………………………………………………………………..
*Asema lengo ni kuendelea kujenga miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya watu
WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais
Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma
ili iweze
kuendelea na ujenzi wa miradi ya kimkakati zikiwemo bandari
kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi wake.
Pia, Waziri
Mkuu amesema changamoto ya usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya
Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itakuwa historia
baada ya kuboreshwa na kujengwa kwa miundombinu ya bandari katika wa
Ziwa Tanganyika ukiwemo upanuzi wa bandari ya Kasanga.
Waziri Mkuu
aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Julai 05, 2020) alipozungumza na
wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa
Bandari ya Kasanga iliyoko wilaya ya Kalambo akiwa katika ziara ya
kikazi mkoani Rukwa. Mradi huo unagharimu zaidi ya sh. bilioni 4.7.
Alisema
upanuzi wa bandari hiyo utawezesha mizigo inayotoka nchini kwenda Congo
kufika kwa wakati kwa sababu itasafirishwa moja kwa moja bila kupitia
katika nchi nyingine kama ilivyo sasa, ambapo madereva wanalazimika
kupita kwenye Mataifa mengine na kutumia muda mrefu.
“Mradi huu
ukikamilika utaongeza pato la mwananchi mmoja mmoja pamoja na Taifa kwa
ujumla. Rais Dkt. Magufuli amedhamiria kuboresha maendeleo ya wananchi
nchi nzima ikiwemo na wilaya hii ya Kalambo. Ujenzi wa miradi hii unatoa
fursa za ajira kwa wananchi, hivyo zichangamkieni.”
Vilevile,
Waziri Mkuu alisema mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa bado
yanaendelea nchini, hivyo mtu yeyote atakayebainika anajihusisha na
masuala hayo atafutwe popote alipo akamatwe na achukuliwe hatua za
kisheria kwa sababu rushwa ni adui wa haki.
Pia, Waziri
Mkuu aliendelea kuwakumbusha watendaji ndani ya Serikali wahakikishe
wananchi wanapofika katika maeneo yao ya kazi wawapokee, wawasikilize na
kuwahudumia bila ya ubaguzi. “Hatuangalii sura wala kabila yeyote
atakayekanyaga kwenye maeneo yenu ahudumiwe ipasavyo.”
Kwa upande
wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe
alisema Tanzania na Congo zimeungana kwa Ziwa Tanganyika, usafiri wa
barabara uliokuwa unatumika awali uliyalazimu maroli ya mizigo kupitia
nchini nyingine na kuchelewa kufika.
Alisema
kukamilika kwa upanuzi wa bandari hiyo pamoja na ujenzi wa barabara kwa
kiwago cha lami kutoka Sumbawanga hadi Kasanga kutarahisisha
usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kutumia bandari hiyo kuingia nchini
Congo moja kwa moja bila kupita kwenye nchi juirani.
Waziri
Kamwelwe alisema kuwa awali kulikuwa na changamoto ya barabara hali
iliyosababisha meli kufika kwenye Bandari ya Kasanga na kulazimika
kusibiri mizigo ambayo ilikuwa ikichelewa kufika kutokana na ubovu wa
barabara na sasa tayari Serikali imeitatua kwa kuijenga kwa kiwango cha
lami.
Awali, akitoa
taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Kaimu Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi, Mhandisi Thomas
Ngulima alisema mradi huo umeanzishwa ili kuongeza ushindani na tija
katika shughuli za kibandari kusini mwa Ziwa Tanganyika.
Alisema mradi
huo unahusisha upanuzi mkubwa wa gati ilililopo sasa lenye urefu wa
mita 20 lifikie mita 120, ambazo zitawezesha kuhudumia meli mbili hadi
sita kwa wakati. Kazi nyingine ni ujenzi wa miundombinu ya bandari
ikiwemo jengo la kupumzikia abiria, mgahawa na nyumba za watumishi.
Mhandisi
Ngulima alisema mradi huo unaojengwa na kampuni ya Inter-Consult Limited
umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi
Septemba, 2020 na kwamba utafungua na kuboresha njia ya biashara ya
mazao ya chakula katika nchi za DRC, Burudi na Zambia.
Aliongeza
kuwa, ujenzi wa barabara ya kimkakati inayoanzia Manispaa ya Sumbawanga
hadi Kasanga (km 107), pamoja na upanuzi wa bandari unaoendelea,
utawezesha mtiririko wa shehena za saruji, makaa ya mawe, chokaa na
sabuni kuongezeka hivyo kukuza uchumi wa wananchi na Taifa.
No comments :
Post a Comment