Wednesday, June 10, 2020

Benki ya CRDB yawaalika wanahisa katika Mkutano Mkuu wa kihistoria wa Mwaka 2020


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuwakaribisha wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 25 utakaofanyika kupitia mtandao (virtual meeting) tarehe 27 Juni 2020. Pamoja pichani kutoka kulia ni Katibu wa Benki, John Rugambo, Afisa Mkuu wa Fedha, Fredrick Nshekanabo, na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Tully Mwambapa.
Benki ya CRDB imetengeza kufanya Mkutano Mkuu wa Wanahisa tarehe 27 Juni 2020 ambapo kwa mara ya kwanza mkutano huo utafanyika kwa njia ya mtandao. Maamuzi hayo ya kufanya Mkutano huo kupitia mtandao yamekuja baada ya kuahirishwa kwa tarehe ya mwanzo ya Mkutano Mkuu Mei 16, 2020, kutokana na janga la ugonjwa wa corona (COVID19) lililoikumba nchi yetu na dunia nzima.

"Tunafahamu kuwa huu ni utaratibu mpya kwa hivyo kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha kuwa Wanahisa wanapata haki yao ya kushiriki kikamilifu kwenye Mkutano Mkuu kwa kushiriki mada mbalimbali, kupiga kura, kuuliza maswali na kuwasilisha michango mingine, " alisema Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.

Nsekela alisema kuwa agenda mbalimbali zitajadiliwa katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ikiwamo uwasilishaji wa Ripoti za Mwaka na Taarifa za Fedha, kupitisha pendekezo la gawio, malipo ya Bodi, uteuzi wa Wajumbe huru wa Bodi, uteuzi wa wakaguzi wa nje pamoja na kujadili mada mbalimbali zitakazowasilishwa na Wanahisa. Nsekela alisema kufanyika kwa Mkutano Mkuu kupitia mtandao kutatoa fursa kwa Wanahisa wengi zaidi kushiriki mkutano huo.

Nsekela aliwahimiza Wanahisa wa Benki ya CRDB kutumia mfumo wa fomu za uwakilishi “Proxy Forms” kupiga kura kabla ya Mkutano Mkuu wa mwaka. “Haki za kupiga kura kwa wanahisa zinaweza kutumiwa kupitia fomu hiyo ya uwakilishi (proxy form),” alisema Nsekela.

Nsekela alisema Wanahisa wote ambao watakuwa wamekamilisha usajili watatumiwa taarifa za kujiunga na Mkutano Mkuu kupitia anwani zao za barua pepe au nambari za simu zilizosajiliwa. Kwa wale ambao watakuwa na wawakilishi (Proxies); watahitaji kujaza Fomu za uwakilishi (proxy form) na kusajili taarifa zao. Fomu ya uwakilishi (proxy) inapatikana kwenye mtandao kupitia tovuti yetu www.crdbbank.co.tz ”.

Wanahisa wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanawasilisha Fomu zao za uwakilishi (proxy form) kupitia matawi ya Benki ya CRDB, barua pepe shareholders@crdbbank.com au kupitia nambari ya WhatsApp 0767 757 215 kabla ya saa 10:00 jioni Ijumaa 19 Juni, 2020. 

Baada ya kudhibitisha kushiriki, Wanahisa watatumiwa pewa uthibitisho wa kujiunga na mkutano, ikiwa ni pamoja na namba ya mkutano, namba ya utambulisho ya mwanahisa, na namba ya siri itakayo wezesha kushiriki mkutano kwa njia ya mtandao.

Kwa hivyo wanahisa na wawakilishi wao wanahimizwa sana kutumia fursa hii ya kushiriki katika Mkutano Mkuu kwa njia ya mtandao. Mkutano unaweza kufikiwa mtandaoni kupitia web.lumiagm.com au mwanahisa anaweza kupakua Programu ya “Lumi AGM” kutoka Google PlayStore au Apple AppStore na atumie taarifa zilizotumwa kwake kushiriki katika mkutano.

Nsekela alisema Benki ya CRDB imejipanga vilivyo kuhakikisha Mkutano Mkuu wa Wanahisa unakuwa wa mafanikio ambapo Wanahisa watakuwa wakipewa taarifa mbalimbali kupitia simu zao za mkononi, barua pepe na mitandao ya kijamii.

No comments :

Post a Comment