*********************************
Serikali imesema licha ya
mipaka ya nchi kujifunga kutokana na janga la ugonjwa wa COVID 19,wageni
wachache wanaoingia nchini wanapokelewa kwa mujibu na taratibu za
kuingia nchini na kuhudumiwa kwa hadhi inayoendana na mahitaji ya
Kimataifa kama ilivyo katika nchi nyingine yeyote duniani huku tahadhari
ya kujikinga na ugonjwa huo ikipewa kipaumbele.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Kanali Wilbert Augustine
Ibuge ameyasema hayo alipofanya ziara katika uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere kukagua na kujionea namna wageni kutoka
mataifa mbalimbali wanavyopokelewa na hatua wanazopaswa kuzifuata kabla
ya kuruhusiwa kuingia nchini.
Balozi Kanali Ibuge amesema
licha ya ukweli kwamba kwa sasa wageni wanaoingia nchini ni wachache
sana kutokana na mipaka kujifunga ni muhimu serikali kuhakikisha kuwa
wale wachache wanaoingia wanafuata taratibu za nchi na kupewa utaratibu
wa namna ya kujikinga na ugnjwa wa COVID 19 bila ya uwepo wa malalamiko
kutoka kwa wageni hao.
Ameongeza kuwa ameridhishwa na
hali ilivyo katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
kwa kuwa hadhi wanayopewa wageni hao haina tofauti na hatua
zinazochukuliwa katika mataifa mengine duniani na kwamba ni muhimu
kufanya hivyo ili kuhakikisha usalama wa Taifa na raia wake kwa ujumla.
Amewataa watumishi
wanaoendelea kutoa huduma katika uwanja huo kuchukua tahadhari ya
kujikinga na COVID 19 huku wakitumia kauli nzuri wakati wa kutoa huduma.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Kanali
Wilbert Ibuge amekagua jengo la kwanza la uwanja huo na jengo jipya la
tatu akiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya viwanja vya ndege TAA
Mhandisi Julius Ndyamukama.
No comments :
Post a Comment