Mkuu
wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Julius Kadawi
akitoa taarifa kuhusu kujiunga na mafunzo ya JKT mujibu wa sheria mwaka
2020 kwa vijana waliohitimu
kidato cha sita katika shule za Tanzania
Bara, Taarifa hiyo ameitoa leo Makao Makuu ya Jeshi hilo Wilayani
Chamwino Mkoani Dodoma Julai 16, 2020.
**************************************
Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
limetangaza majina ya vijana waliohitimu kidato cha sita kutoka shule
zote za Tanzania Bara waliochagulwa kujiunga na mafunzo ya Jeshi hilo
kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2020 .
Akizungumza leo Julai 16, 2020
Makao Makuu ya Jeshi hilo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, Mkuu wa
Tawi la Utawala, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Julius Kadawi
amesema kuwa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge anawakaribisha
waliochaguliwa kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo,
umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha , utayari wa kulijenga
na kulitumikia Taifa kupitia mafunzo hayo.
“Orodha kamili ya majina ya vijana
waliochaguliwa, maeneo ya makambi ya JKT waliyopangiwa na vifaa
wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz”, Alisisitiza Kanali Kadawi.
Aidha, Kanali Kadawi amesema kuwa
vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia tarehe 24 hadi 27
Julai, 2020 ambapo mafunzo yatafunguliwa rasmi Agosti 1, 2020.
Akifafanua, Kanali Kadawi amesema
kuwa kwa upande wa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho
(Physical disabilities) wanatakiwa kuripoti katika kambi ya JKT Ruvu
iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu
wa jamii hiyo.
“Kutokana na Ugonjwa wa Homa kali
ya Mapafu (COVID -19) nchini, Tahadhari za kuzuia maambukizi ya ugonjwa
huo kama ilivyoelekezwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya zitazingatiwa
kwa kipindi chote vijana watakapokuwa katika mafunzo”, Alisisitiza
Kanali Kadawi
Vijana waliochaguliwa wamepangiwa
katika kambi za JKT Rwamkoma- Mara, JKT Msange- Tabora, JKT Ruvu-Pwani,
JKT Mpwapwa Dodoma, JKT Mafinga- Iringa, JKT Mlale-Ruvuma, JKT Mgambo
na JKT Maramba- Tanga, JKT Makuyuni- Arusha, JKT Bulombora, JKT
Kanembwa, JKT Mtabila- Kigoma, JKT Itaka- Songwe, JKT Luwa na JKT
Milundikwa- Rukwa, JKT Nachingwea- Lindi,JKT Kibiti na Oljoro- Arusha.
No comments :
Post a Comment