Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi
wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima akitoa elimu kwa
wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga
dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara
ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la
Project CLEAR wakiendelea na uhamasishaji jinsi ya kujikinga dhidi ya
maambukizi ya virusi vya Corona kwa wafanyabiashara katika eneo la soko
la Mabibo Jijini Dar es Salaam.
Sfaff sergeant (S/Sgt ) Valentine
Ngowi, akitoa elimu kwa wafanyabiashara katika kituo cha daladala cha
feli Jijini Dar es Salaam.
Timu ya uhamasishaji kutoka Wizara
ya Afya kwa kushirikiana na Wadau kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la
Project CLEAR wakiendelea na utoaji elimu ya kujikinga dhidi ya
maambukizi ya virusi vya Corona kwa wafanyabiashara katika kituo cha
daladala cha feli Jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………….
Na WAMJW- DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
imetoa wito kwa wananchi kuteketeza Barakoa zao vizuri baada ya kumaliza
matumizi yake kisha kuitupa sehemu salama ili kuepusha kusambaa kwa
magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa homa kali ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya Corona.
Wito huo, ameutoa Mkuu wa Kitengo
cha maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike
Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam
kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya
Corona.
“Wale ambao mmevaa Barakoa (mask)
zile ambazo zinatakiwa kutupwa baada ya kutumika (disposable mask) ,
ukumbuke kabla hujaitupa uitoboe ili mtu mwingine asiweze kuiokota na
kuisafisha na kuirudisha katika mzunguko jambo litalosaidia kuepusha
magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa Corona” alisema.
Alisema, katika baadhi ya nchi
imethibitika kuwa, mgonjwa mmoja wa Corona anaweza kuambukiza mpaka watu
kumi kwa wakati mmoja hii inatokana na mwingiliano uliopo baina ya
watu, hivyo kutoa wito juu ya kuchukua tahadhari kwa hali ya juu.
“Kwa baadhi ya nchi zilizopata
maambukizi, inasemekana kuwa, mtu mmoja aliyeambukizwa virusi hivi
anauwezo wa kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja” alisema.
Aidha, alisema kuwa, kwa wale
ambao wanatumia Barakoa za kitambaa, kuhakikisha wanabadirisha mask hizo
kila baada ya masaa manne ili kuepusha kupata magonjwa mengine, huku
akisisitiza kuwa, ni muhimu kabla ya kuivaa zifuliwe kwa maji na sabuni
kisha ipigwe pasi ili kujiweka salama zaidi dhidi ya magonjwa.
“Kwa wale ambao mnavaa Barakoa
(mask) za kitambaa basi mkumbuke kuwa, mask hiyo inatakiwa ivuliwe kila
baada ya masaa manne mpaka sita, na hakikisha kuwa, unaifua kwa maji na
sabuni, umeinyoosha ili kama kuna virusi humo waweze kufa, usivae
barakoa (mask) ambazo ni chafu” alisema
Kwa upande wake, Sfaff sergeant
(S/Sgt ) Valentine Ngowi, alisisitiza kuwa, wazazi watoe elimu kwa
watoto kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona kwa
kuhakikisha wananawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, huku
akisisitiza waepuke kuzulula mtaani kuepusha kuokota Barakoa
zilizotupwa hovyo bila utaratibu.
Nae Balozi wa kampeni ya Mikoni
safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba), amewakumbusha
Watanzania kuepuka msongamano katika maeneo yote, huku akisisitiza kuwa,
kama hakuna sababu yakutoka nje ni vema watulie majumbani.
No comments :
Post a Comment