*****************************
Na Magreth Kinabo-Mahakama
Majaji 125 kutoka katika mabara
manne duniani wamefanya mkutano kwa njia ya mtandao kujadili jinsi
ya kuendelea na shughuli za utoaji haki kwa kutumia Teknolojia ya Habari
na
Mawasiliano (TEHAMA) ili kuepuka kuenea kwa maambukizi ya virusi vya
Corona vinavyosababisha ugonjwa homa ya mapafu (COVID 19).
Mkutano huo uliandaliwa na Shirika
la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) ambalo liko chini ya Umoja wa Mataifa
(UN), uliofanyika Makao Makuu ya shirika hilo Geneva, kwa njia ya
mtandao hivi karibuni. Lengo la mkutano huo wa siku moja lilikuwa ni
kubadilishana uzoefu jinsi gani Mahakama zinaweza kuendelea na huduma za
utoaji haki katika kipindi cha janga la Corona.
Akizungumza kuhusu mkutano huo,
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe. Stephen
Magoiga alisema mkutano huo ulishirikisha Majaji kutoka Bara la Afrika,
Ulaya, Marekani na Asia. Katika mkutano huo, Tanzania iliwakilishwa na
yeye pamoja na Mwakilishi wa WIPO kutoka Mahakama ya Tanzania, ambaye ni
Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Upendo Ngitiri.
Jaji Magoiga alifafanua kwamba
miongoni mwa waliyopendekeza katika mkutano huo, ni Majaji kuwezeshwe
kuwa na huduma ya mtandao (internet) nyumbani na sio ofisini tu ili
waweze kuendelea na huduma ya utoaji haki hususan kipindi cha ugonjwa wa
homa ya mapafu, ikiwemo kuenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
“Suala la mabadiliko ya TEHAMA)
ni muhimu ili tuendane na mabadiliko ya teknolojia. Hivyo Majaji
wasiwe na huduma ya mtandao maofisini tu bali hata kwenye nyumba zao ili
waweze kuendelea na huduma za utoaji haki hasa katika kipindi hiki cha
janga la Corona hata wakiwa nyumbani kwa kuwa wakati mwingine hawawezi
kumaliza kazi ofisini, pia itawawezesha kufanya tafiti mbalimbali,”
alisema Jaji Magoiga.
Jaji Magoiga alisema kupitia
mkutano huo, wamejifunza kuwa Majaji wa Uingereza mazingira yao
yanawaruhusu kufanya kazi hata wakiwa nyumbani kwa mujibu wa Jaji
wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Mhe. Collins Birss.
Aliongeza kwamba matumizi ya
TEHAMA pia yanasaidia kulinda usalama wa watumishi katika kipindi hicho
na kutoa huduma kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Mhe. Ngitiri
alisema katika mkutano huo, wamejifunza kwamba huduma za utoaji haki
zinaweza kuendelea kutolewa kwa njia ya mawasiliano ya simu kwa nchi
ambazo zimewekewa zuio la kutotoka nje ikiwa ni hatua za kukabiliana na
virusi vya Corona, kupitia Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Marekani,
Mhe. Cathleen O’ Malley.
Aidha Ngitiri alitoa uzoefu wa
Mahakama ya Tanzania katika kipindi hiki, akisema imechukua hatua
stahiki, shughuli za Mahakama zinaendelea kufuatia agizo la Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kusisitiza matumizi ya TEHAMA
kwenye suala la ufunguaji mashauri kwa njia ya kielektroniki na
Mahakama Mtandao ‘Video Conference’ itumike kusikiliza.
Katika mkutano huo walijadili matumizi ya kamera mahakamani kuwa yanaweza kufanyika kwa kurekebisha ya baadhi ya kanuni.
WIPO ilifanya mkutano wa siku 7
hapa nchini Tanzania mwaka jana katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini
Dar es Salaam ulioshirikisha washiriki 35 kutoka nchi za Sweden,
Switzerland, Nepal, Cambodia, Rwanda, Uganda, Mozambique, Zambia,
Malawi, Burtan, Ethiopia n.k.
Aidha Mahakama ya Tanzania kwa
kushirikiana na WIPO kwa mara ya kwanza iliwapatia Mafunzo ya Haki
Miliki jumla ya Mahakimu 30 yaliyolenga kuwawezesha kuandika hukumu bora
zaidi kwa mashauri yanayohusiana na haki miliki.
No comments :
Post a Comment