Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martin
Shigela (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald
Kusaya (wa kwanza kushoto) mara baada ya mazungumzo yao kuhusu mkakati
wa kukuza kilimo cha mpunga mkoani Tanga leo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya akiwa na Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mlingano
Dkt.Catherine Sendoro wakati alipotembelea kituo hicho wilayani Muheza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo
Bw.Gerald Kusaya akipata maelezo ya namna mbegu bora za mkonge
zinavyozalishwa kwenye vitalu kwa njia ya maabara.Kulia ni Mtafiti wa
zao la mkonge Gelleson Mkongwe wa kituo cha TARI Mlingano akitoa
maelezo
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyeinama) akiangalia mbegu
bora za zao la mkonge zilizozalishwa kwa njia ya maabara ya sayansi
katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano wilaya ya Muheza mkoa
wa Tanga.
Picha na habari na Wizara ya Kilimo.
……………………………………………………………….
Na.Bashiri Salum,Wizara ya Kilimo,Muheza
Watumishi wa sekta ya kilimo
nchini wametakiwa kufanya kazi kwa kujiamini na weledi ili kuongeza tija
katika kuhudumia wakulima na hivyo kufanya sekta ya kilimo iwe na
mchango
mkubwa katika uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo
(27.04.2020) wilayani Muheza mkoa wa Tanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo Gerald Kusaya wakati alipoongea na watumishi wa Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano na wale wa Chuo cha Mafunzo Kilimo
(MATI)Mlingano.
“ Watumishi msijione wanyonge
kwenye shughuli zenu,nataka mjiamini na muwe wabunifu katika kutekeleza
kazi za wananchi ili tija iongezeke kwa wizara na taasisi zake kutoa
huduma bora “ alisema Kusaya
Kusaya alisema ni wakati muafaka
sasa watafiti wa zao la mkonge kujikita katika kutoa matokeo chanya ya
mbegu kwani kuna maeneo mengi nchini kama wilaya za
Kahama,Kishapu,Kilosa na Geita wameonesha nia ya kuanzisha mashamba ya
zao la mkonge.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa
kituo cha TARI Mlingano ,Mkuu wa kituo hicho Dkt.Catherine Senkoro
alisema uzalishaji wa mbegu mpya za mkonge zenye uwezo mkubwa wa mavuno
umefikia mbegu 500,000 kati mahitaji ya wakulima ya mbegu 1,600,000 kwa
mwaka.
Dkt.Senkoro alisema kwa sasa wana
mkakati wa kuzalisha mbegu bora za mkonge kwa kutumia teknolojia ya
maabara na vipando ili kuweza kufikia lengo la kuzalisha mbegu 2,000,000
ifikiapo mwaka 2021.
Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu
aliagiza taasisi ya TARI Mlingano kuhakikisha inazalisha mbegu 5,000,000
kwa mwaka na kuwa Wizara yake itatoa fedha za kuwezesha utafiti na
uboreshaji maabara ya kupima afya ya udongo na ile ya kuzalisha mbegu
bora za mkonge.
“Wizara ya Kilimo ipo tayari
kusaidia kituo hiki kupata fedha za kutosha ili kuzalisha mbegu bora za
mkonge na kuwafikia wakulima wengi zaidi kama alivyoagiza Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa wakati alipotembelea kituo hiki Machi mwaka huu” alisema
Kusaya
Kwa mujibu wa Dkt.Senkoro kwa sasa
ekari moja inazalisha tani moja ya mkonge wakati China wanazalisha tani
tano kwa ekari na kusema taasisi hiyo inahitaji kuongezewa nguvu ili
izalishe mbegu bora zenye kutoa matokeo makubwa kwa wakulima.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu
huyo alitembelea na kuongea na watumishi wa wa Vyuo vya mafunzo ya
Kilimo ambapo aliwataka wawe watulivu wakati serikali ikifanya
maboresho na ukarabati wa miundombinu ya chuo hicho.
Kusaya aliwakumbusha watumishi hao
kuwa kazi ya ualimu ni ya wito hivyo wasichoke badala yake waifanye
kwa moyo na jitihada kufundisha vijana na wakulima mbinu bora za kilimo.
Katika kuhakikisha watumishi
wanakuwa na weledi wa kazi,Katibu mkuu Kusaya amewataka watumishi
kujitokeza na kuomba nafasi ya kwenda masomoni kujiendeleza kielimu na
kuwa serikali itawezesha .
“Katika kipindi hiki nataka
watumishi wa wizara ya Kilimo na taasisi waweze kujiendeleza kwa mafunzo
ya muda mrefu au mfupi ili wasaidie serikali kuboresha utoaji huduma
na tija katika usimamizi wa sekta ya kilimo nchini .” alisisitiza Kusaya
Nao watumishi Mary Zakayo na
Valentine Njau wa chuo cha MATI Mlingano walimuomba Katibu Mkuu asaidie
waweze kupata stahili zao za malipo ya likizo na madeni ya vibarua.
Akijibu maombi hayo ,Kusaya
alisema kuanzia mwezi ujao Mei watumishi hao watalipwa madeni yao kwani
Wizara imepokea tayari shilingi Bilioni Tano kulipa madeni ya watumishi
na watoa huduma kwa taasisi zote chini ya Wizara ya Kilimo..
No comments :
Post a Comment