakahuru kilichopo kata Nyakahuru, Wilaya ya Biharamulo, Mkoani Kagera.

Aidha,amesema kuwa,Sekta ya Nishati ina nafasi kubwa kuziwezesha sekta nyengine zifanikiwe kwakuwa bila ya nishati umeme Sekta ya afya itashindwa kutoa huduma bora kwa watanzania kwasababu huduma nyingi na muhimu kwenye vituo vya afya zinategemea nishati ya umeme.

Ameongeza kuwa, kwasasa Serikali inajenga vituo vya afya vingi nchini kwa kuzingatia hilo Sekta ya Nishati imeamua kuongeza kasi zaidi ya usambazaji umeme katika vituo vya afya ili Watanzania wapate huduma bora ya afya.

Kwa upande wa elimu, Naibu Waziri amesema kiwango cha ufaulu nchini kimeongezeka hasa katika maeneo ya vijiji kwasababu ya kazi  nzuri ya usambazaji umeme vijijini ambapo shule nyingi ambazo zipo kwenye vijiji hivyo zimeunganishwa na umeme.

Amesema kuwa, umeme umeboresha sekta ya Elimu nchini na  kuwataka  wanafunzi kutumia umeme huo kikamilifu kwaajili ya kujisomea na kujiongezea ufaulu katika shule zao.

Aidha, amtaka mkandarasi ya mkoa huo kuendelea kusambaza umeme katika maeneo ambayo yamesalia kwakuwa mradi huo upo ukingoni na wananchi wa vijiji hivyo wanahitaji huduma hiyo.

Pia, amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Kagera na kuwahakikishia kupatikana kwa umeme wa uhakika mara baada ya kumalizika kwa miradi mikubwa ya umeme.

“Serikali inatekeleza miradi mikubwa miwili ya umeme  inayojenga njia ya kusafirisha umeme na vituo vyake, mradi mmoja ni Bulyanhuru-Geita  ya njia ya kusafirishia ya msongo wa Kv 220 na mwengine Geita-Nyakanazi  wa msongo wa kV 220 miradi yote inatarajiwa kukamilika  mwakani ambavyo itakuwa ndio muarubaini wa tatizo la kukatika umeme,”alisema.

Vilevile,amelipongeza shirika la umeme Tanzani (TANESCO)kwa juhudi zake mbalimbali kwa kutatua changamoto za umeme zinazojitokeza mkoani huo.

Naye Mganga Mkuu wa kituo cha afya cha Bukiriro, Dkt Wilbroad Bukiriro, ameishukuru Serikali kwa kupeleka umeme kwenye kijiji hicho na kuwezesha kituo cha afya kupata umeme kituo ambacho kilikuwa hakina umeme tangu kilipoanzishwa mwaka 1977.

Ameeleza, kuwa kwasasa huduma mbalimbali zimeimarika katika kituo hicho cha afya hicho kwasababu ya upatikanaji kwa huduma katika kituo hicho.

Katika ziara yake hiyo, pia aliwasha umeme katika Shule ya Sekondari ya Muyenzi iliyopo kijiji cha Muyenzi, kata ya Lulenge,Wilaya ya Ngara na Shule ya Sekondari Nyakahuru,kijiji cha Mabale, kata ya Nyakahura.

 

No comments :

Post a Comment