


***************************
WAMJW- Dar es Salaam
Serikali imezindua mwongozo wa
Taifa wa matibabu kwa watu wenye ugonjwa wa sikoseli, huku ikiagiza
kuanzishwa kwa kliniki maalumu za kuchunguza ugonjwa huo katika ngazi ya
wilaya na mikoa ili kuhakikisha watu wengi hasa watoto wanafikiwa.
Akizindua mwongozo huo leo, Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
amesema kuanzishwa kwa kliniki katika ngazi za wilaya na mikoa itasaidia
watu mbalimbali kupata huduma ya utambuzi ya ugonjwa wa sikoseli karibu
na maeneo wanayoishi.
“Naagiza vipimo vya utambuzi
kupelekwa kwenye ngazi ya wilaya na mikoa ili kila mtu aweze kuchunguzwa
kama ana tatizo la sikoseli”. Amesema Waziri Ummy.
Pia, Waziri ameshauri upatikanaji salama wa damu kwa ajili ya
watu wenye tatizo la ugonjwa sikoseli ili kuondoa changamoto ya tiba
kwa wagonjwa mbalimbali.
Waziri wa Ummy ameshauri wananchi
kufanya uchunguzi wa afya zao mapema ili kubaini kama wana ugonjwa huo
kwani endapo watabaini itawasaidia kuanza matibabu mapema.
Katika hatua nyingine, Waziri wa
Afya amewataka wadau wa ugonjwa huo kupunguza gharama za dawa kwani
wagonjwa wengi hawezi kuzinunua.
“Naagiza pia dawa ya sikoseli
ziingizwe katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili iwe rahisi
kupatika kwa wagonjwa wengi”. Amesema Waziri Ummy.
Nae Mganga Mkuu wa Serikali, Prof.
Abel Makubi amesema Serikali imefikia hatua kubwa ya kuanzishwa kwa
mwongozo wa Taifa wa matibabu kwa wagonjwa wa sikoseli kwa kuwa utazuia
vifo vingi.
Amesema vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa sikoseli, vinaweza kuzuilika endapo utagundulika mapema kwa watoto wachanga.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru amesema katika
kliniki ya wagonjwa wa sikoseli, watoto 50 hadi 70 wamekuwa wakipatiwa
matibabu ya ugonjwa huo wakati kwa mwezi ni wagonjwa 211 hadi 300.
“Katika kliniki ya watu wazima,
kwa siku wanaonwa wagonjwa 30 hadi 40 na kwa mwezi wagonjwa 160 hadi 200
wanatibiwa hapa Muhimbili”. Amesema Prof. Museru.
Prof. Museru amesema watoto wenye ugonjwa huo wamekuwa wakipata tatizo la kupumua, damu kuganda mwilini na kiharusi.
Kauli mbiu ya mwaka huu, “Huduma Bora kwa Kila Mhitaji; Chukua hatua, panua wigo.”
No comments :
Post a Comment