Asasi isiyo ya kiserikali ya
Change Tanzania Limited ambayo mmiliki wake ni Bi. Maria Sarungi Tsehai
imeshindwa kwa mara nyingine kesi iliyoifungua dhidi ya Msajili wa
Makampuni. Katika kesi hiyo, ambayo uamuzi wake umetolewa tarehe 20 Mei,
2020, Mahakama Kuu ya Tanzania imeona kuwa hoja zilizowasilishwa
Mahakamani hapo hazina msingi hivyo kuifuta kesi hiyo na kuitaka Asasi
hiyo kulipa gharama zote za Serikali. - KIINI CHA SHAURI
Asasi ya Change Tanzania ilifungua
shauri tajwa Namba. 27 la mwaka 2019 katika Mahakama Kuu (Kitengo cha
Biashara) ambapo pamoja na mambo mengine, ilikuwa ikipinga Marekebisho
katika Sheria ya Makampuni Sura ya 212.
Marekebisho katika Sheria ya
Makampuni Sura ya 212 yalihusu pamoja na mambo mengine kuweka tafsiri
mpya ya maneno “Kampuni” na “Asasi” katika Sheria husika na pia kuzitaka
Asasi zote zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni ambazo hazikuwa
na malengo ya kibiashara kujisajili chini ya Sheria husika na iwapo
zingeshindwa kufanya hivyo ndani ya muda wa miezi miwili zingehesabika
kuwa zimefutiwa usajili wake.
Asasi ya Change Tanzania ilitaka
Mahakama itoe Amri ya kukubalika kwa ombi la kubadili Katiba yake ili
iweze kuendelea kutambulika kama Asasi iliyosajiliwa chini ya Sheria ya
Makampuni baada ya kubadilishwa kwa Sheria husika kwa lengo la kutaka
Asasi zote zisizo na malengo ya kibiashara zisisajiliwe chini ya Sheria
ya Makampuni na badala yake zikajiandikishe chini ya Sheria yenye
kukidhi malengo ya Asasi hizo.
Change Tanzania ilitaka pia
Mahakama itoe Amri ya kumtaka Msajili wa Mahakampuni kupokea na
kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya Taasisi hiyo ambayo walidai kuwa
yamekwishafanyika na kuwasilishwa kwa Msajili wa Makampuni na kulipiwa.
- UTETEZI WA SERIKALI
Katika utetezi wake, Serikali
kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliwasilisha hoja tano (5) za
kisheria kupinga maombi hayo kwa msingi kwamba maombi hayo yamepitwa na
muda kwa kuwa Sheria iliyokuwa ikibishaniwa ilishaanza kutekelezwa na
katika Shauri hilo, Asasi ya Change Tanzania haikuwa na msingi wowote
kisheria wa kumshtaki Msajili wa Makampuni. Pia, Serikali ilipinga madai
hayo kutokana na Asasi hiyo kufungua Shauri dhidi ya Msajili wa Wakala
wa Usajili na Leseni (BRELA) ambaye hayupo kisheria badala ya Msajili wa
Makampuni.
- UAMUZI WA MAHAKAMA
Baada ya kusikiliza pande zote
mbili, mnamo tarehe 20 Mei, 2020, Mahakama Kuu ya Tanzania (Kitengo cha
Biashara iliafikiana na hoja za Serikali na kuitupilia mbali kesi hiyo
kwa kukosa hoja za msingi kisheria.
Mahakama imeamuru pia Asasi ya Change Tanzania kulipa gharama zote za Serikali kutokana na shauri hilo lisilo na msingi.
Hii ni kesi ya pili kwa Asasi ya
Change Tanzania kushindwa. Mnamo tarehe 14 Mei, 2020, Mahakama Kuu ya
Tanzania ilitupilia mbali kesi ya Kikatiba Namba. 21 ya mwaka 2019.
iliyofunguliwa tarehe 29 Agosti, 2019 na Asasi za Centre for Strategic
Litigation ambayo mmoja wa wamiliki wake ni Wakili wa Kujitegemea Bw.
Jebra Kambole na Change Tanzania Limited. Kesi hiyo ilifunguliwa kupinga
Marekebisho katika Sheria ya Makampuni Sura ya 212, Sheria ya Asasi
Zisizo za Kiserikali Sura ya 337 na Sheria ya Miunganisho ya Wadhamini
Sura ya 318.
No comments :
Post a Comment