Msajili Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma akizungumzia kuhusu matumizi
ya mfumo wa kusajili mashauri kwa njia mtandao.
***************************
Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha- Mahakama
Watumishi wa
Mahakama ya Tanzania na Mawakili wamehimizwa kuwa mstari wa mbele katika
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili
kupunguza
msongamano wa watu mahakamani, kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona
na kuokoa gharama za utoaji haki.
Akizungumza leo
ofisini kwake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Wilbert Chuma
alisema matumizi ya TEHAMA kwa watumishi na Mawakili yawe ni sehemu ya
utendaji kazi wao wa kila siku ili kuendesha mashauri pasipokuwa na
ulazima wa wananchi kufika mahakamani na hivyo kupunguza msongamano usio
wa lazima.
‘‘Mashauri yote ya madai yanayohusisha mawakili yafunguliwe kwa njia ya mtandao na si vinginevyo,’’ alisema Msajili Mkuu.
Kanuni za
ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (Electronic Filling Rules,
2018 GN 148/2018) iliyotolewa na Jaji Mkuu na kuanza kutumika Aprili 13,
mwaka 2018 inasisitiza mashauri kufunguliwa kwa njia ya mtandao.
Alisema hivi sasa
kuna Mawakili 1,732 waliojisajili katika mfumo wa kufungua mashauri kwa
njia ya mtandao, lakini wanaoutumia ni 1,250. Hivyo alitoa wito kwa
Mawakili hao, wakiwa kama Maofisa wa Mahakama kuona umuhimu wa kutumia
mfumo huo hasa katika kipindi hiki cha kuenea kwa maambukizi ya virusi
vya Corona.
Kuhusu masuala ya
utoaji wa elimu ya matumizi ya njia hiyo, Msajili Mkuu alisema Maafisa
TEHAMA wa Mahakama kwa kushirikiana na Maafisa wengine wa Mahakama
wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi wa kawaida juu ya mfumo huo.
Mhe. Chuma
alisema viongozi wa kila ngazi ya Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani
hadi Mahakama ya Wilaya wanapaswa kuhakikisha kuna kioski au sehemu
maalumu yenye vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kusajili mashauri
kimtandao ili kuwasaidia wananchi wasioweza kumudu kutumia huduma hiyo
hususani wale wasio na uwakilishi.
Aliongeza kuwa
Maafisa TEHAMA wahakikishe kwamba wanatoa msaada unaohitajika wakati
wote katika maeneo hayo ili kufanikisha zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na
kuwapa haki wale wote wanaopaswa kupewa kwa mujibu wa taratibu.
‘‘Ni jukumu la
kila Mtendaji wa Mahakama katika eneo lake kuhakikisha mahitaji muhimu
yanapatikana ili kufanikisha zoezi hili, ’’alisisitiza.
Msajili Mkuu
huyo aliwataka watendaji kushirikiana na maafisa TEHAMA katika maeneo
yao kuhakikisha Majaji na Mahakimu wote wanatengenezewa sahihi za
kielektroniki ndani ya siku 21 kupitia maagizo aliyoyatoa Aprili 14,
mwaka huu.
Mhe. Chuma
aliwataka viongozi wa Mahakama kudhibiti idadi ya waandishi wa habari
wanaoingia maeneo ya Mahakama na kutoruhusu midahalo au mahojiano yoyote
ya waandishi wa habari maeneo ya viwanja vya Mahakama kuanzia sasa ili
kupunguza msongamano.
Kwa upande wa
uendeshaji mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao (Video Conference),
alisema tayari taratibu za manunuzi zimeshafanyika ili kuwezesha
upatikanaji wa vifaa hivyo kwa Mahakama ambazo hazina. Alisema
televisheni za ukutani 13 zitapelekwa katika magereza mbalimbali na
saba (7) zitapelekwa kwenye vituo vya Mahakama Kuu. Aidha kompyuta
mpakato 24 na scanner zitakazogawiwa kwenye maeneo hayo.
Machi 23, mwaka
huu, Jaji Mkuu wa Tanzania, katika Taarifa yake aliyoitoa kwa Umma
aliwataka viongozi wote wa Mahakama katika ngazi zote kuonyesha
uongozi kwa kuwasaidia Watanzania ili waendelee kupata huduma za utoaji
haki katika dunia ambayo inapata msukosuko mkubwa wa ugonjwa wa Corona.
No comments :
Post a Comment