
**************************
Tarehe 16 Juni 2020, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa Hotuba ya Kufunga
Bunge la 11 la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Bunge, Dodoma. Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inatoa pongezi za dhati kwa
Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa Hotuba yake iliyojaa mafanikio makubwa yaliyopatikana
katika kipindi cha miaka mitano cha uongozi wake, yaani kuanzia mwaka
2015 hadi 2020. Hotuba hiyo ilieleza kwa kina mafanikio mbalimbali ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii yaliyopatikana katika kipindi hicho. Aidha,
hotuba hiyo ilisheheni hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali
katika kuimarisha haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
Mhe. Rais alieleza kuwa katika
awamu ya tano uchumi wa nchi ya Tanzania umekuwa kwa asilimia 6.9
kutoka 6.2 mwaka 2015 na pato ghafi la Serikali kuongezeka kutoka
milioni 345 hadi milioni 1,399 na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa
nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi Barani Afrika na kwamba kiwango cha
umaskini kimepungua hadi asilimia 26.4 mwaka 2020. THBUB imeona kwamba
kwa ukuaji huu wa uchumi imewezekana kuimarisha upatikanaji wa haki
mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Katika kuzingatia haki za
binadamu, Mhe. Rais alielezea pamoja na mambo mengine, mafanikio katika
upatikanaji wa haki ya afya, elimu na upatikanaji wa maji safi na
salama. Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza na kusogeza karibu na
wananchi vituo vingi vya kutolea huduma za afya zikiwemo zahanati,
vituo vya afya, na hospitali za Wilaya, Mikoa, Rufaa na Kanda. Kwa
upande wa sekta ya elimu, Serikali iliendelea kutoa elimu bila ya malipo
kwa shule za msingi na sekondari pamoja na kuongeza shule za msingi,
sekondari, vyuo vya ufundi, kujenga mabweni, maabara na kuongeza bajeti
ya mikopo ya elimu ya juu.
Katika kuimarisha utawala bora
na utoaji haki, Serikali ya Awamu ya Tano iliteuwa majaji 17 wa
Mahakama ya Rufani na 52 wa Mahakama Kuu na kuajiri watumishi wengine
890 wa mahakama, wakiwemo Mahakimu 396. Aidha, Serikali ilijenga
Mahakama Kuu mbili, Mahakama za Hakimu Mkazi tano, Mahakama za Wilaya 15
na Mahakama za Mwanzo 18. Hatua hizi zimesaidia kuharakisha
usikilizwaji wa mashauri na hivyo kusaidia kupatikana kwa haki kwa
wakati. Katika kipindi cha miaka mitano Serikali ilipunguza mlundikano
wa mahabusu ambapo mahabusu wapatao 2,812 wamefutiwa kesi zilizokuwa
zinawakabili. Aidha, Mhe. Rais alitoa msamaha kwa wafungwa 42,774.
Pia, Serikali ya Awamu ya Tano
iliimarisha maadili na nidhamu ya kazi nchini ambapo jumla ya watumishi
32,555 walichukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kuwashusha vyeo,
kuwapunguzia mishahara na kuwapa onyo kali. Vile vile, watumishi 15,508
walifukuzwa kazi kwa kukutwa na vyeti feki na idadi ya ajira hewa 19,708
zilibainika ambazo zilikuwa zikiigharimu Serikali T.Shs. Bilioni 198
kila mwezi. Katika kupambana na rushwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU), imeweza kufungua mashauri 2,256, ambapo mashauri
1,926 tayari yametolewa uamuzi.
Katika kulinda haki na
demokrasia nchini, Mhe. Rais kwa mara nyingine ameirejea ahadi yake
aliyoitoa katika sherehe za Maadhimisho ya Muungano zilizofanyika jijini
Mwanza tarehe 26 Aprili, 2020, amewahakikishia Watanzania kuwa Uchaguzi
Mkuu wa Mwaka 2020 utakuwa huru na wa haki. Sambamba na ahadi hiyo,
Mhe. Rais amevitaka vyama vya siasa na wanasiasa kujiandaa ili kushiriki
kikamilifu katika uchaguzi na kujiepusha na matusi, kejeli na
kumtanguliza Mungu katika kampeni za uchaguzi.
Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora inawaomba Watanzania kuendelea kulinda na kuthamini hatua
mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kulinda haki za binadamu
na kudumisha amani na utulivu uliopo pamoja na kuheshimu haki za
binadamu na misingi ya utawala bora ambavyo ni chachu ya amani na
utulivu wa Taifa letu.
Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora kwa mara nyingine inampongeza sana Mhe. Rais kwa kutoa
matumaini makubwa kwa wananchi katika kuendelea kuzingatia haki za
binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
No comments :
Post a Comment