Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mary Haule
akiwaelezea wananchi namna ambavyo mashine ya kusaidia kupumua
(ventilator) inavyotumika kwa wagonjwa waliolazwa katika chumba cha
uangalizi maalum (ICU) wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa
ya Dar es Salaam.Wataalam
wa maabara kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakipima vipimo
vya damu kwa ajili ya kuangalia magonjwa ya moyo kwa wananchi waliofika
katika banda hilo kwa ajili ya kupima afya zao wakati wa Maonesho ya 44
ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
**********************************
Wananchi
waliotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika
Maonesho ya Sabasaba wamevutiwa na uwepo wa chumba cha mfano cha
kuhudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) pamoja na mashine
maalum ya kupumulia ‘ventilator’.
Mashine hiyo
ndiyo ambayo hutumika kusaidia mgonjwa mwenye shida ya upumuaji kuweza
kupumua vema baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa ikiwemo upasuaji wa
moyo.
Mkazi wa
Buguruni, Said Abdallah alisema amefurahi kuona mashine hiyo kwa macho
yake, kwani hapo kabla alisikia kwenye vyombo vya habari ikielezwa
kwamba ni msaada mkubwa kwa watu wenye shida ya upumuaji.
“Katika kipindi
hiki cha Corona, nilisikia wakisema mashine ya ‘ventilator’ inasaidia
kuokoa maisha, sasa sikuwa nimewahi kuiona mashine hiyo, ndiyo maana leo
unaona nina furaha kubwa, nimeiona hapa kwenye banda la JKCI,
SABASABA,” alisema Abdallah.
Kwa upande wake
Afisa Uuguzi kutoka JKCI, Mary Haule akizungumza na waandishi wa habari
alisema wananchi wengi wamevutiwa na mashine ya ventilator na kuuliza
maswali mengi hasa namna gani mashine hiyo inaweza kusaidia kuokoa
maisha.
“Sabasaba ya
mwaka huu imekuwa ya tofauti katika banda letu tumeweka mfano wa chumba
cha ICU, tuna mfano wa binadamu (mdoli) na tumekuja na mashine hii ya
‘ventilator’ tunawaonesha wananchi jinsi tunavyomsaidia mgonjwa
aliyetoka katika chumba cha upasuaji na kuwekewa mashine hii kumsaidia
kupumua,” alisema Haule.
Aliongeza
“Mgonjwa tunayemuhudumia hapa anakuwa bado hajaamka kutoka kwenye dawa
ya usingizi, tunamsaidia mpaka hali yake itakapoimarika na kutoka
usingizini.
“Hivyo, tunatoa
ufahamu kwa wananchi waweze kuelewa kwamba katika Taasisi yetu tuna
kitengo cha kusaidia wagonjwa mahututi waliofanyiwa upasuaji na hapa
tumekuja tu na baadhi ya mashine kwa ajili ya maonesho, Lakini pale JKCI
tunazo zaidi ya mashine 20 za Ventilator, wananchi wamefurahi kuona
mfano wa chumba hiki,” alisema Haule
Wakati huo huo
Mariam Kaisa ambaye ni Mkazi wa Kiwalani alisema amepata elimu ya
kutosha katika banda la JKCI kuhusu lishe na umuhimu wa kufanya mazoezi
ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya moyo.
“Nimepima afya
yangu, nimeambiwa moyo wangu upo vizuri, nimeshauriwa kuzingatia kanuni
za afya hasa ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili nizidi kulinda
afya ya moyo wangu,” alisema Mariam.
No comments :
Post a Comment