Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza
jambo wakati akiongea na Wataalamu wa Sekta ya Afya ngazi ya Mkoa
(hawapo kwenye picha) katika ofisi za mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Muonekano wa chumba atakacholazwa
mgonjwa wa Corona endapo atatokea, kilichopo katika jengo lililotengwa
kwaajili ya wagonjwa hao katika kituo cha Afya Mkonze Jijini Dodoma,
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na
Wataalamu wa Sekta ya Afya ngazi ya Mkoa katika ofisi za mkuu wa Mkoa wa
Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akikagua jengo la
wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akinawa mikono
kwa maji safi tiririka na sabuni pindi alipowasiri katika kituo cha Afya
Mkonze Jijini Dodoma kukagua jengo lililotengwa kwaajili ya washukiwa
wa ugonjwa wa Corona endapo watatokea.
Jengo lililotengwa kwaajili ya
matibabu ya ugonjwa wa Corona katika kituo cha Afya cha Mkonze Jijini
Dodoma endapo mgonjwa atatokea.
***********************
Na Rayson Mwaisemba, WAMJW-DOM
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaasa
Wataalamu wa Sekta ya Afya kuendelea kutoa Elimu kwa Wananchi kuhusu
maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Ameyasema hayo leo wakati wa ziara
yake ya kukagua hali ya utayari wa kupambana dhidi ya
maambukizi ya
ugonjwa wa Corona endapo utaingia Jijini Dodoma katika maeneo yote
yaliyopangwa.
“Elimu bado haitoshi, kila siku ni
lazima tuhakikishe tunatoa elimu kwenye jamii ili watu waweze kuelewa,
watu waelewe ugonjwa huu maana yake ni nini, na kwanini tunasisitiza
watu wanawe mikono, kwanini tunasisitiza maji tiririka na sabuni”
alisema.
Amesema kuwa, ni muhimu kwa
Wataalamu wa Sekta ya Afya kutoa Elimu ya kutosha kwa Wananchi, huku
akisisitiza kuwa si kweli kwamba matumizi ya vitakasa mikono
(sanitaizer) ni bora zaidi kuliko maji tiririka na sabuni.
“Si kweli kwamba Vitakasa mikono
(Sanitaizer) ni bora zaidi kuliko kutumia maji tiririka na sabuni,
tunahitaji tuwatoe hofu wanancni juu ya matumizi ya njia hizi mbili
katika kujikinga dhidi ya ugonjwa huu.” Alisema.
Aliendelea kusisitiza kuwa,
Wataalamu wa Sekta ya Afya kuongeza ubunifu katika kutoa elimu ili
kuepuka upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu katika jamii juu ya
kutibu maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona.
Aidha, Dkt. Ndugulile amewaagiza
Wataalamu wa Sekta ya Afya kutumia njia nyepesi zaidi katika kutoa elimu
ya ugonjwa wa Corona ili maambukizi haya yaweze kueleweka zaidi kwa
Wananchi.
Mbali na hayo, Dkt. Ndugulile
amesema kuwa, Serikali inaendelea kuleta mahitaji ya vifaa vyote
vinavyohitajika katika maeneo yaliyotengwa kwa wagonjwa wa maambukizi ya
virusi vya Corona endapo watatokea Jijini Dodoma.
“Niwahakikishieni vifaa vyote
tutavileta, lakini pia niendelee kuwaomba tuwe imara muda wote,
msisubiri ili kuweza kupambana na ugonjwa huu inabidi kuwa mbele muda
wote” alisema.
Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Dkt. Best Magoma ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa
kuendelea kuboresha maeneo ya utayari na kuweka msisitizo katika maeneo
yote ya muhimu ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti maambukizi ya
ugonjwa wa Corona endapo utatokea.
“Tunashukuru Wizara ya Afya na
Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa kutuunga mkono, wamekuwa karibu na sisi
katika kutupa maelekezo na muelekeo wa nini chakufanya katika kuboresha
Sekta ya Afya”alisema.
Dkt. Best Magoma, aliendelea
kusema kuwa, katika ngazi ya Mkoa wataendelea kuboresha maeneo yote
ambayo Wizara ya Afya kupitia Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile
ameelekeza katika zaira hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Faustine ndugulile amefanya ziara
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Kituo cha Afya Mkonze na
makazi ya chuo cha Dodoma, kukagua hali ya utayari wa kupambana dhidi ya
maambukizi ya ugonjwa wa Corona endapo utaingia.
No comments :
Post a Comment