********************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amepokea kutoka kwa wadau msaada wa fedha pamoja na
vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya
mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya
sh. bilioni 6.226.
Baada ya
kupokea kupokea msaada huo, Waziri Mkuu amewashukuru wadau hao kwa
kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya
corona, ambapo hadi sasa kesi 24 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa
huo nchini na wagonjwa watano wamepona.
Waziri Mkuu
amepokea msaada huo leo (Jumatano, Aprili 8, 2020) katika Ofisi Waziri
Mkuu Mlimwa, jijini Dodoma. Amewataka Watanzania waendelee kushirikiana
na Serikali katika kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Amesema hadi
sasa jumla ya watu 396 wapo kwenye karatini katika maeneo mbalimbali
yaliyotengwa wakiwemo wageni wanaoingia nchini ambao wanafuatiliwa afya
zao na baada ya siku 14 kama watakuwa hawana maambukizi wataruhusiwa
kuungana na familia zao.
Waziri Mkuu
amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua mbalimbali katika
kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na kwa sasa imejiimarisha kwenye utoaji
wa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona.
“Serikali
inatoa misitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu
kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo kunawa mikono kwa
sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya
lazima.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam waendelee kuchukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae kwa sababu hadi
sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi wa corona nchini.
Pia, Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuvishukuru vyombo vya habari nchini kwa
ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na
virusi vya corona pamoja na wasanii waliotunga nyimbo za kuuelimisha
umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.
Miongoni mwa
wadau waliotoa msaada huo ni kampuni ya Madini ya Twiga iliyotoa sh.
bilioni nne, mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz ametoa sh.
bilioni moja, kampuni ya Taifa Gesi imetoa sh. milioni 100 na kampuni ya
mafuta ya Puma imetoa msaada wa mafuta lita 50,000 zitakazotumika
katika magari yanayotoa huduma za kupambana na corona nchini yakiwemo
magari ya kubebea wagonjwa.
Wengine ni
kampuni ya TEHAMA ya Huawei imetoa vifaa kuendeshea mikutano kwa njia ya
video ambavyo ni cloudlink camera tatu, Cloudlink Mic tatu, Cloudlink
TV terminal tatu, Cloudlink Platform pamoja na Thermal Imaging
Temperature Measuring System moja vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni
940, Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetoa sh. milioni 79.
Baada ya
kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli
aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya
kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia
Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Kuhusu wadau
wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema ofisi yake iko
wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto na kwa walio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza
kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National
Relief Fund Electronic.
Awali, mfanyabiashara
maarufu nchini, Rostam Azizi alisema ametoa sh. bilioni moja ambayo
ameielekeza katika kununua vitakasa mikono ambavyo vitatumiwa na
wasafiri wa daladala wa Dar es Salaam na Zanzibar ili waweze kutumia
kabla ya kupanda usafiri huo, hivyo kuweza kujikinga.
Pia,
Mfanyabiashara huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John
Magufuli kwa kuwaongoza Watanzania kwa hekima na busara na kuwaepusha na
taharuki kama ilivyotokea katika mataifa mengine. Amempongeza Waziri
Mkuu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa
namna wanavyoshiriki katika kukabiliana na corona.
No comments :
Post a Comment