1.0 UTANGULIZI
Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Usajili wa Laini za Simu) za mwaka 2020, yaani “The Electronic and Postal Communications (SIM Card Registration) Regulations, 2020”, zimeainisha katika Kanuni ya 18 kuwa:-
18 (1) Mtu anayehitaji kumiliki na kutumia laini ya simu ataruhusiwa kusajili:-
(a) Kama ni mtu binafsi
- Idadi ya laini moja kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kupiga simu za sauti, kutuma ujumbe mfupi pamoja na matumizi ya data;
- Idadi ya laini zisizozidi nne kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa matumizi ya mawasiliano kati ya mashine na mashine; na
(b) Kama ni Kampuni au Taasisi
- Idadi ya laini zisizozidi thelathini kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya kupiga simu za sauti, kutuma ujumbe mfupi pamoja na matumizi ya data;
- Idadi ya laini zisizozidi hamsini kwa kila mtoa huduma za mawasiliano kwa matumizi ya mawasiliano kati ya mashine na mashine.
- Laini zilizosajiliwa kwa matumizi yaliyoainishwa kwenye Kanuni 18 (1) (a) hazipaswi kutumiwa kwa kubadilishana (interchangebly).
- Bila kujali Kanuni ya 18 (1), Mtu binafsi, Kampuni au Taasisi inaweza kuruhusiwa kusajili na kumiliki laini zaidi ya zilizoainishwa kwa kuomba na kupata idhini kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
- Mtu yeyote atakayekiuka masharti ya Kanuni hizi, atakuwa ametenda kosa la jinai.
Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) inapenda kuutaarifu umma kwamba zoezi la kuomba idhini
ya umiliki wa laini za simu zaidi ya moja katika mtandao mmoja
linaendelea. Tunawashauri wamiliki wa laini za mawasiliano ya simu
kuendelea kuhakiki usajili wa laini zao zote wanazomiliki.
2.0 KUTHIBITISHA IDADI YA LAINI ZILIZOSAJILIWA KUTUMIA KITAMBULISHO CHA TAIFA (NIDA)
2.1 Kila mmiliki wa laini ya
simu anatakiwa kupiga namba *106# na kuangalia usajili wa laini
anazomiliki na endapo atakuta namba ambayo haitambui na imesajiliwa kwa
kutumia namba ya kitambulisho chake cha Taifa anashauriwa kuwasiliana na
mtoa huduma wake ili azifunge mara moja kuepusha matumizi mabaya na
kumsababishia usumbufu usiokuwa wa lazima utakaojitokeza.
2.2 Kwa wale ambao kwa sasa
wanamiliki laini zaidi ya moja katika mtandao mmoja, mwisho wa kuhakiki
laini zao itakuwa tarehe 31 Julai 2020.
2.3 Utaratibu wa kuomba idhini
ya kumiliki laini mpya za ziada katika mtandao mmoja unaendelea na
mteja anaweza kupata huduma hii kupitia kwa wakala au kwenye ofisi za
watoa huduma ambapo kwa kutumia njia za kielektroniki mtoa huduma
atawasilisha maombi ya mteja wake TCRA kwa idhini ya kusajili na
kumiliki laini za ziada; mteja atapokea majibu ya maombi yake ndani ya
takribani dakika tano.
3.0 URASIMISHAJI WA LAINI ULIZOTHIBITISHA
3.1 Urasimishaji wa laini za
ziada kwa sasa unaweza kufanyika kwa wakala au kwenye ofisi za watoa
huduma ambapo kwa kutumia njia za kielektroniki ambapo mtoa huduma
atawasilisha maombi yake ya idhini ya kurasimisha laini za ziada TCRA
na kupokea majibu ndani ya takribani dakika tano; au
3.2 Kwa kupitia namba *106#
ambapo wewe mwenyewe utaweza kuomba idhini ya kurasimisha kutoka TCRA
kupitia simu yako. Huduma hii ya kurasimisha kwa njia ya simu yako
itaanza kutumika rasmi Agosti 1, 2020.
No comments :
Post a Comment