…………………………………………………………………………….
KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA UDANGANYIFU [MTANDAO WA KIJAMII].
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawashikilia watuhumiwa wawili 1. SOPHIA ELIA MWALUANDA [22]
Mfanyabiashara na Mkazi wa Sistila Jijini Mbeya na 2. MPAJI SELEMAN
MWINYIMVUA [38] Mkazi wa Manzese Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia akaunti feki ya
“facebook” yenye jina la Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli Mke wa
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe
Magufuli.
Watuhumiwa wamekamatwa mnamo
tarehe 28.04.2020 majira ya saa 15:00 Alasiri katika operesheni na msako
uliofanywa huko eneo la Ikuti Sokoni, Kata ya Ikuti, Tarafa ya Iyunga,
Jijini Mbeya.
Mbinu wanayoitumia watuhumiwa ni
kufungua akaunti “facebook” yenye jina la JANETH MAGUFULI SACCOS na
kuuaminisha umma kwa kuweka picha ya mama Janeth Magufuli na kisha
kutangaza kutoa mikopo nafuu kwa sharti la muombaji kutuma kwanza fedha
kiasi cha Shilingi 76,500/= kwenye namba ya simu waliyoiweka kama ada ya
mkopo ili aweze kupata mkopo wa Shilingi Milioni 3,000,000/=.
Watuhumiwa wamekutwa na simu mbili
aina ya Infinix Smartphone ambayo
imetumika kufungulia akaunti hiyo ya
“facebook” na simu aina ya Siccoo Mobile [Analogue] inayotumika kupokea
fedha zinazotumwa na watu mbalimbali. Aidha watuhumiwa wamekutwa na
fedha taslimu shilingi 470,000/= ambazo wamekiri kuzipata kwa njia ya
udanganyifu kupitia akaunti hiyo feki.
Mtakumbuka Februari 21, 2020 huko
katika Mji Mdogo wa Mbalizi Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliwakamata
vijana kumi na moja [11] kwa tuhuma za kujihusisha na wizi kwa njia ya
mtandao kwa kutumia akaunti feki za mitandao ya kijamii ikiwemo
“facebook” wenye majina ya viongozi wa Serikali na Wasanii maarufu wa
hapa nchini. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya
kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
WITO WA KAMANDA.
Natoa rai kwa watanzania kuheshimu
ikulu kwani ni mahali patakatifu na hapachezewi kabisa, Chombo cha dola
hakitavumilia kuona mtu wa aina yeyote kwa vyovyote vile akitumia jina
la ikulu kuibia au kutapeli watu wengine.
Ninatoa wito kwa wananchi kuwa
makini na taarifa mbalimbali zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii
ambazo zinaelekezea fursa mbalimbali kama vile ya mikopo, masomo na
biashara ambazo zinawataka kutuma kiasi kadhaa cha fedha ikiwa ni moja
ya masharti ya kupata fursa hiyo, ni vyema kujiridhisha kwenda mamlaka
za serikali zilizo karibu kwa ajili ya kupata uhakika kabla ya kufikia
uamuzi wa kutuma fedha.
Aidha ninawataka vijana kujenga
utamaduni wa kufanya kazi ili kujipatia kipato halali badala ya
kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu ambavyo vitawasababisha kupata
adhabu kali kwa mujibu wa sheria.
Mwisho, ninatoa rai kwa mtu/watu
waliotuma fedha kupitia namba ya watuhumiwa kwa lengo la kupata mkopo
kufika kituo cha Polisi kilichopo jirani kwa ajili ya kutoa taarifa ili
taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawashikilia watuhumiwa wanne 1. RIZIKI ANTHONY MUHEMA [20] Mkazi wa
Mtakuja Mbalizi, 2. REHEMA KASELA [36] Mama Mzazi wa marehemu na Mkazi
wa Iwindi 3. ESTA MSONGOLE [52] Mganga wa Kienyeji na Mkazi wa
Sumbawanga na 4. MTUMWA HAONGA [65] Mganga wa Kienyeji na Mkazi wa
Mtakuja Mbalizi kwa tuhuma za mauaji ya mtoto TAMALI SIMON, miaka miwili
na miezi mitatu.
Watuhumiwa walikamatwa katika
operesheni maalum iliyofanywa na kikosi kazi cha Jeshi la Polisi Mkoa wa
Mbeya tarehe 06.05.2020 majira ya saa 04:00 usiku huko Iwindi, Kata ya
Utengule Usongwe katika Mji Mdogo wa Mbalizi na kufanikiwa kuwakamata
watuhumiwa hao ambao wamekiri kufanya tukio hilo kwa kushirikiana na
mama mzazi wa marehemu.
Chanzo cha tukio ni tamaa ya
kupata utajiri kwa njia za kishirikina baada ya mtuhumiwa ambaye ni
mganga wa kienyeji kuwapa masharti yaliyopelekea kifo cha mtoto huyo.
Awali mnamo tarehe 04.05.2020
majira ya saa 20:00 usiku huko Kijiji na Kata ya Iwindi, Tarafa ya
Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya, Mtoto TAMALI SIMON,
miaka miwili na miezi mitatu, Mkazi wa Iwindi alikutwa ameuawa kwa
kunyongwa shingo na mtu asiyejulikana na mwili wake kutelekezwa.
Kutokana na tukio hilo, Kikosi
kazi cha Polisi Mkoa wa Mbeya kilifanya msako mkali na kufanikiwa
kuwakamata watuhumiwa katika maeneo tofauti na katika mahojiano
watuhumiwa wamekiri kuhusika kwenye tukio hilo baada ya kupewa masharti
na mganga wa kienyeji. Aidha upekuzi umefanyika nyumbani kwa Mganga wa
kienyeji na kukamata vifaa mbalimbali vya uganga na dawa za kienyeji za
aina mbalimbali. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya
kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawashikilia watuhumiwa wanne 1. VIOLETH SIMELUTA [26] Mwalimu na
Mkazi wa Isanga, 2. CHARLES SIMELUTA [39] Mkazi wa Isanga, 3. EMMANUEL
KIWALE [30] Mkazi wa Mafiati na 4. SOPHIA SAMSON [42] Mkazi wa Airport
ya Zamani kwa tuhuma za mauaji ya JUNIOR CHARLES MACHIBYA [30] Mkazi wa
Airport ya Zamani.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo
tarehe 07.05.2020 baada ya kikosi kazi cha Polisi Mbeya kufanya msako na
upelelezi wa kina na kubaini kuwa marehemu aliuawa kwa kupigwa vitu
butu usoni na kunyeshwa sumu huku chanzo cha tukio hilo kikiwa ni ugomvi
wa kifamilia.
Awali mnamo tarehe 30.04.2020
majira ya saa 20:00 usiku huko Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya JUNIOR
CHARLES MACHIBYA [30] Mkazi wa Airport ya Zamani alifikishwa Hospitalini
hapo na wasamalia wema wakidai kuwa amekutwa maeneo ya nyumbani kwake
akiomba msaada na akilalamika maumivu makali ya tumbo akidai kuwa
amenyweshwa sumu bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Tarehe 01.05.2020 majira ya saa
18:00 jioni alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu na ndipo
upelelezi ulianza pamoja na msako na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa
wanne kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo. Upelelezi unaendelea.
No comments :
Post a Comment