Afisa Usalama, Afya Mazingira na
Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles akimkabidhi Mwenyekiti wa
wafanyabiashara wa soko la Mashine Tatu, Japhary Sewando baadhi ya
barakoa zilizotolewa kwa niaba ya mama lishe wa sokoni hapo kati barakoa
500 zilizotolewa kwa mama lishe wanaofanya biashara katika masoko
matano ya manispaa ya Iringa,
Mmoja ya mama lishe wa soko kuu
la Iringa akiwa amevaa barakoa zilizotolewa na kampuni ya Asas kwa mama
lishe wote ndani ya manispaa ya Iringa
Afisa Usalama, Afya Mazingira na
Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles (kushoto) akiwa na baadhi
wafanyabiashara wa soko la mashine tatu baada ya kuwakabidhi barakoa
zilizotolewa na kampuni hiyo ambazo zimetolewa barakoa 500 kwa masoko
matano
Picha na Denis Mlowe)
………………………………………………………………………………
NA DENIS MLOWE. IRINGA
Katika kuendelea na mapambano
dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona nchini kampuni Asas yenye makao
makuu mkoani Iringa imegawa msaada wa barakoa 500 kwa mama lishe
wanaofanya biashara zao katika masoko matano yaliyoko manispaa ya Iringa
kwa ajili ya kujinga na Virusi Vya Corona.
Msaada huo umetolewa kwa mama
lishe hao ikiwa ni juhudi za kampuni hiyo kuungana na serikali katika
kutokomeza kuenea kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa
Covid 19 ambao umekuwa janga la dunia kwa sasa.
Akikabidhi msaada huo, Afisa
Usalama, Afya Mazingira na Ubora wa Kampuni ya Asas Cosmas Charles kwa
niaba ya mkurugenzi wa uzalishaji wa kampuni hiyo, Ahmed Salim
Abri alisema kuwa huo ni mwendelezo wa kampuni hiyo katika kusaidia
jamii ambayo inahusisha mikusanyiko ya watu wengi zaidi ndani na nje ya
mkoa wa Iringa
Alisema kuwa kampuni ya Asas
imekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii bila kuchoka kutokana hali za
wananchi wengi sana kwa sasa kuhitaji msaada hivyo imekuwa mstari wa
mbele katika kusaidia jamii hasa katika suala zima la kupambana kuenea
kwa virusi vya corona mkoani hapa na kuweza kutoa misaada mbalimbali kwa
jamii yenye mikusanyiko kwa watu wengi.
Alisema kuwa msaada huo
umewafikia mama lishe kutokana na kuwahudumia watu mbalimbali ambao
wanatoka sehemu tofauti na kwa kuona changamoto yao baada ya kufanya
utafiti na kubaini wengi wao wanauhitaji wa kupewa msaada wa barakoa
ambazo ni bora.
Cosmas alisema alitoa wito kwa
mama lishe hao kuhakikisha kwamba wanatumia barakoa na kunawa mikono
kwa lengo la kujilinda wao na wateja wao wanaowahudumia kwa kuwa bila
hivyo itakuwa rahisi endapo mmoja ana virusi hivyo kuvieneza kwa urahisi
na kuwataka kuhakikisha wana nawa mikono kwa maji safi na sabuni za
kutakasa mikono.
Alisema kuwa msaada huo umewafikia
mama lishe wanaofanya biashara katika masoko ya Mashine Tatu, Kihesa,
Soko la kisasa la Mlandege, Soko Kuu la Iringa na soko la Ipogoro ambapo
kuna mwingiliano wa watu wengi wanaopata mahitaji sokoni hapo.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo
imekwisha toa msaada kwa umoja wa madereva daladala kwa kuwakabidhi
vifaa kama ndoo maalum kunawia mikono na vitakasa mikono, barakoa zaidi
ya 2000 kwa umoja wa madereva bajaji, msaada wa mashine ya kujifukuzia
kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.
Kwa upande wao wenyeviti
wa masoko hayo wakizungumza kwa niaba ya mama lishe baada ya
kukabidhiwa msaada huo walishukuru kampuni ya Asas kwa kuwa mstari wa
mbele kurudisha faida kwa jamii na kutoa wito kwa makampuni mengine
kuiga mfano wa kampuni hiyo kujitoa kwa jamii.
Walisema kuwa kampuni ya Asas
inapata Baraka za MUNGU kwa kuwa imekuwa ikisaidia jamii hasa wenye
uhitaji hali ambayo imewafanya kujijengea imani kubwa kwa wananchi ambao
wamekuwa wateja wazuri wa kununua bidhaa zao kutokana na wao
kuwathamini katika mazingira magumu.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara
wa soko la Mashine Tatu, Japhary Sewando alisema kuwa wafanyabiashara wa
soko hilo wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya kuenea kwa
virusi vya corona katika soko hilo hivyo msaada huo umekuja wakati
mwafaka kwa mama lishe hao hali ambayo wamefurahia na kushukuru kampuni
ya Asas.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
wafanyabiashara wa soko kuu la mjini Iringa, Odilo Ngamilaga alisema
kuwa kampuni hiyo imefanya jambo kubwa sana kwa mama lishe kuwapatia
msaada huo ambapo wengi wao wanashindwa kumudu kutokana na hali halisi
ya maisha kwa sasa.
Alisema kuwa kampuni hiyo
imeunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana dhidi
ya maambukizi ya virusi vya corona licha kwa sasa kupungua kwa kiasi
kikubwa hivyo kutokana na kazi kubwa ya mama lishe wanahitaji kuwa na
afya bora.
No comments :
Post a Comment