Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
akizungumza na Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara mwishoni mwa wiki jijini
Dodoma wakati wa uwasilishaji Taarifa ya Utekelezaji wa kutoondolewa
vijiji 920 vilivyopo katika maeneo ya hifadhi. Wengine katika picha
kutoka kushoto Dkt Hamis Kigwangala (Waziri Maliasili na Utalii),
Suleiman Jafo (Waziri TAMISEMI), Omari Mgumba (Naibu Waziri Kilimo) na
Jumaa Awesu (Naibu Waziri Maji).
Sehemu ya Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara wakifuatilia uwasilishaji
Taarifa ya Utekelezaji wa kutoondolewa vijiji 920 vilivyopo katika
maeneo ya hifadhi uliofanywa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo
akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa kutoondolewa vijiji 920 vilivyopo
katika maeneo ya hifadhi mbele ya Wakuu wa mikoa ya Tanzania Bara
mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.Baadhi
ya Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara wakifuatilia uwasilishaji Taarifa ya
Utekelezaji wa kutoondolewa vijiji 920 vilivyopo katika maeneo ya
hifadhi uliofanywa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
mwishoni mwa wiki jijini Dodoma. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA
ARDHI)
***********************************
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasilisha taarifa ya
utekelezaji
maagizo ya kutoondolewa vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwa katika
migogoro maeneo ya hifadhi nchini kwa Wakuu wa mikoa wa Tanzania Bara.
Uwasilishaji
taarifa hiyo umefanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mary Makondo jijini Dodoma mwishoni mwa wiki na
kuhudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wataalamu
kutoka wizara za Ardhi, Ofisi ya Raisi TAMISEMI, Kilimo, Mifugo,
Maliasili na Utalii, Maji na Makamu wa Raisi ambazo Mawaziri wake
walitembelea maeneo yenye mgogoro na kuja na mapendekezo yaliyosababisha
Rais kuchukua uamuzi huo.
Awali wananchi
waliokuwa wakiishi kwenye vijiji vya hifadhi walionekana wavamizi wakati
serikali ilitoa hati za usajili kwa vijiji na wananchi wake kushiriki
shughuli mbalimbali zikiwemo za uchaguzi jambo lililomfanya Rais John
Pombe Magufuli kuchukua uamuzi wa kuvibakisha vijiji 920 baada ya kupata
ushauri wa mawaziri wa sekta husika.
Akizungumza
wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo kwa Wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo
alisema, utekelezaji maamuzi ya kutoondolewa vijiji 920 ni wa awali huku
kazi kwa vijiji 55 vilivyosalia ikiendelea ambapo alisema itahusisha
Wakuu wa mikoa, wilaya na wataalamu wengine.
Kwa upande wake
Waziri wa Ardhi William Lukuvi aliwaambia wakuu hao wa mikoa kuwa,
uwasilishaji taarifa ya utekelezaji maagizo yaliyofikiwa kuhusiana na
vijiji 920 unafanyika kwa kwa lengo la kuwafahamisha ni vijiji gani
vimefutwa na ipi ya kupunguzwa katika maeneo yao.
‘’kazi ya
kubakisha vijiji kwenye maeneo ya mgogoro katika hifadhi imeanza na
lengo hapa ni wananchi wasiishi kwa hofu na ninyi kama Wakuu wa mikoa
lazima mfahamishwe ili kujua ni misitu gani imefutwa na ipi
imepunguzwa’’ alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa
Lukuvi, wizara yake imeona ni wakati muafaka kuiwasilisha taarifa ya
utekelezaji maagizo hayo kwa wakuu wa mikoa kutokana na wao kuwa na
mamlaka katika maeneo yao na kuongeza kuwa pamoja na Wizara hiyo
kushughulika na migogoro kwenye maeneo ya hifadhi lakini itaendelea
kushughulikia migogoro mingine kwa utaratibu wa serikali.
Hivi karibuni
Waziri Lukuvi alisisitiza kufanyika uchambuzi wa kina wakati wa
utekelezaji maagizo hayo ili kuja majibu yatakayokidhi malengo ya uamuzi
uliofanyika ambapo alisema wakati kazi ya uchambuzi ikiendelea
wasimamizi wa sheria wanapaswa kuendelea kusimamia sheria na
kuwatahadharisha kuwa makini wakati wa utekelezaji majukumu yao ili
kuepuka uvunjifu wa amani.
Kwa muda mrefu
wananchi wa Vijiji 975 vilivyo katika hifadhi wamekuwa katika mgogoro
kwa kudaiwa kuwa wavamizi na kusababisha nyumba zao kuchomwa moto huku
baadhi yao wakiwa wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya miaka ishirini.
Mgogoro huo
ulisababisha Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati na kuridhia vijiji
920 kubaki maeneo ya hifadhi sambamba na kufutwa misitu ya hifadhi saba
yenye ukubwa wa ekari 46,715 ili ipangwe upya. Pia Rais Magufuli alifuta
mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na ardhi hiyo
kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, kilimo na shughuli za
ufugaji.
No comments :
Post a Comment