Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuelezea tathmini ya hali ya Hewa kwa mwaka 2019. |
MAMLAKA ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) imesema Mwaka 2019 umeweka historia ya pekee kwa kuwa wa
nne kihistoria kwa kupata mvua nyingi tangu mwaka 1970.
Akifafanua kwa baadhi ya
wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes
Kijazi amesema nchi ilipata wastani wa milimita 1283.5 za mvua sawa na
asilimia 125 ya wastani wa mvua ya muda mrefu, yaani tangu mwaka 1981
hadi mwaka 2010.
Alisem kiwango hicho ni zaidi
ya wastani wa mvua ya muda mrefu kwa milimita 256.5. huku maeneo mengi
ya nchi yakipata mvua juu ya wastani katika msimu wa vuli na mvua za
wastani katika msimu wa masika.
“…Kiwango cha mvua
kilichorekodiwa mwezi Oktoba 2019 ni kiwango cha juu kabisa kurekodiwa
tangu mwaka 1970. Wastani wa joto nchini kwa mwaka 2019 ulikuwa ni nyuzi
joto 23.8 sawa na nyuzi joto 0.9, juu ya wastani wa joto wa muda mrefu
(1981-2010) Kiwango hiki cha joto kimechukua nafasi ya nne katika
historia ya vipimo vya joto kali tangu mwaka 1970,” alieleza Dk. Kijazi.
Aidha aliongeza kuwa Miezi ya
Machi na Aprili 2019 iliongoza kuwa na joto la juu ya wastani kwa nyuzi
joto 1.1 (Machi) na nyuzijoto 1.6 (Aprili) ukilinganisha na wastani wa
muda mrefu.
Alibainisha kuwa takwimu
zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 1970 na 2019 kumekuwa na matukio kumi na
matatu (13) ya mvua za za juu ya wastani katika msimu wa Vuli, na
matukio manne (4) tu katika msimu wa Masika na mwaka 2003 ndio ulikuwa
na upungufu zaidi wa mvua ukilinganisha na miaka mingine tangu mwaka
1970.
“…Takwimu zinaonyesha kuwa joto
la nchi limeendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu kuanzia mwaka 1995.
Ambapo joto la usiku (minimum temperature) limeongezeka zaidi
ikilinganishwa na joto la mchana (maximum temperature),” alibainisha
mtaalam huyo ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya
Hewa Duniani, WMO.
No comments :
Post a Comment