Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akinawa mikono kama njia ya
kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Korona katika Karakana ya Mamlaka
ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akitoa maelekezo kwa Meneja wa
Karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Mbeya,
Mhandisi Ezekiel Mong’ateko, mara baada ya kukagua vichwa viwili vya
treni ya shirika hilo vilivyofungwa mashine ya kufua umeme (traction
motor) mpya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akimsikiliza Meneja wa Karakana ya
Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Mbeya, Mhandisi Ezekiel
Mong’ateko, wakati akimweleza hatua ya ukarabati iliyofikiwa katika
karakana ya tazara mkoani Mbeya.
Muonekano wa moja ya Vichwa vya
treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) vilivyokamilika
baada ya kufungwa mashine ya kufua umeme (Tranction Motor), katika
karakana ya Mamlaka hiyo Mkoni Mbeya.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza na wafanyakazi wa
karakana ya maelekezo Karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia
(TAZARA) mkoani Mbeya (hawapo pichani) wakati alipokagua maendeleo ya
ukarabati wa vichwa vya treni mkoani humo.
Muonekano wa vifaa vinavyofanyiwa ukarabati katika karakana ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) mkoani Mbeya.
Mafundi wa Mamlaka ya Reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA) mkoani Mbeya, wakiendelea na ukarabati wa
vichwa vya treni katika karakana hiyo mkoani humo. TAZARA iko katika
hatua za mwisho za kukamilisha ukarabati wa kichwa cha tat umara baada
ya kufunga traction motor mpya.
………………………………………………………………………………………………
Serikali ya Tanzania imetoa kiasi
cha shilingi bilioni 10 ikiwa ni kuhakikisha inaifufua upya Mamlaka ya
Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuiongeza mtaji na kufikia lengo
la
kujiendesha kibiashara.
Akizungumza mkoani Mbeya mara
baada ya kukagua vichwa viwili vilivyokamilika baada ya kufungwa mashine
mpya za kufua umeme (traction motor) Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema kuwa kukamilika kwa
ukarabati huo kutaongeza usafirishaji wa mzigo kwa mamlaka.
“Makusudi makubwa ya Serikali
kuwekeza fedha hizi ni kuhakikisha mnafanya biashara na kurejesha mzigo
wa tani milioni tano mnaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka”, amesema
Mhandisi Kamwelwe.
Kamwelwe amefafanua kuwa fedha
hizo zilizotolewa zimeshanunua mashine mpya za kufua umeme takribani
arubaini na mbili ambazo zitafungwa kwenye vichwa saba.
Meneja Karakana ya TAZARA
mkoani humo, Mhandisi Ezekiel Mong’ateko, amesema mpaka sasa vichwa
viwili vimeshakamilika na mwishoni mwa mwezi huu kichwa cha tatu
kitakamilika ambapo kichwa kimoja kina uwezo wa kusafirisha tani laki
mbili na nusu kwa mwaka.
“Kukamilika kwa vichwa hivi
kutaongeza mzigo tunaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka kwani kwa sasa mzigo
tunasafirisha umepungua sana na hauzidi tani laki tatu, tunaishukuru
sana Serikali kwa kuiwezesha mamlaka”, amesema Mhandisi Mong’ateko.
Mhandisi Mong’ateko ameongeza
kuwa sambamba na ukarabati wa vichwa hivyo mkoani humo, Mamlaka
inaendelea na ukarabati wa mabehewa katika karakana ya mamlaka jijini
Dar es Salaam ili kuhakikisha ukamilikaji wa vichwa hivyo unaendana na
ongezeko la usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kukamilika kwa ukarabati wa
vichwa hivyo kutaongeza idadi ya vichwa kumi na tatu vilivyopo kwa sasa
na kufikia vichwa 20 ambapo kila kichwa kina uwezo wa kubeba tani elfu
thelathini.
Utoaji wa fedha hizo ni
utekelezaji wa makubaliano ya nchi Mbili ya Tanzania na Zambia ambazo
kwa pamoja zilikubaliana kutoa bilioni 20 ambapo kila nchi ilitakiwa
kuchangia bilioni kumi ili kuifufua upya mamlaka hiyo na kuiwezesha
kujitegemea mara baada ya kushuka kwa usafirishaji kutokana na upungufu
wa vichwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments :
Post a Comment