Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza kwa njia ya video na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Mkoa wa Mwanza akiwa ofisini kwake, Mlimwa jijini Dodoma, Aprili 15,
2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa (KUU) wa
Mwanza imchukulie hatua za kisheria mfanyabiashara aliyekamatwa kwa
makosa ya kujihusisha na biashara ya zana haramu za uvuvi.
“Yuko mfanyabiashara anaitwa Jeremiah Asam Omolo amekamatwa mara kadhaa kwa
kukutwa na nyavu haramu. Wizara ilitoa specifications (aina
ya nyavu) zinazoruhusiwa kutumika na KUU ya Mkoa ikasimamia lakini kuna
maafisa wa Wizara waliingilia zoezi hilo mara tatu na akatozwa faini
mara zote,” amesema.
Waziri Mkuu
ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Aprili 15, 2020) wakati akizungumza na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao alichokifanya
kwa njia ya video (video conference) kutokea ofisini kwake Mlimwa,
jijini Dodoma.
“Mkuu wa Mkoa
aliunda timu ya kuchunguza matukio haya. Hii ni timu ya Serikali na
imeaminiwa kufanya kazi hii, na ina uwezo wa kuchukua hatua. Lazima KUU
ya Mkoa isimamie na ichukue hatua. Hatuwezi kuwa na Wizara ambayo
haiiamini KUU ya Mkoa,” amesisitiza.
Amesema hatua
pekee ambazo zilichukuliwa na Wizara ni kumtoza faini mfayabiashara
huyo kwa kumlipisha zaidi ya sh. milioni 470. “Lengo la Serikali siyo
kutoza fedha peke yake, bali ni kudhibiti matumizi ya nyavu haramu
nchini,” amesisitiza.
Amesema kwa
kuwa si mara yake ya kwanza kukamatwa, KUU ya Mkoa haina budi kuchukua
hatua kali zaidi kwa sababu nia ya kutoa adhabu ni kumfanya mkosaji
asirudie kosa lakini mfanyabiashara huyo amekuwa akilipa faini na
kurudia makosa yaleyale.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella alisema katika kosa la
kwanza, mfanyabiashara huyo alipatikana na marobota 66 ya nyavu haramu
aina ya makila sawa na vipande 13,200 ambapo alitozwa faini ya sh.
milioni 50.
Amesema
katika tukio la pili, Aprili 3, mwaka huu, Bw. Omolo alikutwa na zana
haramu za uvuvi aina ya makila vipande 6,964 na Timba vipande 179 na
kutozwa faini ya sh. milioni 129.8.
“Katika tukio
la tatu, Aprili 4, 2020 alipatikana na kosa la kumiliki zana haramu za
uvuvi ambazo ni marobota 10 ya nyavu haramu aina ya makila sawa na
vipande 300 na marobota 437 ya nyavu haramu aina ya Timba sawa na
vipande 12,875 na kutozwa faini ya sh. milioni 300,” alisema.
Alisema
uongozi wa mkoa uliamua kuunda timu ya wataalamu inayojumuisha vyombo
vya usalama ambayo itafuatilia na kuchunguza kwa undani mienendo ya
mtuhumiwa huyo ikiwemo masuala la kikodi na ufanyaji wa biashara.
Mkuu huyo wa
Mkoa alimweleza Waziri Mkuu kwamba timu hiyo iliyoundwa Aprili 9, mwaka
huu, itapaswa kukamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa yake, Jumatatu
ijayo (Aprili 20, 2020).
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amekemea mikusanyiko inayofanyika kwenye nyumba za
ibada kwa kigezo cha kutaka watoto wasikae majumbani kwa vile hawaendi
shuleni.
“Ninazo taarifa kwamba wameanzisha mfumo wa kupeleka watoto kwenye madarasa ya dini maarufu kama Sunday School. Tumeruhusu
ibada tu, na hizo ibada lazima ziangaliwe ziwe za muda mfupi kadri
inavyowezekana. Tumesisitiza kwenye makanisa au misikiti ambako ibada
zinafanyika, waumini wakae kwa kuachiana nafasi.”
Amesema
changamoto inajitokeza kwenye makanisa makubwa ambayo yana waumini
karibu 3,000. “Hayo sasa yatakuwa ni makongamano. Tunaaamini Maaskofu na
Mufti wataliweka vizuri suala hili la sunday school na madrassa,” amesema.
Amesema Serikali haitazuia biashara kwenye masoko, maduka au supermarkets isipokuwa
amewataka wenye biashara hizo wahakikishe wanaweka ndoo za maji na
sabuni ili wateja wanawe mikono kabla ya kuingia kupata huduma na wakati
wanapotoka kupatiwa huduma hizo.
Kuhusu
mikusanyiko mingine, Waziri Mkuu amesema watu wanapaswa wajizuie kwenda
kuzagaa kwenye vituo vya mabasi na kama hawana shughuli za lazima za
kufanya huko, basi wabakie majumbani kwao.
Naye Mkuu wa
Mkoa alisema mkoa huo una mgonjwa mmoja ambaye vipimo vyake vya mwisho
vilichukuliwa na kupelekwa maabara na kama itathibitishwa hana
maambukizi, ataruhusiwa kurudi nyumbani.
No comments :
Post a Comment