Waziri wa Nishati
Dkt.Medard Kalemani (wa pili kulia) Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais
(Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu,(wa tatu kulia) na
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said(wa kwanza kulia)
wakiwasili kwenye ukaguzi wa Bwawa la Mtera ambalo lipo Mkoani Iringa,
tarehe 7 Mei mwaka huu.
Waziri wa Nchi
Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu
(katikati), akizungumza na waandishi wa Habari mara baada kumaliza
kufanya ukaguzi wa Bwawa la Mtera Mkoani Iringa, Mei 7,2020.
Picha ya taswira ya Bwawa la
Kidatu ambalo Waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani na Waziri wa Nchi
Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu
walifanya ziara ya ukaguzi kwenye Bwawa hili lililopo Mkoani Morogoro,
Mei 7,2020.
Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said(aliyevaa miwani) akizungumza na
waandishi wa Habari mara baada kumaliza kufanya ukaguzi wa Bwawa la
Kidatu Mkoani Morogoro, Mei 7,2020.
Waziri wa
Nishati Dkt.Medard Kalemani(mwenye shati la bluu) akizungumza na
waandishi wa Habari mara baada kumaliza kufanya ukaguzi wa Bwawa la
Kidatu Mkoani Morogoro, Mei 7,2020.
Waziri wa Nishati
Dkt.Medard Kalemani(wa kwanza kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
Mhe.Loata Ole Sanare(katikakati) Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi
Zena Said(kulia) wakielekea kwenye ukaguzi wa Bwawa la kidatu, Mkoani
Morogoro, Mei 7,2020.
**********************************
Hafsa Omar-Morogoro -Iringa
Waziri wa Nishati
Dkt.Medard Kalemani tarehe 7 Mei mwaka huu amefanya ziara ya kikazi
kwenye kwenye vituo vya kufua umeme kwa maji vya Mtera na Kidatu
vilivyopo Mkoani Morogoro na Iringa.
Katika ziara yake
hiyo aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Mussa Hassan Zungu, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati
Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati na
Ofisi ya Makamu wa Rais(Mazingira).
Akizungumza na
waandishi wa habari, wakati akiwa kwenye ziara hiyo Dkt. Kalemani
alisema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha kuwa maji ya kutosha
yanapatikana ya kuzalisha umeme wa kutosha na wa uhakika pamoja na
kuangalia athari za mazingira kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha
nchini.
Dkt. Kalemani
alisema, kufuatia athari zilizojitokeza kipindi cha mvua wameunda timu
ambayo itakuwa chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said
itakayoshirikisha wataalamu mbalimbali ili kuja na mipango ambayo
itasaidia kuondoa athari zilizojitokeza katika mabwawa hayo.
Amesema kuwa,
Bwawa la Kidatu lina kimo cha mita 450 ambavyo ndio kimo chake cha juu
cha kujaa kwa maji na ikitokea yamejaa zaidi ya hapo yanahitajika
kufunguliwa, na kuruhusiwa kwenda mbele ili kwenda kulijaza Bwawa la
Rufiji, na kuwataka wataalamu wanaohusika na shughuli hiyo kuhakikisha
wanapoyafungulia hayaleti madhara yoyote ya kimazingira.
Ameongeza
kuwa,waatalamu hao wanapofunguliwa maji hawapaswi kuwafungulia na
kuwacha yakizaga badala yake wayafungulie ili kwenda kwenye mkondo wake
unaostahili, kwakuwa yanapozagaa ndio madhara yanapotokea kwa wananchi
ambao wanaishi kandokando ya maeneo hayo.
“ Tuna jukumu
kubwa la kuhakikisha maji hayaleti madhara nilipokuja kipindi cha nyuma
niliona madhara kwenye baadhi ya maeneo na ndio maana nikaunda timu
kupitia kwa Katibu Mkuu na baadhi ya viongozi wa Mikoa inayozunguka
bwawa hili wafanya uratibu ili kuhakikisha yasiendele kuleta madhara kwa
wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo lazima tuyalinde mazingira
yetu” alisema Kalemani.
Aidha, alitoa
wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya mito kuwa wachukue
tahadhari ili wasije wakathirika kipindi cha mvua kubwa, na kuwataka
kutunza vyanzo vya maji na kulima kwa ustarabu bila kuathiri vyanzo
hivyo.
Pia,
amewataka waatalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzani(TANESCO) kuhakikisha
kipindi ambacho kuna maji ya kutosha na umeme umezalishwa wa kutosha
wahakikishe kuwa umeme hauzimwi nchini kwasababu hakuna sababu ya
kufanya hivyo katika kipindi hiki.
Kwa upande wake,
Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamu Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa
Hassan, amesema lengo la Serikali ni kulinda vyanzo vya maji kwasababu
maji yakikosekana umeme utashindwa kuzalishwa nchini na umeme
usipozalishwa uchumi wa nchi yetu utayumba na nchi inategemea umeme na
umeme wa bei chini ni umeme unaotokana na vyanzo vya maji.
“vyanzo vya maji
vilindwe, vyanzo hivi visipolindwa vitashindwa kusafirisha maji kwenda
kwenye miradi mikubwa kama mradi wa umeme wa Julius Nyerere kwahiyo
lazima tuliende vyanzo vyetu kwa umakini zaidi” Alisema.
Aidha, amesema
ametoa siku kumi kwa timu iliyoundwa ambayo ipi chini ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati, kutoa taarifa rasmi ya namna gani sasa ya kwenda
kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na umeme wa uhakika unapatikana
nchini.
Nae, Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati Mhandisi Zena Said, amesema kuwa yeye na pamoja na
timu ambayo imeundwa watakaa na wataalamu mbalimbali ili kuangalia data
za miaka ya nyuma ili waweze kuona watazitumiaje kuweka mipango ya
kuzuia uharibifu usitoke kwenye vyanzo hivyo vya umeme.
No comments :
Post a Comment