Friday, May 8, 2020

Hotuba ya Utangulizi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anayeshughulikia Afrika Tibor Nagy



*********************************
Habari za asubuhi kwa wale mliopo Jijini Washington na nchini Marekani na habari za mchana kwa wale mliopo Barani Afrika. Asanteni sana kwa kujiunga nasi hivi leo katika
mkutano huu kupitia njia ya simu. Ni matumaini yangu kuwa ninyi pamoja na familia zenu mpo salama
tunapopita katika nyakati hizi ngumu sana na tunaendelea kufanya kila tunachoweza ili tuweze kuzivuka na kuendelea na maisha yetu.  

Nimekuwa katika kazi hii kwa takriban miaka miwili sasa, nikirejea katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani baada ya kustaafu utumishi wangu wa miaka 32 kama mwanadiplomasia hususan katika Bara la Afrika na nikishughulikia masuala ya Afrika. 

Baada ya maisha yangu yote ya utumishi na kuishi barani humo, nina matumaini makubwa kwamba sio tu tutalishinda janga hili na kuvuka kipindi hiki kigumu, bali pia ushirikiano wetu na watu wa Afrika utaimarika zaidi ya ilivyokuwa hapo awali. Ninasema hili kutokana na uzoefu na ufahamu wa kina kwamba dhamira yetu ya dhati kwa Afrika itasimama imara.  

Mbali na ushirikiano wetu wa muda mrefu katika masuala ya afya, tunafanya kazi pamoja katika kuimarisha utawala bora, kuongeza biashara na uwekezaji, kuimarisha maendeleo ya vijana wa Kiafrika na wajasiriamali wanawake pamoja na kuimarisha usalama. 

Kama Waziri wa Mambo ya Nje Pompeo alivyosisitiza mara kadhaa, huu ni wakati wa Marekani kuimarisha
ubia wetu wa muda mrefu na marafiki zetu wa Kiafrika.

Tuna historia ndefu ya kufanya kazi pamoja tukikabili changamoto mbalimbali za afya ya umma na nina imani kuwa uhusiano wetu na uzoefu wetu wa pamoja wa miongo kadhaa utatusaidia tunapokabiliana na janga la wakati huu.

Chini ya Rais Trump, ushirikiano huu umeendelea kuimarika zaidi na zaidi.  Marekani ndio
mfadhili mkubwa zaidi wa Bara la Afrika na matokeo ya kazi yetu yanaonekana katika nyanja
mbalimbali.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita Marekani imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 100 kusaidia afya ya umma barani Afrika na kutoa mafunzo kwa zaidi ya
wahudumu wa afya 285,000. Kwa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa
Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) pekee, maisha ya zaidi ya watu milioni 18 yameokolewa
katika kipindi cha miaka 18 iliyopita.  

Aidha, utawala wa Rais Trump unaendelea kufanya kazi ya kuokoa maisha barani Afrika kwa kusaidia miradi ya kupambana na Malaria, Ebola, Avian Flu na Kipindupindu. 

Mpango wa Rais wa Kudhibiti Malaria (President’s Malaria Initiative – PMI) umesaidia kuokoa maisha ya
zaidi ya watu milioni 7 na kuzuia zaidi ya visa bilioni moja vya maambukizi ya malaria katika
kipindi cha miaka 20 iliyopita. 

Pale ambapo mpango wa PMI unaendeshwa, vifo
vinavyotokana na Malaria vimepungua kwa asilimia 60 toka mwaka 2006.
  
Na hivi sasa tunapopambana na janga la COVID-19, dhamira na kujitoa kwetu kwa dhati
kunaendelea. Hakuna nchi yoyote inayofanya zaidi yetu.

Katika zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 780 ambazo Marekani imeahidi kuzitoa ili kukabiliana na virusi hivi duniani, takriban dola milioni 250 zinaelekezwa Afrika.

Hatua zetu zinakwenda mbali zaidi ya kutoa fedha hizi
za ziada. Katika nchi za Ghana, Senegal, Uganda, Sierra Leone na Mauritania, hospitali, magari ya kubebea wagonjwa na mahema yaliyokuwa yakitumiwa kwa ajili ya mipango ya kulinda amani yalibadilishwa ili kutumiwa katika jitihada za kukabiliana na COVID-19. 

Hali ya kuaminiana iliyojengeka baina yetu kwa miaka mingi imechangia kwa kiasi kikubwa kuwezesha Serikali za Kiafrika, mashirika ya ndege na wadau wengine kusaidia kurejeshwa nyumbani kwa zaidi ya Wamarekani 10,000 kutoka barani Afrika.  
Isitoshe, si tu serikali yetu ndiyo inayoongoza; tuna utaratibu wa nchi nzima kuchangia
tunaouita “all-of-America approach”.  Katika utaratibu huu, biashara, mashirika yasiyo ya
kiserikali na mashirika ya kidini nayo pia yamechangia.  Kwa pamoja, Wamarekani
wamechangia karibu Dola za Kimarekani bilioni 6.5, ikiwa ni pamoja na wataalamu
tuliowapeleka sehemu mbalimbali duniani na madaktari na wahudumu wengine wa afya ya
jamii wanaoendesha mafunzo kwa njia ya video pamoja na madaktari na wahudumu wengine
wa afya waliopata mafunzo kwa ufadhili wa Marekani na katika taasisi zake za kielimu.
  
Pia, huu ni wakati wa kutafakari kuhusu umuhimu wa uwazi. Nyakati kama hizi ndizo
zinazoonyesha ni nani unaweza kumuamini. Nina fahari kusema kuwa kwa kiwango kikubwa
wabia wetu wa Kiafrika wamesimama pamoja nasi kama ambavyo nasi tumesimama na kuwa
upande wao.  Kwa bahati mbaya, kuna watu wengine ambao hawana maadili haya,
wakiendelea kuiharibu dunia hii kwa usiri na uongo. 
Hivi karibuni tuliadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari na kwa masikitiko
makubwa tumeshuhudia baadhi ya nchi zikitumia janga la COVID-19 kuminya zaidi uhuru wa
vyombo vya habari, hususan katika kutoa kwa uhuru taarifa kuhusu janga hili. Hatua za serikali
za kukabiliana na janga la COVID-19 ni lazima zilenge katika kulinda afya ya umma. Serikali
zisiutumie ugonjwa huu kama kisingizio cha kuminya haki za watu au maoni yanayotolewa
katika vyombo vya habari au kwingineko. Vyombo vya habari vilivyo huru na thabiti ni
muhimu sana wakati huu ili kuhakikisha kuwa umma unapata kwa wakati taarifa sahihi kuhusu
virusi hivi na jinsi ya kudhibiti kuenea kwake.  Uwazi na uwajibikaji wa serikali pamoja na
uhuru wa kujieleza, ikijumuisha uhuru wa wanahabari ni muhimu sana katika kukabiliana na
COVID-19 kwa ufanisi.  Tunapotafakari kuhusu umuhimu wa uwazi na mambo mengine kama
vile misaada, madeni na taarifa za afya tunabaini kuwa kuna manufaa mengi na makubwa ya
kufanya kazi katika jamii huru na yenye uwazi kuliko ilivyo katika jamii ambayo haina vitu
hivyo. Ninaamini kuwa rafiki zetu wa Kiafrika wataona tofauti hii.
 
Kama kawaida, Marekani itaendelea kushirikiana na wabia wetu wa Kiafrika ili kukabiliana na
janga la COVID-19 na changamoto nyingine zozote zitakazojitokeza mbele yetu. Na kama ada,
tutavuka mtihani huu kwa afya na usalama wa Marekani na Bara la Afrika.

No comments :

Post a Comment