Friday, April 10, 2020

TAKUKURU Yatoa Tathmini Ya Mafanikio Mwaka 2019-2020


Habari Ndugu Wahariri wa Vyombo vya Habari pamoja na waandishi wa habari mlioko hapa,

Kwanza, nianze kwa kuwashukuru sana kwa kuitikia wito wetu.


Hii ni mara yangu ya kwanza kuwaiteni kwa lengo la kuzungumza nanyi, tangu niteuliwe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Machi 26, 2020 - takriban wiki mbili zilizopita.


Nimewaita hapa kama kundi la kwanza kabisa kukutana nalo, kutokana na umuhimu wenu kwa TAKUKURU katika kufanikisha mapambano dhidi ya Rushwa.


Ndugu Wahariri,
TAKUKURU inafahamu kwamba VYOMBO VYA HABARI ni wadau muhimu sana na pia ni kiungo kikuu kati yetu na jamii ya Watanzania ambayo ndiyo tunayoitumikia.


Bila kufikisha habari kwa wananchi kupitia VYOMBO VYA HABARI, Wananchi na wadau wetu hawawezi kufahamu:
  • Jitihada zinazofanywa na Serikali yao katika Kuzuia na Kupambana na Rushwa;
  • Jamii haiwezi kufahamu Rushwa ni nini na madhara yake kwa jamii ni yepi,
  • Mwananchi hawezi kufahamu nini haki zake na ni wapi afikishe malalamiko yake dhidi ya Rushwa.
  • Jamii haiwezi kupata fursa ya kushirikishwa katika mapambano dhidi ya rushwa.

Hivyo basi, kutokana na umuhimu huo niliona ni vema nikutane nanyi mapema sana.

 
Ninashukuru kwamba licha ya kuwa mwaliko huu ulikuwa ni wa muda mfupi (short notice) lakini bado mmeweza kufika.

Ndugu Wahariri,
Katika mazungumzo yangu ya leo nitazungumzia maeneo makuu manne yafuatayo:
  1. Mafanikio katika Utendaji Kazi wa TAKUKURU kwa mwaka 2018/ 2019;
  2. Mikakati tuliyojiwekea na tunayoendelea nayo katika mwaka huu wa 2020/2021 ikiwa ni pamoja na tulivyojipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Viongozi wa mwaka 2020;
  3. Ushirikiano na vyombo vya habari katika kuuhabarisha umma juu ya jitihada za Serikali za kuzuia na kupambana na Rushwa nchini; na mwisho ni
  4. Wito wangu kwa jamii ya Watanzania ambao ndiyo tunaowatumikia.

Ndugu Wahariri,

I. MAFANIKIO KATIKA UTENDAJI KAZI WA TAKUKURU KWA MWAKA 2018/ 2019;

Kama ambavyo mlisikia wasilisho langu la Taarifa ya Utendaji Kazi wa TAKUKURU niliyoitoa kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 26, 2020 nilieleza kwamba:

Sote tunatambua kuwa madhara ya kansa ya rushwa ni makubwa sana kwani husababisha:
  • Dhuluma kwa wananchi wanyonge,
  • Kutotekelezwa vyema kwa miradi ya maendeleo ambayo huligharimu Taifa fedha nyingi sana,
  • Husababisha ukwepaji kodi na upotevu wa fedha za serikali, na pia husababisha
  • Wananchi kukosa huduma bora za huduma za kijamii.

Kwa sababu hiyo, ni wajibu wetu sote – Sisi TAKUKURU na kila Mtanzania, kuhakikisha kwamba tunapambana na rushwa kwa mapana yake yote.

Ndugu Wahariri,

Katika taarifa ile nilisisitiza na kumuahidi Mhe. Rais kwamba TAKUKURU itaendelea kuwa mstari wa mbele kabisa katika kuimarisha jitihada za kuijenga Tanzania Mpya ambayo INAWEZEKANA BILA RUSHWA.

Ninaomba nirudie kuitoa ahadi hiyo kwa Watanzania kupitia hadhira hii kwamba, TAKUKURU itahakikisha kwamba Tanzania mpya inayojengwa na Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitakuwa mahala salama kwa WALARUSHWA AU MAFISADI.

A. TATHIMINI YA UTENDAJI KAZI 2018/2019

Ndugu Wahariri,

Sasa tuangalie TAHIMINI YA UTENDAJI KAZI WA TAKUKURU KWA UJUMLA:
Kama mnavyofahamu, TAKUKURU ndicho chombo chenye dhamana kisheria ya kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Taasisi hii inatekeleza majukumu yake ya msingi ya kuchunguza na kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kuwafikisha washitakiwa mahakamani;

Pia tunafanya utafiti na udhibiti wenye lengo la kubaini na kuziba mianya ya rushwa kwenye sekta za umma na binafsi; na vilevile tunawaelimisha wananchi kuhusu madhara ya rushwa na kuwahamasisha ili waweze kushirikiana na Serikali yao katika mapambano dhidi ya rushwa na kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika mapambano haya.

Ndugu Wahariri,
  • Katika kipindi cha mwaka 2018/19, utekelezaji wa malengo ya msingi ya TAKUKURU ulifikiwa kwa wastani wa asilimia 88.1 ambapo mwaka jana (2017/2018) utekelezaji ulifikiwa kwa asilimia 81.4. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 6.7.
  • Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa kiasi cha fedha kilichookolewa kutoka shilingi bilioni 70.3 kwa mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 82.8 kwa mwaka 2018/2019.
  • Vile vile idadi ya Miradi ya Maendeleo iliyofanyiwa ufuatiliaji iliongezeka kutoka miradi 691 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,494 hadi miradi 1,106 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,668.
  • Pamoja na utendaji huo, mafanikio haya tunaweza kusema yamechangiwa na mifumo thabiti ya usimamizi na ufuatiliaji wa utendaji kazi wetu unaozingatia Mpango Mkakati wa TAKUKURU (PCCB STRATEGIC PLAN) ambao umetuwekea vigezo vya kujitathimini.

Ndugu Wahariri,

B. UCHUNGUZI NA MASHTAKA

Katika kipindi husika, Taasisi imechunguza na kukamilisha majalada 911 yenye kuhusisha tuhuma mbalimbali. Kati ya majalada haya:
  • Majalada 266 yalihusu hongo;
  • Majalada 645 yalihusu vifungu vingine vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007;
  • Majalada 388 yaliwasilishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kuombewa kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani ambapo kati ya majalada hayo, majalada 277 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani yakiwemo majalada tisa (9) ya kesi za rushwa kubwa.
  • Kesi mpya 497 zilifunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya kesi zilizoendeshwa mahakamani kufikia 1,013.
  • Kati ya kesi mpya zilizofunguliwa mahakamani, kesi 4 zilihusu rushwa kubwa ambazo zilifunguliwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (maarufu kama Mahakama ya Rushwa na Mafisadi).
  • Kesi 341 ziliamuliwa mahakamani ambapo kesi 206 watuhumiwa wake walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini wakati kesi 135 watuhumiwa wake hawakukutwa na hatia.
  • Vilevile, kiwango cha kushinda kesi kiliongezeka na kufikia asilimia 62.41 ikilinganishwa na asilimia 60.1 ya mwaka 2017/2018.
Ndugu Wahariri,

Katika kipindi husika, kiasi cha Shilingi bilioni 82.8 kimeokolewa kwenye operesheni mbalimbali zilizoendeshwa au kuratibiwa na TAKUKURU. Kiasi hiki kinahusisha
  • Fedha taslim Shilingi bilioni 5.5 zilizorejeshwa Serikalini
  • Mali zenye thamani ya shilingi bilioni 59.1 na
  • Kiasi cha shilingi bilioni 18.2 kilichodhibitiwa baada ya Taasisi kuingilia kati baadhi ya chunguzi na kuwezesha fedha hizo kurejeshwa kwenye matumizi sahihi yaliyokuwa yamekusudiwa.

Ndugu Wahariri,
  • Kiasi cha shilingi bilioni 5.5 kilichookolewa kwa mfumo wa fedha taslim kimehifadhiwa kwenye akaunti mbalimbali:
  • Shilingi milioni 661 ziliingizwa kwenye akaunti ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU iliyopo Benki Kuu;
  • Shilingi bilioni 3.3 zimehifadhiwa katika akaunti za Mamlaka ya Mapato nchini; na
  • Shilingi bilioni 1.6 zimehifadhiwa katika akaunti za Halmashauri za Wilaya na Katibu Tawala wa Mikoa husika ambako operesheni hizo zilifanyika.
  • Vilevile, katika kipindi hiki TAKUKURU imewekea ZUIO mali za washtakiwa zenye thamani ya:
  • Shilingi bilioni 25.3,
  • Dola za Marekani milioni 5.7,
  • Magari 14 na
  • Nyumba 16

Lengo la kuweka zuio hili, ni kukamilisha taratibu za kisheria za kuzitaifisha mali hizo na kuzirejesha Serikalini.

Ndugu Wahariri,

C. UZUIAJI RUSHWA

Mojawapo ya jukumu la msingi na hatua muhimu katika mapambano ya rushwa ni UZUIAJI RUSHWA kwa kubaini mianya ya rushwa na kupendekeza hatua au njia sahihi za kuiziba mianya hiyo katika mifumo mbalimbali.
Katika kipindi cha mwaka 2018 na 2019, TAKUKURU ilifanya TAFITI tano zifuatazo:
  1. Ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya kimkakati ya Jiji la Dar es Salaam. (Utafiti huu ulihusisha Ubungo Bus Terminal na Maegesho ya Jiji).
  2. Ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa mifumo ya kielektroniki (Point of Sale - POS).
  3. Ukusanyaji wa mapato ya kodi kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (Electronic Fiscal Device - EFD).
  4. Ukusanyaji wa kodi ya majengo nchini pamoja na
  5. Uandaaji na Usimamizi wa Mitihani ya Taifa.

Ndugu Wahariri,
Kutokana na tafiti hizo, TAMISEMI, Baraza la Mitihani la Taifa, na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania zilishauriwa kuchukua hatua za kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.

Ndugu Wahariri,
Vilevile, katika kutekeleza jukumu la uzuiaji rushwa TAKUKURU ilifanya kazi 573 za Uchambuzi wa Mifumo mbali mbali ya Serikali. Pia ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa matokeo ya utafiti na uchambuzi huo - Taasisi iliandaa jumla ya warsha 368 za kukutana na wadau ili kujadili mianya iliyobainishwa na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya luiziba mianya hiyo.

Ni imani ya TAKUKURU kuwa iwapo Taasisi husika zitazingatia na kutekeleza ipasavyo mapendekezo yaliyotokana na tafiti zetu, kiwango cha makusanyo ya mapato ya Serikali kitaongezeka na pia kutakuwa na ufanisi zaidi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

D. UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Katika kipindi cha mwaka 2018/ 2019,

Miradi 1,106 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1,668.2 ilifuatiliwa ambapo asilimia 98 ya miradi hiyo ilihusu sekta za kipaumbele za Maji, Ujenzi, Afya na Elimu.

Katika Ufuatiliaji huo;
  • Miradi 113 yenye thamani ya shilingi bilioni 99.3 ilibainika kuwa na mapungufu mbalimbali ikiwemo ubadhirifu na ukiukaji wa taratibu za manunuzi ambapo hatua za kuanzisha uchunguzi zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha watuhumiwa wa ubadhirifu huo mahakamani.

Ndugu Wahariri,

E. UELIMISHAJI UMMA

Katika kipindi husika, TAKUKURU ilielimisha jamii kwa lengo la kuwahamasisha kushiriki katika vita dhidi ya rushwa kwa kupitia njia mbalimbali za uelimishaji zikiwemo:
  • Semina 2,513,
  • Mikutano ya hadhara na mijadala ya wazi 3,273,
  • Kushiriki katika maonesho 335,
  • Uandishi wa makala 569
  • Uandaaji na urushaji wa vipindi vya redio na televisheni 372.
  • Aidha, filamu ya BAHASHA yenye kutoa ujumbe wa makatazo ya rushwa ilionyeshwa kwenye baadhi ya mikesha ya Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Ndugu Wahariri,

II. MIKAKATI TULIYOJIWEKEA KATIKA MWAKA WA 2020/2021 PAMOJA NA NAMNA TULIVYOJIPANGA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA VIONGOZI WA MWAKA 2020;

Katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi sasa Aprili 2020, TAKUKURU imeendelea na utekelezaji wa majukumu yake tuliyokabidhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007.

Hata hivyo, zipo chunguzi na operesheni mbalimbali ambazo tumezitekeleza ili kuhakikisha kuwa Rushwa katika Taifa letu – INADHIBITIWA. Kazi hizo ni pamoja na zifuatazo:
  • Uchunguzi dhidi ya RIPOTI YA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA YA MWAKA 2018/2019.
  • Uchunguzi huu ni wa ile taarifa iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga - Novemba 26, 2019 na kupewa TAKUKURU kuchunguza vitendo vya ubadhirifu na rushwa katika matumizi ya fedha za ushirika nchini Tanzania.
  • Kwa mujibu wa muhtasari wa taarifa iliyokabidhiwa TAKUKURU, jumla ya fedha ambayo ilikuwa na viashiria vya vitendo vya ubadhirifu na rushwa ilikuwa ni zaidi ya Shilingi Bilioni 124 (124,053,250,874.00).
  • Uchunguzi dhidi ya tuhuma hii unafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza tuliitolea taarifa Januari 22, 2020 na awamu ya pili tuliitolea taarifa Machi 14, 2020.
  • Hadi tulipokamilisha awamu ya II ya uchunguzi huu Machi 14, 2020, tulikuwa tumefanya yafuatayo:
  • Kiasi cha fedha kilichochunguzwa kilifikia Shilingi Bilioni 66,255,488,545.73;
  • Tayari tumeokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 8,898,661,156.88;
  • Tunaendelea na uchunguzi wa Shilingi Bilioni 57,356,827,388.85;
Kupitia hadhira hii, tunaendelea kutoa wito kwa wanaushirika wote nchini, wakiwemo viongozi wa Vyama vya Ushirika na wafanyabiashara walionunua mazao ya wakulima au mtu mwingine yeyote mwenye fedha za ushirika, kurejesha fedha za Vyama vya Ushirika mara moja.


Ndugu Wahariri,

Operesheni kama hizi zinaendelea kufanyika nchi nzima ili kuhakikisha kuwa wale wachache wenye nia ya kuwadhulumu wafanyabiashara na wakulima wanyonge wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Kama tunavyofahamu, Vyama vya Ushirika vina jukumu la kuwasaidia wakulima kupata masoko ya mazao yao kwa lengo la kuwaendeleza kiuchumi na kijamii.


Vilevile, kupitia vyama hivi, wakulima hupaswa kupata utalaam, pembejeo pamoja na mikopo mbalimbali ili kuboresha na kuimarisha kilimo pamoja na masoko ya mazao ya wakulima. LAKINI, malengo haya muhimu yanashindwa kufikiwa kutokana na MAFISADI wachache wanaowadhulumu wakulima wanyoge na kutumia mazao hayo ya wakulima kujinufaisha kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya Mwaka 2007.
  • OPERESHENI DHIDI YA MIKOPO UMIZA
Katika tukio jingine, TAKUKURU imeendelea kupambana na wakopeshaji wa mitaani ambao wamekuwa wakiwabambikiza watumishi wakopaji - riba kubwa kupita kiasi na ambazo kisheria hazikubaliki.

Uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa waathirika wakubwa wa uwepo wa kikundi hiki ni wastaafu na hususani Waalimu.

MIFANO MBALIMBALI YA MIKOPO:
  • Mstaafu mmoja alikopa kiasi cha sh 900,000/= ili alipe sh 1,260,000/= kwa riba ya 40% ambayo bado iko juu, lakini alilazimika kulipa sh milioni 12,500,000/=. Malipo haya ni sawa na RIBA YA ASILIMIA 1,388%.
  • Mstaafu mwingine alikopa kiasi cha sh milioni 5,000,000/= ili alipe sh milioni 7,000,000/= sawa na 40% lakini badala yake akalipa sh milioni 20,000,000/= sawa na RIBA YA ASILIMIA 300%.

Ndugu Wahariri,
Kwa mkoa wa Mara pekee, hadi kufikia Aprili 2020 tayari tumefanikiwa kuwarejeshea wastaafu fedha walizokuwa wameporwa na wakopeshaji kiasi cha Shilingi Milioni 289,000,000/= pamoja na nyumba moja ya MJANE yenye thamani ya shilingi milioni 40

Kwa ujumla, kupitia Operesheni hii TAKUKURU imefanikiwa kurejesha kiasi kikubwa cha fedha lakini pia kurejesha furaha na UHAI ambao Waalimu Wastaafu tayari WALISHAKATA TAMAA YA MAISHA.

Lifuatalo ni jedwali kuonesha urejeshaji wa fedha kupitia operesheni hii uliofanyika katika baadhi ya mikoa nchini:

S/N MKOA KIASI CHA FEDHA KILICHOREJESHWA
1 MARA • Fedha taslim 289,000,000
• Nyumba moja (40,000,000)
2 TABORA 41,200,000 Wilaya ya Kaliua
3 KATAVI 29,000,000
4 MWANZA 17,440,375
5 KAGERA 10,000,000
6 NJOMBE 5,000,000
7 RUKWA Wamekamata Mkopeshaji mwenye Kadi 85 za Banki

NB: Fedha hizi zilirejeshwa kwa Wastaafu mbele ya Wakuu wa Mikoa au Wilaya husika kama ambavyo mtaona katika PICHA zilizoandaliwa.
  • KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA VIONGOZI – OKTOBA 2020
Ndugu Wahariri,

Sote tunafahamu kwamba mwezi Oktoba, 2020 nchi yetu itakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Vilevile, sote tunafahamu kuwa uchaguzi unapogubikwa au kuhisiwa tu kwamba kumejitokeza vitendo vya rushwa, uchaguzi huo unakosa uhalali wa kisiasa na hivyo kusababisha uvunjifu wa amani pamoja na wananchi kuikosa imani na Serikali iliyoko madarakani.

Kutokana na sababu hiyo, mwezi Aprili 2019, TAKUKURU iliona kuna umuhimu wa kuandaa warsha iliyokutanisha wadau kutoka Sekta mbalimbali, ambapo kwa pamoja tulijadili namna ya kudhibiti vitendo vya rushwa katika chaguzi na kisha tulijiwekea mikakati madhubuti ya kudhibiti tatizo hilo katika chaguzi zetu.

Kupitia Warsha hii tulijipanga vema kwa ajili ya Uchaguzi katika ngazi ya Serikali za Mitaa na pia tuliweka mikakati kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Ndugu Wahariri,
Kwa kushirikiana nanyi leo hii tungependa tuwakumbushe wananchi mambo muhimu kadhaa yanayohusu suala zima la uchaguzi. Tunafanya hivi kwakuwa tayari yapo mambo mambo ya SINTOFAHAMU amba yo tayari yameanza kujitokeza majimboni na taarifa zake kubainishwa na TAKUKURU:

MASWALI MUHIMU YA KUJIULIZA:

A. NI YEPI MAJUKUMU YA WABUNGE NA VIONGOZI WA SERIKALI KAMA WAZIRI, NAIBU WAZIRI, KATIBU MKUU, NAIBU KATIBU MKUU - KATIKA MAJIMBO?.

ANGALIZO: Kuna baadhi ya watu, wao si watendaji wa Serikali na wala si Wabunge katika maeneo husika …LAKINI tayari wameanza kukusanya wananchi na kuzungumza nao maneno ya ushawishi.

Watu kama hao TAKUKURU inawashughulikia kwa mujibu wa sheria.

1.1 Majukumu ya Mbunge (akiwemo Waziri na Naibu Waziri) katika majimbo yameainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ifuatavyo:-
  • 63(3) Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza-
  • Kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;
  • Kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti;
  • Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;
  • Kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria;
  • Kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.
Pia Mbunge ndiye mwakilishi wa wananchi waliomchagua katika kuhakikisha mipango ya maendeleo ya Jimbo la Uchaguzi inawasilishwa kwenye vyombo vya uamuzi likiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NB: Kwa upande wa Watumishi wa Serikali hawapaswi kuingia kwenye shughuli za kisiasa zenye lengo la kutaka kuchaguliwa akiwa bado ni mtumishi wa Serikali;

72. Iwapo mtu yeyote mwenye madaraka katika utumishi wa Serikali, madaraka ya aina iliyotajwa katika ibara ya 67(2) (g) ataamua:-

(a) kuwa mgombea uchaguzi wa Rais au wa nafasi
nyingine yoyote chini ya Katiba hii;
(b) kugombea uongozi wa ngazi yoyote katika chama cha siasa kinyume na masharti ya ajira,

Mtu huyo atahesabiwa kuwa utumishi wake umekoma tangu tarehe yake ya kuwa mgombea uchaguzi au ya kugombea uongozi katika chama cha siasa.

Kwa kuzingatia matakwa ya katiba siyo sahihi kwa mtumishi wa serikali kujiingiza kwenye mchakato wa uteuzi wakati mchakato huo haujaanza na hapaswi kuanza kutoa ushawishi wa aina yoyote kabla ya kipindi cha uchaguzi hakijaanza.

B. JE, MAJUKUMU YA WABUNGE YANAPASWA KUKOMA LINI - YAKIWEMO YA KUFADHILI SHUGHULI ZA MAENDELEO KATIKA JIMBO LAKE?.

Ukomo wa Majukumu ya Mbunge umeainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ifuatavyo:-

65.-(1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, maisha ya kila Bunge yatakuwa ni muda wa miaka mitano.

(2) Kwa madhumuni ya Katiba hii maneno "maisha ya Bunge" maana yake ni ule muda wote unaoanzia tarehe ambapo Bunge jipya limeitishwa kukutana kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu na kuishia tarehe ya kuvunjwa kwa Bunge kwa ajili ya kuwezesha Uchaguzi Mkuu mwingine wa kawaida kufanyika.

C. TARATIBU ZA MBUNGE KATIKA KUSAIDIA MAENDELEO YA WANANCHI WAKE PAMOJA NA MATUMIZI YA FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO.

5.1 Matumizi ya fedha binafsi za Mbunge katika kusaidia maendeleo ya wananchi hayasimamiwi na sheria yoyote. Hata hivyo nia ya matumizi hayo ndiyo inayozingatiwa zaidi kama nia ni kushawishi wananchi katika kufanya uamuzi wa kuchagua kiongozi basi Sheria ya Kudhibiti Gharama za fedha za Uchaguzi ya 2010 ndiyo itakayosimamia.

Pia Katiba inaainisha kuwa ni jukumu la kila mwananchi katika kuhakikisha anashiriki katika maendeleo ya nchi ambayo ni shughuli ya Serikali.

8(1)(d) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.

Kuhusu matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo utaratibu wake umeanishwa kwenye Sheria ya Kusimamia Mfuko wa Kuhamasisha maendelo ya Jimbo ya mwaka 2009.

D. JE, NI WAKATI GANI MAJUKUMU YA VIONGOZI WA SERIKALI KAMA WAZIRI, NAIBU WAZIRI, KATIBU MKUU NA NAIBU KATIBU MKUU KUFUATILIA MIRADI YA MAENDELEO MAJIMBONI YANAPASWA KUKOMA?.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaainisha kuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha wananchi wanakuwa na maendeleo.

8(1)(b) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;

Kwa kuzingatia masharti ya Katiba Viongozi wa Serikali wanapaswa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo majimboni katika kipindi chote cha uongozi wao.

Jukumu hilo linakoma tu kwa mtu huyo pale anapokuwa ameondolewa kwenye wadhifa unaomuwezesha kufuatilia miradi ya maendeleo majimboni.

ANGALIZO:
Katika kipindi hiki ambapo Bunge bado halijavunjwa, ukikuta Mhe. Waziri au Katibu Mkuu anakagua miradi ya maendeleo…TAKUKURU tutaizuia?
- Kwa kufanya hivyo, TAKUKURU haitakuwa inazuia jitihada za mendeleo katika eneo fulani?

- Je ni kwanini Mbunge wa jimbo husika asiongozane na huyo Mtendaji wa Serikali katika ukaguzi wa miradi hiyo??

E. JE, NI WAKATI GANI TAKUKURU INAPASWA KUINGILIA KATI SHUGHULI HIZI ILI KUDHIBITI VITENDO VYA RUSHWA?

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeainisha kuwa ni jukumu la kila Taasisi kuhakikisha inapambana na rushwa hapa nchini.

9(h) Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano.

Kwa hiyo, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;

Ndugu Wahariri,

Kwa maelezo hayo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inapaswa kuzingatia matakwa ya Katiba na Sheria za nchi katika kuhakikisha inazuia na kupambana na rushwa wakati wa:-

• Ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo,
• Ufadhili wa miradi ya maendeleo
• Utangazaji nia ya kugombea nafasi zilizoainishwa kwenye Sheria zinazosimamia uchaguzi

Wakati wa kutekeleza jukumu hilo la kuzuia na kupambana na rushwa ni vema kujielekeza pia kwenye Sheria ya Kudhibiti Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo imetoa tafsiri ya baadhi ya maneno ambayo yanatumika zaidi wakati wa uchaguzi na hususan Uchaguzi Mkuu. Maneno hayo ni pamoja na:

“Campaign period” means the period commencing immediately after the nomination day up to the day immediately preceding Election Day;

“election” means the act of selecting by vote a person from among a number of candidates to fill a vacancy in the Office of the President, a Member of Parliament conducted under the National Elections Act or a Councilor conducted under the Local Authority (Elections) Act and includes the nomination process;

“Nomination day” means a day appointed for the nomination of candidates in a contested election for the Office of the President, the Vice-President, a Member of Parliament or a Councilor;

“Nomination process” means the process by whatever procedure whereby a political party invites persons who wish to be sponsored by any of such political parties to stand as candidate in the elections;

“Prohibited practices” means any offence mentioned in and punishable under the provisions of Part V of the Election Expenses Act 2010.

Kwa hiyo basi, kwa kuzingatia masharti ya PART V ya Sheria ya Kudhibiti Gharama za Uchaguzi Na 6 ya mwaka 2010, TAKUKURU inatakiwa kuhakikisha inazuia rushwa na kupambana nayo wakati wote na hasa wakati wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama, wakati wa uteuzi unaofanywa na Tume ya Uchaguzi, na Wakati wa Uchaguzi wenyewe (kupiga kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo).

Ndugu Wahariri,

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inakemea harakati zote zinazofanyika mapema kabla ya KIPENGA cha kuanza kampeni kupulizwa.

Tabia hii ikomeshwe kwani tunataka uchaguzi huu wa viongozi ufanyike vizuri bila ya kuwa hata na harufu ya uwepo wa VITENDO VYA RUSHWA.

USHIRIKIANO NA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Wahariri,
TAKUKURU imechagua kuzungumza nanyi kwa kutambua mchango mkubwa mlionao katika Vyombo vya habari. Ninyi ndiyo mnaofanya yafuatayo:
  • Mnapanga habari ya kuchapwa kwenye gazeti au kurushwa kwenye Radio na Televisheni
  • Mnapanga Vichwa vya habari visomekeje
  • Mnapanga habari gani au ipi ndiyo ipewe uzito wa hali ya juu kwa siku husika
  • Mnapanga ni Mwandishi gani wa habari akaandike habari husika
  • Mnapanga ni taarifa ipi itolewe au isitolewe kwenye Vyombo vya habari.
TAKUKURU tunavishukuru Vyombo vya Habari kwakuwa vina mahusiano mazuri na Taasisi yetu:

- Vyombo vya Habari mmekuwa mkitupa fursa ya kutangaza na kuelimisha jamii juu ya mafanikio ya Serikali katika kuzuia na kupambana na Rushwa.
  • Mnatuita katika vipindi vya Televisheni
  • Mnatuita katika mahojiano kwa njia ya radio na pia
  • Mnatupa fursa ya kuandika makala katika magazeti yenu. TUNAWASHUKURU SANA!
- Tayari wengi wenu mmeshateua Contact Persons ambao tumekuwa tukishirikiana nao na kuwaalika katika MIKUTANO NA VYOMBO VYA HABARI kila tunapofanya hivyo na tunashukuru kuwa taarifa zetu hizo zinatangazwa kwa kiwango kikubwa katika vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii.

- Vilevile, ninatumia fursa hii kuwakumbusha kuwa VYOMBO VYA HABARI mna jukumu la kushiriki katika jitihada za kuzuia na kupambana na Rushwa kupitia MKAKATI WA TAIFA DHIDI YA RUSHWA NA MPANGO WA UTEKELEZAJI – AWAMU YA III (2017 – 2022) NACSAP III.

Ndugu Wahariri,

Niliona ni vema niwaite leo ili kwa kifupi nizungumze nanyi juu ya mambo hayo muhimu. Baada ya maelezo haya tutakuwa na muda mchache baadaye ambapo kwa pamoja TUJADILI NAMNA TUNAVYOWEZA KUBORESHA ZAIDI USHIRIKIANO ULIOPO.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.


IMETOLEWA NA:

BRIG. JEN. JOHN J. MBUNGO, ndc
MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU

No comments :

Post a Comment