Balozi
wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regina Hess akifuatilia huduma
zinazotolewa katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
alipotembelea banda hilo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam. Kushoto ni Daktari kutoka JKCI Pedro
Pallangyo.
Daktari
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo
akimwelezea Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
Bernard Konga mwitikio wa wananchi kufanya uchunguzi wa afya ya mioyo
yao katika banda la JKCI wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam.
Huduma
mpya kabisa ya kutibu tatizo la mfumo wa umeme ulioharibika kwa njia ya
kisasa zaidi inatarajiwa kuanza kutolewa katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI), kati ya kipindi cha kuanzia mwezi Agosti hadi Oktoba,
mwaka huu.
JKCI
hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ili kuanza kutoa
huduma hiyo baada ya kupatiwa na Serikali kiasi cha Sh. bil 4.3 kwa
ajili ya kusimika mitambo pamoja na kuanzisha chumba kingine cha tatu
cha upasuaji.
Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi aliweka wazi hayo hivi karibuni
alipozungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonesho ya 44
ya Biashara ya Kimataifa (SABASABA) ambako JKCI inashiriki kutoa huduma
ya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo pamoja na elimu kwa wananchi
jinsi ya kuepukana na magonjwa hayo.
“Maandalizi
yanakwenda vizuri, tunatarajia kati ya Agosti hadi Oktoba, mwaka huu,
pale JKCI tutaanzisha huduma mpya kabisa, mfumo wa umeme unapoharibika
tutakuwa tunaweza kuingia ndani ya moyo, tukatizama sehemu
zilizoathirika na kuziunguza ama kuzifanyia marekebisho,”
“Huduma
hiyo kitaalamu inaitwa ‘Electrophysiology studies’ ni huduma ambayo
haijawahi kutolewa hapa nchini na maandalizi ya kuanzisha chumba cha
tatu cha upasuaji nayo yanakwenda vyema” alisema Prof. Janabi.
Aliongeza
“Hapa SABASABA hii ni mara ya nne JKCI tunashiriki, mwaka jana tulipata
zawadi ya kuwa banda lililotoa huduma bora kwa upande wa huduma za afya
SABASABA.
“Mwaka
jana banda letu lilikuwa dogo, mwaka huu tumeongeza karibu mara mbili
na nusu, tangu tumeanza hadi sasa namba ya watu tulioona imeongezeka.
Tumeona zaidi ya watu 1,000 na takribani watu 370 tumewakuta na
Shinikizo la Juu la Damu na walikuwa hawajijui hali zao hapo kabla.
“Tumewapa
rufaa kuja kwenye taasisi yetu kwa matibabu zaidi, katika banda letu
tunavyo vifaa ikiwamo kipimo cha Electoral Cardiograph (ECG), tunao
madaktari wa chakula kwa wanaohitajika kupunguza uzito, wanapewa elimu.
“Yupo
daktari wa nasaha anatoa elimu kwanini mtu asiache kunywa dawa na pale
zinapomsumbua nini cha kufanya, tunao madakrari bingwa wa udhamiri wa
magonjwa ya moyo nikiwamo mimi mwenyewe.
“Tunaonesha
pia vifaa kadhaa vinavyotumika wakati wa upasuaji, tunavyo vile
tunavyotumia kusimamisha moyo pale inapohitajika kufanya marekebisho
wakati tunafanya upasuaji,” alisema Prof. Janabi.
Aliongeza
“Tunajaribu kuwaeleza wananchi waelewe, pia tulipata mgonjwa mmoja hapa
Sabasaba ambaye amehangaika kutafuta matibabu, tulipompima kipimo cha
Echo Cardiograph (ECHO) tuligundua moyo wake unafanya kazi chini ya
kiwango cha asilimia 30.
“Ikiwa
tusingemgundua hapa maana yake angeendelea kuhangaika na kutumia fedha
nyingi kujitibu, kutokana na hali yale pale JKCI tunacho kifaa
kinachoitwa CRTD ambacho tunaweza kumpandikiza na akaimarika afya yake
na kuendelea na maisha yake kama kawaida,” alisema.
Alisema
bila kupepesa maneno JKCI imekuwa na mchango mkubwa kwenye tiba ya
magonjwa ya moyo ndani ya nchi na katika nchi jirani zinazotuzunguka.
“Zanzibar, Malawi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wote hawa huduma kama zetu hawana, tunawahudumia hapa JKCI.
“Rwanda
tulipeleka timu yetu mbayo ilikaa wiki nzima na kafanya upasuaji kwa
wagonjwa 25, hii yote tunaishukuru Serikali kwa sababu imekua pamoja
nasi katika kila hatua ya kuimarisha huduma za matibabu ya moyo hapa
nchini,” alisisitiza.
No comments :
Post a Comment