Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akisikiliza maelezo kutoka
kwa kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwanyamala Dkt:
Isdory Kiwale baada ya kufanya ziara hospitalini hapo, kuangalia utoaji
wa huduma za afya, husasani katika kipindi hiki cha kukabiliana na
ugonjwa wa Covid -19.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ummy mwalimu, akizungumza na wagonjwa
waliofika kupatiwa huduma za matibabu katika hospitali ya Rufaa ya
Mwananyamala, baada ya kufanya ziara ya kukagua huduma zinazotolewa
hospitalini hapo.
**********************************
WAMJW Dar es Salaam
Serikali imesema itaendelea kutoa
kipaumbele katika ajira za wauguzi kadri nafasi zitakavyokuwa
zikipatikana ili kuboresha huduma za afya nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa ya
Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Waguzi Duniani ambayo
huadhimishwa tarehe 12 Mei kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni
“Wauguzi; Sauti inayoongoza Uuguzi kwa Dunia yenye Afya.”
Waziri Ummy Mwalimu amesema
Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kwa sababu
kuna uhaba wa wauguzi kwenye vituo vya afya licha ya kuwapo zaidi ya
wauguzi 30,451 katika vituo vya umma na binafsi nchini.
Amesema asilimia 80 ya huduma za
afya katika vituo vya kutoa huduma za afya zinatolewa na wauguzi hivyo
Serikali itaendelea kutambua na kuthamini kazi nzuri zinazofanywa na
wauguzi nchini.
“Wauguzi wamekuwa wapambanaji
wakubwa katika kutoa huduma kwa washukiwa wa ugonjwa wa Corona
(Covid-19), hivyo hongereni wauguzi wote nchini Tanzania,” amesema
Waziri.
Amesema katika jitihada za
Serikali za kuboresha huduma za wauguzi na wakunga, Serikali
imekamilisha muongozo wa kutoa huduma kwa kuzingatia utu, heshima na
maadili.
Waziri wa Afya amesema jumla ya
waguzi 778 katika hospitali 15 za rufaa za mkoa wamepatiwa mafunzo
muhimu ili kuwezesha mpango wa kutoa huduma rafiki kwa wananchi na kwa
kujali utu wao.
“Mafunzo haya yataendelea kutolewa
katika ngazi zote za kutoa huduma na tayari tumetengeneza mfumo wa
kupokea taarifa za malalamiko na kero kutoka kwenye vituo vya kutolea
huduma,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Naye Rais wa Chama cha Wauguzi na
Wakunga Tanzania (TANNA), Bw. Alexander Baluhya amesema ili kuwapo kwa
huduma bora na salama za afya, nchi inapaswa kuwa na wataalamu wenye
weledi wa hali ya juu na mazingira bora ya kazi.
“Hivi sasa nchi yetu ina wauguzi
30,451 waliojiriwa katika sekta ya afya ambao ni takribani asilimia 60
ya wataalamu wote wa afya. Wauguzi hawa wanatoa zaidi ya asilimia 80 ya
huduma za afya ambazo zimekuwa zikitolewa kwa Watanzania. Hivyo upungufu
wa wauguzi na wakunga ni asilimia 48,” amesema Bw. Baluhya.
Bw. Baluhya amewapongeza wauguzi
nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao
hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19).
No comments :
Post a Comment