Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevitoza faini ya Sh milioni 30 vyombo
vya habari sita, kwa kukiuka kanuni na maadili ya utangazaji ikiwamo
redio ya Clouds FM kuzungumzia supu ya pweza kuimarisha tendo la ndoa
katika muda ambao wasikilizaji wanaweza kuwa watoto.
Mbali
ya Clouds FM, vyombo vingine vilivyoadhibiwa ni East Africa Radio, na
televisheni za Star, Sibuka, na Global Tv na Duma Tv.
Akisoma
uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda alisema vyombo hivyo vilikiuka kanuni za
mawasiliano kwa nyakati tofauti.
Mapunda
alisema redio ya Clouds FM kupitia kipindi chake cha Jahazi,
walihamasisha vitendo vya ngono, kwa kutumia supu ya pweza katika
kuimarisha tendo la ndoa kwa muda ambao wasikilizaji wanaweza kuwa
watoto.
Alisema
baada ya kusikiliza utetezi wao, wanatozwa faini ya Sh milioni saba na
kupewa onyo kali baada ya kuwatia hatiani kwa kosa hilo.
Katika
shauri lingine, kituo cha Duma TV kimetozwa faini ya Sh milioni saba na
kufungiwa kuchapisha maudhui kwa muda wa mwezi mmoja ili wajipange na
kuzifahamu kanuni na kuzingatia weledi na maadili ya utangazaji.
Mapunda
alisema Duma ilikutwa na hatia ya kukiuka kanuni kwa kuchapisha na
kutangaza maudhui yenye lugha isiyo na staha na iliyo na udhalilishaji
wa kijinsia kwa wanaume na wanawake.
Alisema
redio ya East Africa imetozwa faini ya Sh milioni tatu na kupewa onyo
kali kwa kukiuka kanuni hiyo, kwa kurusha maudhui ya kukashifu utendaji
wa serikali kupitia uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na kutumia lugha ya kashfa dhidi ya utendaji wake.
Vilevile
Global Tv imetozwa Sh milioni saba na kupewa onyo kali, baada ya
kupatikana na hatia ya kuchapisha picha ya mnato na kutangaza maudhui
yasiyokuwa na lugha ya staha na yenye kushabikia vitendo vya mahusiano
ya kimapenzi ya jinsia moja.
Mapunda
alisema maudhui hayo, yangeweza kuwaumiza na kuwakwaza waumini wa
dhebebu la Anglikana na Watanzania kwa ujumla. Pia, alisema Sibuka Tv
inatozwa faini ya Sh milioni tatu baada ya kupatikana na hatia ya
kushabikia mauaji ya kutisha katika muda, ambao watoto wanaweza kuwa
sehemu kubwa ya watazamaji.
No comments :
Post a Comment