Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe
akizungumza na wamiliki wa viwanda vinavyozalisha saruji (pichani)
kuhusu changamoto za bei ya saruji katika maeneo mbalimbali nchini,
mkutano huo ulifanyika katika Eneo huru la Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje ya
Nchi (EPZA), Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda
na Biashara, Prof.Riziki Shemdoe akizungumza na wamiliki wa viwanda
vinavyozalisha saruji (hawapo pichani) kuhusu changamoto za bei ya
saruji katika maeneo mbalimbali nchini, mkutano huo ulifanyika katika
Eneo huru la Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje ya Nchi (EPZA), Jijini Dar es
Salaam.
Picha na Idara ya Habari-MAELEZO.
****************************
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na
Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, leo Julai 17, 2020 amekutana na
wazalishaji wa Saruji nchini kujadili changamoto ya bei na upatikanaji
wa bidhaa hiyo ambapo amewataka kuongeza uzalishaji katika viwanda vyao.
Akizungumza Katika kikao hicho
kilichofanyika ukumbi wa Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje ya Nchi
(EPZA) Ubungo External jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu alisema kuwa
sababu kubwa iliyofanya bidhaa ya saruji kupanda bei ni pamoja na kuwepo
kwa mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha maeneo mbalimbali nchini.
“Katika Mkutano huu changamoto
zilizoelezwa na wazalishaji wa viwanda vya saruji nchini ambapo
imesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ni pamoja na Mvua kubwa
iliyokuwa ikinyesha nchini nzima katika kipindi cha mwezi Machi, Aprili
na Mei ambapo iliathiri zaidi uzalishaji na usafirishaji wa Saruji”,
Alisema Prof.Shemdoe
Aidha, Prof Shemdoe alisema kuwa
changamoto ya mlipuko wa Ugonjwa wa Corona (COVID 19) ambapo iliathiri
uzalishaji kutokana na kukosekana kwa vipuli vya mitambo inayotumika
katika shughuli hiyo kwani huagizwa kutoka nje ya nchi.
Alibainisha kuwepo kwa upungufu wa
bidhaa hiyo kutokana na Serikali kutekeleza miradi mikubwa inayoendelea
nchini kama vile barabara za kisasa, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR),
Ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha umeme (JNHPP) na ujenzi wa hospital
mbalimbali hapa nchini, pia ujenzi wa mji wa Serikali na Ikulu mpya ya
kisasa jijini Dodoma na ujenzi wa nyumba mpya za wakaazi jijini Dodoma.
Katika kikao hicho Prof. Shemdoe
ametoa rai kwa wazalishaji wa Saruji kuongeza uwekezaji na uzalishaji
katika bidhaa hiyo ambapo kwa sasa ni muhimu kwa kuwa Serikali
inatekeleza miradi mbalimbali ambayo inahitaji saruji kwa wingi.
Aliongeza kuwa wazalishaji kwa
sasa wanapaswa kuangalia fursa katika ujenzi wa miradi hiyo mikubwa na
kujenga viwanda ili kuepusha gharama za usafirishaji wa saruji kufika
katika maeneo ya ujenzi wa miradi, pia aliwashukuru kwa kuitikia wito
wa Serikali na kujadili hatma ya kuondoa kero ya kupanda kwa gharama na
upatikanaji wa Saruji.
“Kikao hiki kimetoa mwongozo mzuri
wa mwendelezo wa ushirikiano baina ya wawekezaji na Serikali katika
kutatua changamoto mbalimbali kwani kitendo cha wenye Viwanda kuridhia
kwa pamoja kuongeza uzalishaji kufikia kiwango kilichokuwa awali pia
kutokupandisha bei kitasaidia bei kushuka na Saruji kupatikana kwa wingi
ndani ya muda mfup”, Alisema Prof.Shemdoe.
Nao Wawekezaji na Wazalishaji
Saruji nchini wamepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Wizara ya
Viwanda na Biashara kwani imekuwa muhimili wa kuwaweka pamoja
kuwasikiliza na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo na wamesema wapo
tayari kushirikiana na Serikali katika kuboresha uchumi wa Nchi na
Maisha ya Watanzania.
No comments :
Post a Comment