Friday, April 10, 2020

WATENDAJI SEKTA YA ARDHI OFISI ZA MIKOA WATAKIWA KUEPUKA URASIMU



Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo akizungumza wakati wa kufunga mafunzo kwa watendaji wa sekta ya Ardhi wa ofisi za Ardhi za mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida na Manyara yaliyofanyika ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma jana.

Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nhonge akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Watendaji wa sekta ya ardhi wa ofisi za Ardhi za mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida na Manyara yaliyofanyika ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma jana.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Watendaji wa sekta ya ardhi wa ofisi za Ardhi za mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida na Manyara yaliyofanyika ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma jana.

Watendaji wa sekta ya Ardhi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo (Hayupo pichani) wakati wa kufunga mafunzo kwa  Watendaji wa sekta ya ardhi wa ofisi za Ardhi za mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida na Manyara yaliyofanyika ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma jana (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA).
……………………………………………………………………………………………………..
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo amewataka
watendaji wa sekta ya ardhi katika ofisi za mikoa kuepuka urasimu na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria ili kutoa huduma bora na zenye tija kwa wananchi.
Alisema, pamoja na kutenda kazi kwa kuzingatia sheria, watendaji hao pia wanapaswa kuhakikisha wanashughulikia kero za wananchi kwa kukaa nao pamoja hasa pale wananchi wanapokosea kwa lengo la kuwasaidia badala ya kuwakatisha tamaa.
‘’Urasimu uishe, lengo hapa ni kumhudumia mwananchi na cha msingi ni kukaa pamoja na mteja na kumueleza alipokesea badala ya kumkatisha tamaa kwa kumzungusha, tuwaonee huruma na kuacha urasimu usio wa lazima’’. Alisema Mary.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Maofisa wa sekta ya ardhi katika mikoa ya Morogoro, Manyara, Singida na Dodoma katika ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma jana, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu na kutenda kazi kwa kasi na kusisitiza kuwa kazi katika maeneo wanayotoka ni nyingi na zinahitaji kushughulikiwa.
Kwa mujibu wa Mary Makondo, watendaji hao ambao ni Makamishna na Wasajili Wasaidizi wa ofisi za ardhi za mikoa wahakikishe wanatoa kipaumbele katika kushughulikia migogoro ya ardhi kwa haraka pamoja na kutilia mkazo mafunzo ya ndani kwa watumishi.
Aidha, alihimiza utoaji huduma nzuri kwa wateja wanaokwenda kupata huduma katika ofisi za mikoa na kubainisha kuwa suala hilo linahitaji uvumilivu mkubwa na wakati mwingine kushirikisha  wataalamu wengine wa ofisi moja ili kuja na uamuzi  utakaohusisha mawazo ya wengi.
Akigeukia utoaji hati za ardhi, Mary Makondo aliwataka watendaji hao kuhakikisha wanaongeza idadi ya utoaji hati miliki za ardhi kwenye maeneo yao zikiwemo hati za kimila, urasimishaji  na leseni za makazi sambamba na kuhakikisha fidia zinalipwa kwa wakati hususan maeneo yaliyotwaliwa kwa shughuli mbalimbali.
Vile vile, katibu Mkuu Wizara ya Ardhi aliwataka watendaji hao wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanapata taarifa zote za makampuni ya urasimishaji na mikataba yao na wakati huo makampuni hayo kufuata miongozo ikiwemo bei elekezi ya urasimishaji.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha alieleza kuwa mafunzo hayo ya watendaji wa sekta ya ardhi kutoka ofisi za mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida na Manyara yatawawezesha watendaji wa ardhi wa mikoa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na aina ya mafunzo waliyoyapata ikiwemo namna ya kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Alisema, watendaji hao walipatiwa mafunzo katika masuala ya ukusanyaji kodi ya pango la ardhi, upimaji na ramani, mipango miji sambamba na masuala ya maendeleo ya makazi aliyoyaeleza kuwa watakuwa wakikutana nayo katika utendahji wa kazi za kila siku.

No comments :

Post a Comment