Viongozi wa NSSF, VETA, Benki ya Azania, SIDO, na NEEC,
wakisaini mpango unaoitwa ‘SANVN Viwanda Scheme’ Machi 9 mwaka huu, unaowezesha
wajasiriamali wa SMEs nchini waanzishe viwanda, kukuza ujuzi na kutafuta
masoko. (Picha ya mtandaoni)
Na Christian Gaya, Majira Ijumaa 17 Julai 2020
UTAFITI unaonesha kwamba sekta ya
viwanda inaendelea kuwa na tija kuwezesha ongezeko pato la taifa, na viwanda
vidogo, vya kati na vikubwa kuongezeka.
Pato la taifa kutokana na sekta ya
viwanda mwaka 2019 ilikuwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na...
asilimia 8.05 mwaka
2018, sawa na ongezeko la asilimia 0.45,
matokeo ambayo ni akisi ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji
viwandani katika kipindi hicho.
Pia, inaonesha kwamba thamani ya
uzalishaji bidhaa viwandani kwa mwaka 2019 iliongezeka hadi shilingi trilioni
10.2 ikilinganishwa na shilingi trilioni 9.6 mwaka 2018, sawa na kasi ya ukuaji
kwa asilimia 5.8.
Vile
vile, kwa mujibu wa tathmini ya Sekta ya Viwanda na Biashara Ndogo na Biashara ya
Kati (SMEs) ya mwaka 2013, sekta isiyorasmi ilichangia asilimia 39.7 ya pato la taifa mwaka 2010.
Aidha
ilikadiriwa kwamba zipo SMEs milioni 3
zinazoajiri wananchi milioni 5.2.
Mafanikio hayo ndiyo yaliyoshawishi Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) washirikiana na taasisi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Benki ya Azania, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuanzisha mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi
Lengo la mpango huo ni kwa ajili ya kutatua changamoto za upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya SMEs nchini unaitwa SANVN KIWANDA SCHEME.
Mpango huo ni kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wakati wenye viwanda wanaojishughulisha katika mnyororo wa kuchakata mazao ya kilimo, unaowezesha kuongeza thamani kwa bidhaa zitokanazo na sekta hiyo.
Mpango huu wa uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati, lengo lake lingine ni kwa ajili ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa ujuzi, masoko na mitaji kwa miradi ya SMEs nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NSSF William Erio
anasema tayari NSSF wametenga jumla ya shilingi bilioni tano zitakazotolewa
kupitia Benki ya Azania, ambayo ndiyo itakuwa na jukumu la kukopesha
wajasiriamali wadogo na wa kati.
“Kiasi hicho cha shilingi bilioni tano ni kianzio
tu ambapo Mfuko wa NSSF utakuwa na uwezo kuongeza fedha zingine kulingana na
mahitaji na ufanisi wa kazi wa awamu hii ya kwanza wa uendeshaji wa viwanda
hivyo vidogo na vya kati,” anasema.
Mikopo kwa ajili ya
uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati kupitia Benki ya Azania ambapo NSSF
imewekeza hela kwenye benki hiyo. Wanufaika wa mikopo hiyo wanatambulika kupitia
za taasisi za VETA na SIDO
NEEC ndio msimamizi Mkuu
katika utekelezaji wa mikopo hiyo kwa wananchi ambao wamewekeza kwenye viwanda
vidogo na vya kati.
Wajasiriamali na wahitimu wa ufundi stadi nchini
wana fursa ya kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu baada ya taasisi tano
nchini kuungana kwa pamoja kuwezesha wananchi kuanzisha viwanda.
Erio anafafanua zaidi kuwa taasisi hizo
zilizounganisha nguvu na NSSF, VETA, SIDO, NEEC na Benki ya Azania, zimesaini
kwa pamoja Makubaliano ‘MoU’ ya kushirikiana pamoja kuwawezesha wananchi
kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.
“Muunganiko huo umelenga hasa kuunga mkono juhudi
za serikali ya awamu ya tano za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa
kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya kushiriki kwa njia moja au nyingine
Erio,”anasisitiza.
Anasema katika makubaliano hayo VETA itahakikisha
inatoa ujuzi unaostahili kwa wananchi kulingana na viwanda husika, na
itasimamia vyema zoezi la kutambua wajasiriamali hao.
Kwamba, pia itakuwa na majukumu ya kusimamia
miradi iliyopata mikopo kupitia kwake na kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu
kwa wajasiriamali ili kuwasaidia kuboresha miradi yao na kuendesha uzalishaji
kwa tija na ufanisi zaidi.
Na kwa upande mwingine katika makubaliano hayo,
SIDO na VETA kwa pamoja zitakuwa na jukumu la kuwatambua, kuwajengea uwezo na
kuwapendekeza wajasiriamali kwa ajili ya mikopo itakayotolewa kupitia Benki ya
Azania, wakati NEEC itakuwa ndiyo yenye dhamana ya uwezeshaji wananchi,
Akifafanua kuhusu mikopo na utaratibu wake, Afisa
Matekelezo (Uwekezaji) NSSF, John Sikoni, anasema ya kuwa kiwango cha mikopo
kwa mjasiriamali mdogo kitaanzia shilingi milioni 8 hadi shilingi milioni 50 na
kiwango cha kati ni kilicho juu ya shilingi milioni 50 hadi shilingi milioni
500 kwa wajasiriamali wa kati.
Anasema kuwa hii ni fursa ya kipekee kwa
watanzania wote wenye nia ya kuanzisha viwanda kujitokeza kwa wingi ili kuweza
kutambuliwa ili watakaokidhi vigezo waweze kupata na kunufaika na mikopo hiyo
yenye masharti nafuu
Mpango huo umeainisha namna bora ya
kisanyansi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo la kukuza mitaji na
kuimarisha vyanzo vyao vya mapato na kukuza akiba na mikopo.
Mpango huu unajikita kuwafika
wananchi wote bila ubaguzi na matabaka ya aina yoyote kwa kuzingatia vigezo na
masharti nafuu yaliyopo katika mfumo huu kwa kuvunja matabaka baina ya makundi
mbalimbali katika jamii na kutoa fursa sawa kuanzia mtu binafsi hadi vikundi
katika kuwapatia mitaji na ujuzi sawa.
Kupitia mkakati huo wa uendelezaji viwanda, NSSF utanufaika
kwa kupata wanachama zaidi na hatimaye kuongezeka kwa michango kwa sababu ajira
za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika mnyororo mzima wa
thamani wa sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi zitaongezeka.
Kwa mzunguko huo itasaidia NSSF iwe na afya zaidi na kuwa endelevu,
kwa kuwekeza kwenye vitega uchumi vyenye kuleta faida na kuchangia
masuala ya kijamii, na kutawanya uwekezaji na hatimaye kupunguza changamoto mbalimbali zinazokabili
jamii kutokana na ongezeko la wasio na ajira nchini.
Mpango umejikita katika kuhakikisha kuwa wajasiriamali
wanasaidiwa kuongeza ujuzi, kupata uzoefu na kuwawezesha kuhimili ushindani
katika masoko ya ndani na nje.
Kwa upande mwingine mpango huu pia unalenga kuwezesha viwanda
kupata vifaa vya kisasa kama mitambo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji ili
uwe na tija, kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kupanua shughuli za uzalishaji
pamoja na kuongeza kinga za hifadhi za jamii kwa wajasiriamali nchini
ambayo mpaka sasa ni asilimia 6.5 ya nguvukazi ndiyo inayonufaika na matunda
yatokanayo na kuwa na mifuko ya hifadhi ya jamii Tanzania.
No comments :
Post a Comment