WAMJW- Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua kituo cha huduma
za simu kwa wateja ambacho kazi kubwa ni kutoa elimu sahihi kwa jamii
kuhusu masuala mbalimbali ya afya ikiwamo magonjwa milipuko.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Waziri Ummy Mwalimu amesema kituo hicho kina
uwezo wa kupokea
simu 1000 kwa wakati mmoja na kuunganisha vituo vitano kwa wakati mmoja.
Amesema kazi ya kituo hicho ni
kupokea maoni, taarifa, maswali na ushauri kuhusu masuala mabalimbali
yanayohusu sekta ya afya na amewataka wananchi kupiga simu 199 ili
wapate huduma na walioko nje ya nchi wanapaswa kupiga namba 0800110124.
Amewataka wananchi watakaopiga simu kuwa wastaarabu, kutumia lugha ya staha na kutoa taarifa sahihi ambazo zitasaidia Serikali na Wizara ya Afya kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
Amewataka wananchi watakaopiga simu kuwa wastaarabu, kutumia lugha ya staha na kutoa taarifa sahihi ambazo zitasaidia Serikali na Wizara ya Afya kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
Amefafanua kwamba kituo hicho
kitatumika kutoa elimu na miongozo mbalimbali kuhusu masuala ya afya na
kitakuwa na watalaamu 150 wakiwamo wataalamu wa afya, wauguzi na
madaktari.
Amesema endapo Wizara ya Afya
itaweza kutumia vizuri Tehama, itachangia changamoto mbalimbali zilizoko
kwenye sekta ya afya, huku akiitaka jamii itambue kinga ni bora kuliko
tiba na kwamba Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka minne
na nusu imefanya vizuri katika masuala ya tiba na kinga.
“Hapa nimeelezwa kwamba kituo hiki
kitahudumia kwa saa 24 kwa mwaka na kina uwezo wa kuhudumia watu
300,000 kwa siku,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya, amependekeza kituo
hicho kipatiwe jina la ‘Afya Call Centre’ badala ya kituo cha huduma za
simu ambacho kitakuwa kikishughulikia magonjwa yote.
“Kituo hiki kitakuwa kikizungumzia
chanjo kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja, tutazungumzia
masuala ya liche kwa kina mama wenye umri wa kuzaa, lishe kwa watoto
wenye umri chini ya miaka mitano, masuala ya huduma ya uzazi ya mama na
mtoto, tutanzungumzia mapambano ya ugonjwa wa kifua kikuu na masuala ya
tiba,” amesema.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amesema kituo hicho kitatumika kutoa taarifa sahihi kwa jamii na kwa wakati.
Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa
Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt. Ama Kasangala alimweleza Waziri
wa Afya, Ummy Mwalimu kwamba kazi kubwa ya kituo hicho ni kupokea
maswali, maoni na ushauri kutoka kwa wananchi na kufanyiwa kazi na
wataalamu wa afya.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la
Afya Duniani Tanzania (WHO), Dkt. Tigest Ketsela amepongeza kuanzishwa
kwa kituo hicho kwa kuwa kitatumika kujibu maswali ya wananchi kuhusu
magonjwa mbalimbali.
Dkt. Ketsela taarifa
zitakazotolewa katika kituo hicho zitatumika kuandaa jumbe za
kuielimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
Wadau wengine walioshiriki katika
ujenzi wa kituo hicho wameipongeza Serikali na Wizara ya Afya kwa
kizindua kituo hicho kwani kitasaidia kujenga imani kubwa kwa wananchi
katika masuala yanayohusu afya.
No comments :
Post a Comment