Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
……………………………………………………………….
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, imefanikiwa kuokoa sh284.6
milioni, baada ya
kufuatilia miradi mbalimbali ya sh7.3 bilioni, kwenye
baadhi ya Halmashauri za mkoa huo.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara,
Holle Joseph Makungu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari mjini Babati.
Makungu alisema wamefanikiwa
kurejesha serikalini fedha hizo katika kipindi cha utendaji kazi wao kwa
muda wa miezi mitatu kwa kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema wamefanikiwa kuokoa fedha
hizo ambazo zimerejeshwa serikalini kupitia operesheni za uchunguzi,
udhibiti, ufuatiliaji na urejeshwaji wa fedha mbalimbali kwenye baadhi
ya halmashauri za mkoa huo.
Alisema katika kipindi hicho cha
robo mwaka wamefanikiwa kurejesha fedha sh66.3 milioni kupitia akaunti
ya Takukuru na sh180 milioni kwenye akaunti ya mamlaka ya mapato nchini
(TRA).
Alitaja baadhi ya fedha hizo
zilizookolewa zimetokana na operesheni tofauti ikiwemo ukwepaji kodi
sh180 milioni na mrejesho wa vyama vya ushirika sh36.6 milioni.
“Fedha nyingine zilizookolewa ni
sh30.2 milioni za posho za madiwani walizorejesha kwa kulipwa bila
kustahili na sh16 milioni zilizorudishwa na mmoja kati ya mzabuni wa
halmashauri,” alisema Makungu.
Alitaja fedha nyingine ni sh1.3
milioni za michango ya wanachama wa CCM zilizorejeshwa kwa katibu wa CCM
wilaya ya Kiteto baada ya wakusanyaji wa fedha hizo kutoziwasilisha
sehemu husika.
Alisema fedha nyingine ni
sh400,000 zilizorejeshwa kupitia akaunti ya mkuu wa wilaya ya Kiteto
kati ya sh1.2 milioni za makusanyo ya vitambulisho vya ujasiriamali.
“Huu ni utekelezaji wa maagizo na
maelekezo ya Rais John Magufuli juu ya ufuatiliaji wa fedha zote za
vyama vya ushirika ambapo baadhi walikopeshwa na kuendelea kukaa nazo
bila kuzirejesha kinyume na utaratibu,” alisema Makungu.
No comments :
Post a Comment