******************************
DAR ES SALAAM:
Tarehe 12 Julai, 2020: Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango, anatarajiwa kuongoza Mkutano wa Mawaziri wanaohusika na masuala
ya
Fedha na Uwekezaji wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) na Jopo la Mapitio ya Uchumi Mpana (Peer Review Panel)
unaotarajiwa kufanyika tarehe 15 Julai 2020 kwa njia ya mtandao
kutokea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNICC) Dar es salaam. Mkutano huu utatanguliwa na kikao cha Makatibu
Wakuu wa Wizara za Fedha na Benki Kuu wa SADC, utakaofanyika kwa siku
mbili kuanzia kesho tarehe 13-14 Julai, 2020.
Mkutano huu
ambao utawakutanisha Mawaziri wenye dhamana na masuala ya Fedha na
Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi 16 wanachama wa
SADC, utajadili masuala ya Fedha na Uwekezaji pamoja na kupokea taarifa
ya utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Mawaziri wa Fedha na
Uwekezaji katika mkutano uliofanyika mwezi Julai 2019, Windhoek,
Namibia.
Vilevile mkutano huu utajadili kwa kina na kutoa maamuzi ya kisera kuhusu athari za Kiuchumi na Kijamii za COVID-19.
Mkutano huu
ulipangwa kufanyika ana kwa ana kuanzia tarehe 13-17 Julai, 2020 lakini
kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na
virusi vya corona (COVID-19), utafanyika kwa njia ya mtandao kuanzia
tarehe 13 hadi 15 Julai, 2020 .
Mkutano huu ni
utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa
SADC uliofanyika tarehe 18 Machi 2020, Dar es Salaam ambapo pamoja na
mambo mengine, ulimuelekeza Mwenyekiti wa Baraza kwa kushirikiana na
Sekretarieti ya SADC kusimamia zuio la kufanyika kwa mikutano ya ana kwa
ana kutokana na mlipuko wa COVID-19.
No comments :
Post a Comment