Friday, July 17, 2020

UNDP yaipongeza Tume kwa ukuzaji wa haki za binadamu nchini


Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bibi Christine Musisi akimkabidhi Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (mstaafu) Mathew Mwaimu mojawapo ya vifaa vilivyotolewa kama msaada.
Jaji (mstaafu) Mwaimu akitia saini nyaraka za makabidhiano ya vifaa vilivyotolewa msaada na UNDP.
Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bibi Christine Musisi akitoa neno wakati wa hafla hiyo muda mfupi kabla hajakabidhi msaada huo kwa Mwenyekiti wa Tume.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (mstaafu) Mathew Mwaimu (katikati) na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bibi Christine Musisi (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi na maafisa wa THBUB na UNDP.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (mstaafu) Mathew Mwaimu akitoa neno la shukrani baada ya kupokea  msaada wa vifaa kutoka UNDP.
************************************
SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limetoa pongezi kwa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa hatua inazochukua kulinda na kukuza haki za binadamu na misingi ya utawala bora hapa nchi.

Vilevile Shirika hilo limeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kufanikisha nchi kufikia uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025 na kupunguza maambukizi ya virus vya corona vinavyosababisha gonjwa hatari la COVID-19.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma Julai 16, 2020 na Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Bibi Christine Musisi wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vyenye thamani ya TShs. Millioni 160,000 kwa Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Jaji (Mstaafu) Mathew Mwaimu.
Mwakilishi Mkazi huyo alisema kuwa UNDP inatambua mchango wa THBUB hapa nchini katika kulinda na kukuza haki za binadamu, ndiyo maana shirika hilo limetoa msaada huo ili kuunga mkono juhudi hizo za Tume.
Pia alisema kuwa: “Sisi UNDP tunaipongeza Serikali ya Dkt. Magufuli kwa jitihada ilizofanya na kupelekea Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za uchumi wa kati, kabla ya 2025 kama ilivyokuwa ikitarajiwa’’.
Aidha, Bibi Musisi aliongeza kuwa: “Kwa kweli tunaipongeza Serikali chini ya Dkt. Magufuli kwa kufanya jitihada kubwa ya kupunguza maambukizi ya virusi vya corona, jambo ambalo limeonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.’’
Kwa hali hiyo, Mwakilishi Mkazi huyo alisema kuwa UNDP itaendelea kuiunga mkono THBUB na Serikali ya Tanzania katika hatua zinazochukuliwa za kuendeleza na kuimarisha haki za binadamu na kuleta maendeleo nchini.
                                                   
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji (Mstaafu) Mwaimu ameishukuru UNDP kwa msaada huo, kwani anaamini vifaa hivyo vitawawezesha watumishi wa Tume kufanyakazi zao kwa ufanisi mkubwa na hivyo changia kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo.
‘’Ninaishukuru UNDP kwa msaada huo, na kwa ushirikiano waliouonesha kwetu, hivyo tunawaahidi vifaa hivyo vitaenda kutumika kama ilivyokusudiwa,’’ Mwenyekiti huyo amesema.

No comments :

Post a Comment