Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu wa Hazina wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Hazina
na Magavana wa Benki Kuu za Jumuiya hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
*************************************
Na Farida Ramadhani, Dar es Salaam
Nchi za Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimeshauriwa kuunganisha
nguvu
zao kupambana na changamoto ya utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa
makundi ya kigaidi zinazotishia usalama na kuharibu uchumi wa nchi hizo
.
Ushauri huo
umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mwenyekiti wa
Maafisa Wandamizi wa HAZINA wa SADC, Bw. Doto James wakati akifungua
Kikao cha Maafisa Waandamizi (Makatibu Wakuu) wa HAZINA na Benki Kuu wa
nchi wanachama wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao kutokea katika
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza
katika kikao hicho, Bw. James ambaye ni Mwenyekiti wa kikao hicho
kitakachofanyika kwa siku mbili, alisema kuwa changamoto
hiyo imesababisha baadhi ya nchi wanachama kuingia katika orodha ya nchi
zilizo kwenye athari ya kuingia kwenye vikwazo vya kimataifa kwa
kushindwa kutimiza vigezo na masharti ya Kikosi cha Masuala ya Fedha
(Financial Action Task Force), hali iyonaweza kuathiri malengo ya
jumuiya ya kuvutia uwekezaji.
Alisema licha ya
kuwepo kwa changamoto hiyo na nyingine kadhaa za kijamii, kimazingira na
kiuchumi Jumuiya hiyo imeendelea kutekeleza azma yake ya kufikia
malengo ya maendeleo iliyojipangia kupitia Mkakati Elekezi wa Maendeleo
wa SADC hali inayoashiria kuwa Jumuiya hiyo ni imara kutokana na kuwepo
kwa sera nzuri na mifumo mizuri wa kitaasisi ndani ya Jumuiya hiyo.
“Pamoja na
mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana kwa miaka ya hivi karibuni, baadhi
ya nchi wanachama zimeendelea kukabiliana na changamoto nyingine katika
sekta za uchumi ikiwemo ukuaji mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya
bajeti na hii changamoto mpya ya ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na
virusi vya corona”, alisema.
Bw. James alisema
katika kikao hicho Makatibu Wakuu hao watajadili na kutoa mapendekezo
ya ajenda mbalimbali za masuala ya fedha na uwekezaji kwenye nchi
za SADC ikiwemo athari za Kiuchumi na Kijamii zinazotokana na mlipuko wa
ugonjwa wa COVID-19 yatakayowasilishwa kwenye Mkutano wa Kamati ya
Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu wa SADC
utakaofanyika tarehe 15 Julai, 2020
Alisema kuwa
Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji, pamoja na mambo mengine,
wanajukumu la kusimamia itifaki ya Fedha na Uwekezaji katika Jumuiya ya
SADC kwa lengo la kuhakikisha Sera na Maamuzi ya Baraza la Mawaziri wa
SADC kwenye masuala yanaohusu Fedha na Uwekezaji vinatekelezwa.
“Ili kukabiliana
na athari hizo, ni vema nchi wanachama kutumia mifumo ya kitaasisi
katika kutafuta njia mbadala zenye ubunifu ili kuharakisha hatua za
kuimarisha uchumi ndani ya jumuiya yetu, ni matumaini yangu kuwa kikao
hiki ni njia muafaka katika kujadili changamoto za kiuchumi na kutoa
mapendekezo ya kitaalam yatakayowasilishwa katika Mikutano ya Kamati ya
Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu kama
ilivyoanishwa katika agenda za mikutano hiyo”, alisema Bw. James.
Alizitaja ajenda
nyingine watakazo jadili na kutoa mapendekezo kuwa ni kupitia taarifa
ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano uliopita wa Kamati ya Mawaziri wa
Fedha na Uwekezaji uliofanyika Windhoek, Namibia mwezi Julai 2019,
kupokea na kujadili taarifa ya hatua iliyofikiwa ya namna uendeshaji wa
Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC (SADC Regional Development Fund)
na kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maandalizi ya Miradi ya
Maendeleo wa SADC (Project Preparation Development Facility).
Viongozi hao
pia watajadili na kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa katika uanzishaji
wa Mfuko Maalum wa Kugharamia Miradi ya Muundombinu ya Usafirishaji wa
Nishati ya Umeme (Regional Transmission Infrastructure Financing
Facility – RTIFF) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, kupitia taarifa ya
maendeleo ya Sekta ya Fedha ya Magavana wa Benki Kuu nakupitia taarifa
ya utekelezaji wa masuala ya udhibiti wa fedha haramu.
Mkutano wa Kamati
ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu wa SADC
unaondaliwa katika kikao hicho ulipangwa ufanyike kuanzia tarehe 13 hadi
17 Julai, 2020 lakini kutokana na mlipuko wa COVID-19, mkutano
huu utafanyika kwa njia ya mtandao kama ilivyoelekezwa katika Mkutano
wa dharura wa Baraza la Mawaziri wa SADC uliofanyika tarehe 18 Machi
2020, Dar es Salaam.
No comments :
Post a Comment