Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani
Manyara, Elizabeth Kitundu akizungumza baada ya kukabidhiwa barakoa
2,750 na miavuli 27 ya thamani ya shilingi milioni 7 iliyotolewa na
shirika la PhamAccess kwa ajili ya kutumiwa na wahudumu wa afya na
wanawake wajawazito, kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Khalifan
Matipula na Meneja mradi wa safari salama ya mama mjamzito ‘Momcare’
Johnson Mali.
********************************
SHIRIKA la PhamAccess Foundation,
limekabidhi barakoa 2,750 na miavuli 27 ya thamani ya
sh7 milioni Wilaya
ya Babati Mkoani Manyara kwa lengo la kuunga mkono mapambano ya
kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Meneja mradi wa safari salama ya
mama mjamzito ‘Momcare’ wa shirika la PhamAccess, Johnson Mali
alikabidhi vifaa hivyo jana kwa mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth
Kitundu.
Mali alisema kati ya barakoa hizo
2,750 barakoa 1,750 ni kwa ajili ya watoa huduma za afya, barakoa 1,000
zitatumiwa wajawazito na miavuli 27 kwa ajili ya wahudumu waandikishaji
wa mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa (iCHIF).
Alisema vifaa hivyo vimetolewa kwa
gharama za shirika la PhamAccess kwa ushirikiano wa wafanyakazi wake
ambao nao kwa hiyari yao walichanga sehemu ya fedha zao ili kuvinunua
katika kupiga vita maambukizi ya virusi vya corona.
“Hizo barakoa 1,000 ambazo
zitatumiwa na wanawake wajawazito zimetokana na michango ya wafanyakazi
wa shirika letu la PhamAccess kama mchango wao kwa jamii katika
mapambano ya virusi vya corona,” alisema.
Alisema hii ni mara ya pili kwa
shirika hilo la PhamAccess, kutoa msaada wa vifaa mbalimbali ya
kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwani mara ya kwanza
walitoa kwenye ngazi ya mkoa wa Manyara.
“Tumetoa msaada wa vifaa hivi huku
tukiendelea kuboresha vituo vyetu kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa
huduma za afya kwa wananchi na usalama wa mgonjwa na watoa huduma,”
alisema Mali.
Alisema wamekuwa wakitoa mafunzo
kwa watumishi vituoni na kutoa miongozo na vifaa tiba kwa lengo la
kuhakikisha mwanamke ananufaika.
Mkuu wa wilaya ya Babati,
Elizabeth Kitundu aliwapongeza wafanyakazi wa shirika la PhamAccess kwa
kufanikisha ununuzi wa vifaa hivyo ambavyo kwa namna moja au nyingine
zitasaidia mapambano hayo.
Kitundu aliwataka wadau wengine
kuiga mfano wa jitihada za PhamAccess katika kusaidiana na serikali
katika vita hiyo ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona.
“Hii ni mara yenu ya pili ya kutoa
msaada wa vifaa kama hivi mara ya kwanza mlitoka kwenye ngazi ya mkoa
na leo mmetoa katika ngazi ya wilaya ya Babati, hongereni sana,
tunawashukuru mno kwa kujali,” alisema.
Mtumishi wa idara ya afya wa
hospitali ya mji wa Babati, Gabriel Sulle alisema kwa niaba ya uongozi
wa halmashauri ya mji anawashukuru PhamAccess kwa kutoa vifaa hivyo.
“Vifaa hivyo tutatolewa kwa
watumishi wa hospitali ya mji, vituo vya afya na zahanati mbalimbali
katika halmashauri mbili za wilaya na mji wa Babati kama mlivyoelekeza,”
alisema Sulle.
No comments :
Post a Comment