Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Msaafu) George
Huruma Mkuchika (Mb) akizungumza wakati wa Mahafali ya 28 ya Chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Kampasi ya Mbeya.
………………………………………………………………..
James Mwanamyoto – Dodoma
Waajiri katika Taasisi za Umma
wenye watumishi ambao hawajapata mafunzo ya namna
Serikali inavyofanya
kazi, wametakiwa kuwapeleka watumishi hao kupata mafunzo Chuo cha
Utumishi wa Umma mapema iwezekanavyo kabla ya kuchukuliwa hatua kwa
kupuuza Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma 2009, kanuni ya G.1
(8).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt.
(Mst.) Mhe. George Huruma Mkuchika (Mb) alipokuwa akisisitiza umuhimu wa
Watumishi wa Umma kupata mafunzo ya namna Serikali inavyofanya kazi
ikiwa ni pamoja na kupewa elimu juu ya miiko ya kiutendaji katika
Utumishi wa Umma.
Mhe. Mkuchika amesema, Serikali
haitosita kumchukulia hatua za kinidhamu mwaajiri yeyote ambaye
hatawapeleka watumishi wake Chuo cha Utumishi wa Umma kupata mafunzo ya
namna Serikali inavyofanya kazi kwani mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea
ufanisi wa kiutendaji.
“Kanuni G.1 (8) ya Kanuni za
Kudumu katika Utumishi wa Umma 2009 inasema; kila mwajiri anawajibika
kupanga na kusimamia mafunzo elekezi kwa watumishi wapya walioajiriwa,
hivyo mtumishi wa umma akishaajiriwa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu
yake anapaswa kupata mafunzo ya namna Serikali inavyofanya kazi, kwa
mantiki hiyo ni kosa kwa mwajiri kutompatia fursa hiyo ya mafunzo”, Mhe.
Mkuchika amesisitiza.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa,
zamani hakukuwa na fursa kubwa ya watumishi kupata nafasi ya kujifunza
utendaji kazi Serikalini katika Chuo cha Utumishi wa Umma, lakini hivi
sasa chuo kina kampasi 6 ambazo ni Dar es Salaam, Mtwara, Tanga,
Singida, Mbeya na Tabora hivyo ni wajibu wa waajiri kuwapeleka watumishi
katika kampasi hizo.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewapongeza
Watumishi wa Umma kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato, ambao
umewezesha uboreshwaji wa miundombinu katika sekta za Afya, Elimu,
Barabara na Reli hivyo kuboresha utoaji huduma kwa umma.
No comments :
Post a Comment