Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitoa maelekezo mbele ya Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ardhi Mary Makondo (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt John Pima (Wa kwanza kushoto) pamoja
na Msajili Msaidizi wa Hati katika ofisi ya Ardhi mkoa wa Arusha Juliana
Ngonyani wakati akikagua masijala ya ardhi alipokwenda kuzindua ofisi
hiyo jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akifafanua jambo mbele ya wananchi
(hawapo pichani) waliohudhuria uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Arusha
jana. Wengine katika picha ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Idd Kimanta (wa
pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo (wa pili kulia),
Katibu Tawala mkoa wa Arusha Richard Kwitega (wa kwanza kulia) na
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Zelothe Stephen.
Baadhi ya Watendaji wa sekta ya
ardhi mkoa wa Arusha na wananchi wakimsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) alipokwenda
kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Arusha jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikata utepe kuzindua ofisi ya ardhi
mkoa wa Arusha jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Arusha Idd Kimanta, wa
tatu kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo na Kulia ni
Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Leo Komba.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi pamoja na viongozi wengine wakiwa
katika picha ya pamoja na wananchi wa mkoa wa Arusha waliopatiwa hati za
ardhi wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi ya mkoa wa Arusha jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza wakati wa uzinduzi wa
ofisi ya ardhi mkoa wa Arusha jana. Wengine katika picha ni Mkuu wa mkoa
wa Arusha Idd Kimanta (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi
Mary Makondo (Kulia) na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Zelothe Stephen
(Kushoto). (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI)
………………………………………………………………………………..
Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Maafisa Ardhi
nchini kuhakikisha wanawafuatilia wamiliki wa ardhi ambao hati zao
zimekamilika lakini hawataki kuzichukua ili wazichukue katika kipindi
cha siku tisini.
Lukuvi alisema
hayo jana jijini Arusha wakati akizindua ofisi ya ardhi ya mkoa huo
ikiwa ni
muendelezo wa ziara yake ya kuzindua ofisi za ardhi katika
mikoa mbalimbali nchini.
Waziri Lukuvi
ambaye tayari amezindua ofisi za ardhi kwenye mikoa ya Tanga na Manyara
alisema, hivi karibuni Bunge lilipitisha sheria inayotaka mmiliki wa
ardhi aliyepimiwa eneo lake kuchukua hati katika kipindi cha siku tisini
na asipofanya hivyo utaratibu wa kumkata kodi ya pango la ardhi
utafanyika.
Kwa mujibu wa
Waziri wa Ardhi, kumekuwa na tabia ya baadhi ya wamiliki wa ardhi
kutojitokeza kuchukua hati za viwanja vyao kwa lengo la kukwepa kulipa
kodi ya pango la ardhi jambo alilolielezea kuwa linamnyima fursa
mbalimbali mmiliki sambamba na kuikosesha serikali mapato yatokanayo na
kodi ya ardhi.
Alitolea mfano wa
mkoa wa Arusha kuwa, pamoja na mkoa huo kuwa na jumla ya viwanja 78,405
vilivyopimwa na hati zake kusajiliwa lakini ni hati 29,000 pekee ndizo
zilizochukuliwa na wamiliki wake na hivyo kufanya hati 49,405
kutochukuliwa na kuikosesha serikali mapato ya ardhi.
‘’Ardhi ndiyo
ulinzi wa rasilimali na inachangia kodi ya serikali kwa hiyo wale wote
wasiochukua hati wajitokeze katika kipindi cha siku tisini, tunataka
idadi ya viwanja vilivyopimwa na kuwekewa mawe ifanane na hati zilizopo
na wote waliopimiwa wakachukue baada ya hapo kama hujachukua hati
utaletewa invoice ya malipo’’ alisema Lukuvi.
Akizungumzia
uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa, Lukuvi ambaye alitoa hati 201 kwa
wamiliki wa ardhi mkoa wa Arusha alisema, ofisi hizo zimeanzishwa ili
kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kubainisha kuwa, sasa
wananchi watapata huduma zote za ardhi kwenye mikoa yao kama walivyokuwa
wakipata Makao makuu ya Wizara na Ofsi za ardhi za Kanda.
Kwa upande wake
Mkuu wa mkoa wa Arusha Iddy Kimanti ameipongeza wizara ya ardhi pamoja
na mhe Rais John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kusogeza huduma za ardhi
karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa na kubainisha
kuwa ofisi yake itatoa ushirikiano na kusaidia masuala mbalimbali ya
ofisi ya ardhi kwenye mkoa wake ili kufanikisha azma ya serikali.
Naye Katibu Mkuu
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alimshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa
kuwezesha utekelezaji jukumu la kusogeza huduma za sekta ya ardhi karibu
na wananchi kwa uanzishaji ofisi za ardhi za mikoa.
Kamishna Msaidizi
wa Ardhi mkoa wa Arusha Leo Komba alisema, tangu kuanzishwa ofisi yake
mwezi Machi mwaka huu tayari jumla ya hati 210 zimeandaliwa na 101
kutolewa kwa wamiki wake huku miamala 282 ikiwa imefanyika na michoro 19
yenye viwanja 4,196 kuandaliwa sambamba na Ramani 29 zenye viwanja 133
kuidhinishwa.
No comments :
Post a Comment