Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiongea wakati wa kuzindua mpango huo.
Waziri Ummy Mwalimu akionyesha magari 18 ambayo yatatumika katika utoaji wa elimu kwa umma kwa siku 20
Waziri Ummy Mwalimu akiwa na
Mkurugenzi huduma ya Kinga Dkt. Leonard Subi(kushoto) na Mwakilishi
kutoka Red Cross Bw. Jonston Weston wakati wa uzinduzi wa mpango maalum
wa kutoa elimu kwa umma kwa jiji la Dar es Salaam.
*****************************
Serikali imezindua mpango maalumu
wa kutoa elimu ya afya kwa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na
kuwapo kwa ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Corona ikiwa ni
mwendelezo wa kuwafikia watu wengi katika ngazi ya mtaa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
wakati akizundua mpango wa elimu ya afya kwa umma kwa siku 20 ambao
utaongozwa na vikundi vya kijamii kwa kushirikiana na Red Cross chini ya
Wizara ya Afya.
Waziri Ummy amesema lengo la
kuzindua mpango huo ni kukata mnyororo wa maambukizi ya ugonjwa wa
Corona Kati ya mtu na mtu kwa kutumia vikundi vya kijamii ambavyo
vitaelimisha na kutoa taarifa sahihi kwa Jamii kuhusu ugonjwa wa Corona.
“Vikundi hivi vya kijamii, vitashirikiana na Wizara ya Afya na Red Cross na UNICEF kutoa elimu ya afya kwa umma.
Magari 18 yatatumika kwa siku 20
na yatakwenda katika maeneo ya masoko, stendi za mabasi na maeneo
mengine yenye mikusanyiko ya watu,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri amefafanua kuwa Ijumaa,
Jumamosi na Jumapili, vikundi vya kijamii vitakwenda katika maeneo ya
nyumba za ibada kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kutoa elimu ya afya
kutokana na kuwapo kwa ongezeko la ugonjwa wa Covid-19.
“Niwatoe hofu Watanzania,
tutashinda hii vita endapo kila mmoja katika Jamii atazingatia maelekezo
ya Wataalamu wa Afya,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri amesema mbali ya Elimu ya
afya kutolewa katika Mkoa wa Dar es Salaam, pia vikundi vya kijamii
vitakwenda katika mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza na Arusha kwa ajili ya
kutoa elimu ya afya kwa umma kuhusu kujikinga na maambukizi ya ugonjwa
Corona.
“Serikali inawashukuru Watanzania
kuhusu suala la kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, wameelewa,
wamepokea hili vizuri sana, hata katika ngazi ya Kijiji nje ya nyumba
wameweka ndoo ya maji na sabuni, kwa hili tunawashukuru Sana Watanzania
na tunawatia moyo wa kuendelea kunawa mikono kwa maji tiririka na
sabuni,” amesema Waziri.
Waziri amewasisitiza Watanzania
kuepuka mikusanyiko na misongamano ili kukabiliana na ugonjwa huo Kama
walivyofanya kwenye hatua ya kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Elimua
ya Afya kwa Umma wa Wizara ya Afya, Dkt. Ama Kasangala amesema
atahakikisha elimu kwa Jamii inatekelezwa ili kukabiliana na maambukizi
ya ugonjwa wa Corona nchini.
“Nitashirikiana na Red Cross na
wenzangu wa kitengo cha elimu ya afya kwa umma ili kuhakikisha Mipango
ya utoaji wa elimu kwa wananchi inatekelezeka,” amesema Dkt. Kasangala.
No comments :
Post a Comment