Friday, July 10, 2020

13 mbaroni tuhuma za mauaji walinzi 4 mgodini


Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Kahama
JESHI la Polisi Mkoani Shinyanga limekamata watu 13 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya watu 4 yaliyotokea katika mgodi wa wachimbaji wadogo eneo la Tambalale Namba 4, Kijiji cha Wisolele, Kata ya Segese, Tarafa ya Msalala, wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.
Baadhi ya viroba vyenye mchanga wa Carbon yenye dhahabu ambayo ilikamatwa kufuatia Opresheni maalumu ya kuwasaka watuhumiwa wa mauaji ya walinzi wanne wa Mgodi wa dhahabu katika kijiji cha Wisolele wilayani Kahama. Taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao imetolewa mbele ya waandishi wa habari katika Kituo kidogo cha Polisi cha Bugarama wilayani Kahama na Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Opresheni Maalumu nchini, Mihayo Msikhela ambaye aliongoza opresheni ya kuwakamata watuhumiwa hao.
Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Opresheni Maalumu nchini, Mihayo Msikhela akionesha bunduki moja iliyokuwa imeporwa na watuhumiwa wa mauaji ya walinzi wanne wa Mgodi mdogo wa dhahabu wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga. (Picha na Suleiman Abeid) Kamishina Msikhela amesema waliokamatwa wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya walinzi 4 na kumjeruhi mmoja wao ambao wote walikuwa walinzi wa mgodi wa wachimbaji wadogo wa dhahabu ulioko katika Kijiji cha Wisolele, wilayani Kahama.
Walinzi waliouawa ni Juma Jigwasanya (42) mkazi wa Nundu Nyang’hwale, Lusajo Michael (31) mkazi wa Kata ya Tinde wilayani Shinyanga, Raphael Kipenya (27) aliyekuwa Mwendesha Mitambo, mkazi wa Katoro Geita na Daniel William (25) Msimamizi Mkuu wa Plant mkazi wa Geita.
Kamishina Msikhela alimtaja majeruhi katika tukio hilo kuwa ni Exavery Maulidi (21) aliyekuwa mwendesha mitambo katika mgodi huo na kwamba alinusurika baada ya kujeruhiwa kwa kugongwa ama kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani kisha kuwekwa pamoja na marehemu wakiamini amefariki.
‘Baada ya tukio, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi, lilianza msako wa kuwatafuta wahalifu hao katika msako huo tulifanikiwa kukamata wahalifu 13 na vielelezo mbalimbali, na baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo,” ameeleza Kamishina Msikhela.
Kamishina huyo ametaja vitu vilivyokamatwa katika opresheni hiyo kuwa ni pamoja na mchanga wenye carbon iliyonasa dhahabu viroba 7 ambavyo viliibwa siku ya tukio la mauaji ukiwa na uzito wa kilogramu 385.34 na makapi ya mchanga wa carbon viroba 7 vyenye uzito wa kilogramu 465.76.
Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Opresheni Maalumu nchini, Mihayo Msikhela akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo Pichani) ya kukamatwa kwa watuhumiwa 13 wa mauaji ya walinzi wanne katika Mgodi wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Wisolele wilayani Kahama mkoani Shinyanga (Picha na Suleiman Abeid) “Katika Opresheni yetu pia tulikamata pikipiki 5 zilizotumika kubebea mzigo wa mchanga, bunduki moja aina ya shot gun namba 9025817 ikiwa na namba za usajili TZCAR103855 ambayo iliibwa kutoka kwa mmoja wa walinzi waliouawa ikiwa na risasi mbili na kisha ilitelekezwa mita 400 toka eneo la tukio,” ameeleza Kamishina Msikhela.

No comments :

Post a Comment