Wednesday, May 27, 2020

MFUMO WA STAKABADHI GHALANI UNAKWENDA KUMNUFAISHA MKULIMA WA UFUTA -RC NDIKILO


……………………………………………………………………………
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKOA wa Pwani, umekemea wakulima wa ufuta waliofanya udanganyifu  msimu wa ununuzi uliopita kwa kuchanganya ufuta na mchanga, kwani umesababisha doa kwenye soko hivyo kwasasa mfumo utakaotumika ni wa stakabadhi ghalani ,ambao utadhibiti udanganyifu na kuinua pato la mkulima.
Aidha minada ya ununuzi wa ufuta mwaka huu yatafanyika kupitia mfumo huo na kwa njia ya kielektroniki kupitia soko la bidhaa Tanzania (TMX).
Akifungua kikao cha kujadili maandalizi ya msimu wa ununuzi wa ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo aliwataka wakulima kuacha udanganyifu ili kurudisha imani kwa wanunuzi na mkulima mwenyewe kuondokana na maumivu ya bei zilizokandamizi .
“Mkoa unatambua changamoto zilizojitokeza msimu wa ununuzi wa mwaka 2019/2020 ,ikiwemo udanganyifu ,baadhi ya viongozi wa  vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS kutokuwa waaminifu pamoja na ubora duni wa miundombinu ya maghala na ucheleweshaji wa zoezi la usafirishaji ufuta kutoka kwenye maghala “; alifafanua Ndikilo .
Ndikilo alieleza ,changamoto hizo zilisababisha wadau kulalamikia ufanisi mdogo wa mfumo mzima wa ununuzi wa zao hilo .
Mkuu huyo wa mkoa alisema ,ili kukabiliana na changamoto hizi serikali imeamua kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani kuanzia msimu huu .
Ndikilo alibainisha kupitia mfumo ,wanachama na wakulima watapeleka ufuta kwenye maghala ya vyama vya ushirika vya msingi ambavyo vitapeleka ufuta kwenye maghala makuu yaliyosajiliwa na bodi ya leseni za maghala Tanzania ,huku maghala makuu yatapeleka taarifa za ufuta uliopokelewa kwenda TMX ambayo itaratibu minada .
Ndikilo alielekeza pia ,wakulima walipwe katika akaunti zao na wakala wa vipimo wasimamie ubora wa mizani ili wakulima wasipunjwe .
Hata hivyo ,aliwaelekeza viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wahakikishe vifungashio vya ufuta ghafi vinapatikana kwa wakati kwa wakulima.
Nae mrajisi wa mkoa wa Pwani ,Angela Nalimi alisema ,katika msimu wa mwaka 2019/2020 jumla ya kilo milioni 7.326.980 za ufuta zenye thamani ya bilioni 19.352.7 zilikusanywa na kuuzwa kupitia maghala ya Amcos .
Nalimi alisema kwamba ,matarajio ya uzalishaji wa zao la ufuta kwa msimu wa mavuno wa mwaka 2020/2021 unakadiriwa kuzalisha  kilo milioni 9.5 sawa na tani 13,250 zitakazokusanywa kupitia Amcos 53.
Mrajisi huyo alisema bayana ,hadi sasa wana vifungashio 14,000 vitakavyosafirishwa kupelekwa kwenye Amcos na kuzigawa kwa wakulima.
Mkoa wa Pwani, ni miongoni mwa mikoa inayozalisha zao la ufuta kwa wingi hapa nchini 

No comments :

Post a Comment