Mwenyekiti wa Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Hashim Kabanda, akisisitiza
jambo kwa waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya kikandarasi ya China
Railway 15 Group, ambao walipunjwa mishahara yao wakati wa ujenzi wa
Daraja la Mto Kilombero (Magufuli), wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
Mkuu wa Wialaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Ismail Mlawa akizungumza
na waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15
Group, ambao walipunjwa mishahara yao alipokuatana nao wilayani humo kwa
ajili kuhakiki malipo yao ili wapate stahili zao.
Waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya kikandarasi ya China Railway 15
Group, ambao walipunjwa mishahara yao wakati wa ujenzi wa Daraja la Mto
Kilombero (Magufuli), wakiwasiliza wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), waliofika wilayani hapo kwa
ajili ya kuhakiki malipo ya wafanyakazi hao ili kulipwa stahili zao.
Wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi), wakiwa na wawakilishi kutoka kampuni ya kikandarasi ya China
Railway 15 Group, wakihakiki taarifa za malipo ya waliokuwa wafanyakazi
wa kampuni hiyo, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Wataalamu
kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
wakihakiki majina na malipo ya wafanyakazi ya waliokuwa wakiidai kampuni
ya kikandarasi ya China Railway 15 Group, wilayani Kilombero, mkoani
Morogoro.
*******************************
Serikali imeendesha zoezi la
malipo kwa waliokuwa wafanyakazi zaidi ya 250 wa kampuni ya
kikandarasi
ya China Railway 15 Group ambao walipunjwa mishahara yao wakati wa
ujenzi wa daraja la Magufuli (Kilombero), mkoani Morogoro, mara baada ya
uhakiki wa taarifa zao kukamilika.
Akizungumza wakati wa
uendeshaji wa zoezi hilo, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro,
Mwenyekiti wa timu ya uhakiki wa madai ya malipo hayo kutoka Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Hashim
Kabanda, amesema kuwa zoezi lilikuwa na mafanikio makubwa kwani kila
mfanyakazi aliyekuwa anastahili kulipwa amepata haki yake kama
ilivyohakikiwa na jopo la wataalamu hao kwa kushirikiana na wawakilishi
wa mkandarasi huyo.
“Tunashukuru kwa kukamilisha
zoezi hili kwani haikuwa kazi rahisi kama ambavyo watu wanafikiri,
changamoto zilikuwa nyingi zikiambatana na lawama ambazo baadae
zilitafutiwa ufumbuzi na hatimaye madai ya wafanyakazi hawa tumeyamaliza
leo”, amesema Mhandisi Kabanda.
Aidha, Kabanda ametaja
changamoto mbalimbali walizokutana nazo ikiwemo baadhi ya majina
kujirudia na mengine kukosewa ambapo awali orodha iliyowasilishwa kwa
Kamishna wa kazi ilikuwa na idadi ya wadai 269 na mara baada ya uhakiki
huo idadi ilipungua hadi kufikia 252 ambao kati yao wadai 242
walijitokeza na kulipwa na waliobaki hawakujitokeza.
Sambamba na hilo, wakati zoezi
hilo likiendelea liliibuka kundi jingine la wadai ikiwemo walinzi na
wafanyakazi wengine ambao walilalamika kuwa nao walipunjwa mishahara yao
na kampuni hiyo hali iliyopelekea Mwenyekiti huyo kuwasilisha madaia
yao kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero ili yashughulikiwe kwa
taratibu stahiki na hatimaye kupata haki zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Kilombero, Ismail Mlawa, amesema kuwa Serikali ipo kwa ajili
ya wananchi, hivyo kundi jingine la walinzi ambalo limejitokeza nalo
lifuate utaratibu kama waliofanya wenzao ili nao waweze kushughulikiwa
madai yao na hatimaye kupata haki zao.
“Sisi kama Serikali tupo kwa
ajili ya wananchi, hakuna kulalamika, mnachotakiwa kufanya ni kufuata
maelekezo mnayoambiwa ili msaidiwe kama ambavyo wenzenu wamefanya, na
mimi naahidi kuwa sambamba nanyi ili tujue hatma ya hili”, amesema Mkuu
wa Wilaya.
Naye, Mwenyekiti wa
wafanyakazi wa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero Bw. Alex Ndagaro,
ameeleza kuwa mwaka 2013 waligundua kuwa walikuwa wanapunjwa mishahara
yao ukilinganisha na viwango vya Serikali vilivyowekwa kwa malipo ya
siku hivyo wakaamua kupeleka malalamiko yao Serikalini ili kupata
stahili zao.
“Tunashukuru Serikali kwa
jitihada zao zote za kukubali kuwasimamia wananchi wake na kwa kumbana
mkandarasi alipe madai ya wafanyakazi wake, hii ni Serikali sikivu na ya
wanyonge, hakika tunampongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na
timu nzima ya Sekta ya Ujenzi”, amesisitiza Mwenyekiti huyo.
Madai ya mapunjo ya mishahara
ya wafanyakazi hao yaliibuka mnamo mwezi Mei 2015, baada ya Ofisi ya
Kazi Mkoa wa Morogoro kupokea malalamiko ya Wafanyakazi dhidi ya
Mkandarasi huyo kupitia Ofisi ya Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa
Morogoro.
No comments :
Post a Comment