………………………………………………………………..
Na Grace Semfuko, Dar Es Salaam
Mkurugenzi Mpya wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt Maduhu Issac Kazi amesema ubunifu, nidhamu na
kujituma ndio njia pekee ambayo itakifanya kituo hicho kuleta ufanisi
katika kazi masuala ambayo amepanga kuyasimamia.
Dkt Kazi aliyasema hayo alipokuwa
akizungumza na Viongozi na Wafanyakazi wa TIC Julai 13, 2020,
aliporipoti rasmi kwenye kituo chake kipya cha kazi alichopangiwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli Julai 12
mwaka huu.
“Kwa uwezo wangu nitakuwa
nahamasisha zana ubunifu, kujituma na nidhamu, Kituo cha Uwekezaji
Tanzania-TIC imekuwepo muda mrefu, kina tamaduni zake na tuziishi
tamaduni hizo, yaani kwamba ukiongea na mtu au watu lazima waseme huyu
anatoka TIC” alisema Dkt Kazi.
Alisema kutokana na Tanzania
kuingia kwenye nchi ya uchumi wa kipato cha kati, wafanyakazi wa kituo
hicho hawana budi kuendana na kasi ya hatua hiyo kwa kufanya kazi kwa
bidi na nidhamu, ili kufanikisha adhma ya Serikali ya utendaji kazi
wenye viwango.
“Nchi yetu imeingia katika uchumi
wa kipato cha kati, ni hatua kubwa sana, sote tunafahamu kuwa tumefikia
hatua hiyo miaka mitano kabla ya wakati tuliojiwekea, kwa hiyo tuchape
kazi na utendaji wetu lazima ubadilike uendane na uchumi huo, ili hata
aina ya wawekezaji tulionao wajiweke tofauti na wale tuliowazoea wakati
tukiwa kwenye kipato cha chini, tunatakiwa tujiongeze ili tuendane na
hatua ya uchumi huo”alisema.
Alisema ni ushirikiano tu ndio
utawezesha kufikia mafanikio ya utendaji kazi wa Kituo hicho na kuzitaka
taasisi zinazoshirikiana na TIC kufanikisha uwekezaji, kuboresha na
kuimarisha mifumo ya utendaji kazi wao.
“Kikubwa ni kwamba tuchape kazi,
tushirikiane na kama kuna changamoto zozote tuendelee kuwasiliana, hiki
chombo ni mtambuka, yaani ni kwamba humo ndani kuna taasisi mbalimbali
ambazo zinashirikiana,mfano TRA, BRELA, OSHA na nyinginezo,naomba tuwe
kitu kimoja kwa lengo la kuisaidia TIC na wakati huo huo, mtimize
wajibu wenu kwenye taasisi zenu mlizotoka” alisema Dkt Kazi.
No comments :
Post a Comment