***********************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
TAWI jipya la Bilal Muslim
Mission of Tanzania Kanda ya Ziwa, limeanza kazi kwa kufadhili vifaa vya
huduma ya kutakasa mikono vyenye thamani ya milioni 1.5 kwa taasisi za
dini na umma.
Vifaa hivyo vimetolewa jana kwa
waumini wa misikiti saba iliyo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) Mkoa wa Mwanza na Taasisi ya The Bakhiyyatullah Foundation
pamoja na Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mwenyekiti wa Bilal Kanda ya
Ziwa, Alhaji Sibtaib Meghjee akikabidhi vitakasa mikono hivyo kwa
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Hasani Kabeke, alisema lengo ni kusaidia
jamii kupambana na virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya
mapafu.
Alisema dunia inahangaika na
watu wako kwenye taharuki kubwa, hivyo taasisi hiyo katika kuunga mkono
juhudi za serikali ya awamu ya tano imeamua kufadhili misikiti saba,
taasisi ya Bakhiyyatullah Foundation na NIDA Wilaya ya Nyamagana kwa
kuwapatia matenki hayo yatumiwe na jamii kunawa mikono.
“Tunafanya haya kwa serikali ili
jamii ijue na kuonyesha uislamu ni dini ya amani tofauri na
inavyotupiwa madongo.Kazi inayofanywa na Waislamu ni kwa nia njema tena
bila ubaguzi,”alisema Meghjee.
Aidha aliwataka Watanzania
kuchukua tahadhari na kuzuia maambukizi ya corona kwa kunawa mikono
kila wakati na kuzingatia njia zinazoelekezwa na Wizara na wataalamu
kujikinga na virusi hatari vya corona (Covid-19).
Kwa upande Sheikhe Kabeke,
alisema vifaa hivyo ya kutakasa mikono ni muhimu katika kujikinga na
corona na kuishukuru taasisi ya Bilal kwa msaada huo muhimu hasa
kipindi hiki.
“Kimsingi tunashukuru Bilal
kutupatia sadaka hii kwenye misikiti yetu katika vita ya kukabiliana na
virusi vya corona.Wangeweza kusaidia kokote lakini wameona kheri
kusaidia taasisi ya dini,” alisema.
Alieleza kuwa Meghjee amekuwa
mwalimu bora katika kusaidia jamii ya watanzania maeneo mbalimbali
nchini bila ubaguzi wa aina yoyote na kumwombea kwa Mungu ampe afya
njema na kumwondolea watu wabaya.
Pia Sheikhe Kabeke alimshukuru
Rais John Magufuli kwa kuruhusu nyumba za ibada ziendelee kutoa hufuma
ya kiroho na maombi ili Mungu aliepushe taifa na janga hili hatari.
“Nitumie fursa hii kumshukuru
Rais Magufuli, ni Rais pekee ambaye hakufunga nyumba za ibada na hapa
watu wanamtegemea Mungu.Lakini Bilal niombe Mwenyezi Mungu akiwawezesha
msiishie kwenye misikiti saba tu na pia wengine nao wajitokeze ingawa
si kwamba hawawezi bali ni kiburi tu,”alisema.
Awali Sheikhe Hashimu Ramadhani
wa Bilal Muslim alisema ufadhili huo umetolewa na waumini wa Shia Ithna
Asheri Imamia Mwanza katika kuadhimisha siku ya Muhammad Al Mahdy
aliyezaliwa miaka 155 iliyopita.
No comments :
Post a Comment