Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimpima mwananchi
alietembelea banda la JKCI lililopo ukumbi wa Karume shinikizo la damu
(BP) pamoja na kutoa ushauri wa magonjwa ya moyo wakati wa Maonesho ya
44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) George Msabila akielezea vifaa mbalimbali
vinavyotumika katika chumba cha upasuaji mdogo wa moyo kwa wananchi
waliotembelea banda la JKCI katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Mary Haule akimpima kiwango cha sukari mwilini
mwananchi aliyetembelea banda la JKCI lililopo ukumbi wa Karume wakati
wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Maafisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwapima wananchi waliotembelea banda la JKCI
lililopo ukumbi wa Karume shinikizo la damu (BP) pamoja na kutoa ushauri
wa magonjwa ya moyo wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa
ya Dar es Salaam.
…………………………………………………………………….
ASILIMIA 68 ya
waanchi kati ya 1500 waliojitokeza kujiandikisha ili kuonwa na madaktari
kwenye banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), katika maonesho
ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (sabasaba), wamekutwa na
uzito uliopitiliza (obesity).
Uzito
uliopitiliza ni kiashiria cha hatari kwani wananchi hao wapo kwenye
uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza
(NCD’s), ikiwamo magonjwa ya moyo.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana katika banda la JKCI, lililopo ndani ya jengo
la Karume, Daktari kutoka JKCI Winnie Masakuya, alisema asilimia 58 kati
ya watu waliotembelea banda la JKCI ni wanawake huku wanaume wakiwa
asilimia 42.
“Tangu Julai
mosi, mwaka huu hadi kufikia leo (Julai 8, 2020) tumeona watu wapatao
1,500, kati ya hao asilimia 68 tumewakuta na uzito uliopitiliza huku
asilimia 40 tumewakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu (high blood
pressure).
“Asilimia saba
tumewakuta na kisukari bila ya wao kujijua hali zao kabla ya kufika
kwenye banda letu, na asilimia 18 tuliwakuta wana kiwango kikubwa cha
mafuta kwenye damu (cholesterol’)” alibainisha.
Dk. Masakuya
alisema watu 500 kati ya hao 1,500 walioonwa, wamefanyiwa uchunguzi wa
magonjwa ya moyo kwa kutumia kipimo cha ECG na ECO ambavyo wanavyo ndani
ya banda JKCI.
“Maonesho haya
ni fursa kwa wananchi, kwa sababu kwa kuja kwao hapa kwenye banda letu,
wameonwa na madaktari bingwa na waliogundulika kuwa na matatizo tumewapa
rufaa kwenda kwenye taasisi yetu kwa matibabu zaidi.
“Aidha, wananchi
waliofika kwenye banda letu wamepata fursa ya kupata elimu ya lishe
kutoka kwa wataalamu wetu wa lishe, namna gani wanaweza kulinda afya zao
kwa kuzingatia mfumo bora wa maisha, ulaji unaofaa na hivyo kuepuka
magonjwa mbalimbali yasiyo ambukiza hususan magonjwa ya moyo,” alisema.
Aliongeza
“Nawasihi Watanzania waendelee kuja kwenye banda letu hapa sabasaba hadi
tarehe 13 Julai mwaka huu, hii ni fursa nzuri ya kuweza kujifunza
mtindo wa maisha ulio mzuri ili waweze kutunza afya za mioyo yao,
isichoke mapema.
Naye mwananchi
aliyetembelea banda la JKCI katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam Zainab Hassan ameshukuru kwa kupatiwa huduma
nzuri na ya wakati katika banda la JKCI na kuomba fursa za upimaji wa
magonjwa ya moyo kwa wananchi kama zinazofywa katika banda la Sabasaba
ziweze kuongezwa ili wananchi wengi waweze kufahamu afya zao hasa afya
ya moyo.
“Nimefurahi sana
kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo wangu na kukutwa salama, sikutarajia
kama siku moja nitapima afya ya moyo wangu, hii ni fursa kubwa sana
kwetu wananchi kujitokeza na kuchunguza afya zetu”.
No comments :
Post a Comment