Thursday, March 5, 2020

VIJANA WAOMBA SERIKALI KUANZISHA VIJIJI VYA KILIMO



Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiongoza majadiliano wakati wa kongamano la vijana kujadili fursa za kilimo mifugo na uvuvi kwa mikoa ya Tabora,Singida,Dodoma na Kigoma katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi leo mjini Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiwa na vijana wakisoma maazimio ya mkoa kuhusu upandaji miti mara baada ya kupanda miti ya kumbukumbu akihimiza vijana kupanda miti naili kutunza mazingira na kupata ajira 
Kijana Raphael Malongo( kushoto)  toka mkoani Singida akitoa ushuhuda wa mafanikio aliyoyapata baada ya mafunzo kwa vitendo toka nchini Benin yaliyomwezesha kuanzisha kilimo biashara na kuajili vijana wenzie Singida.Kulia ni Mwezeshaji wa kongamano Joseph Massimba wa SUGECO Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiwa na vijana mara baada ya kumaliza zoezi la upandaji miti ikiwa ni uhamasishaji kilimo cha miti na kuzalisha ajira kwa vijana wa mikoa ya Tabora,Singida,Dodoma na Kigoma
(Habari na picha  WK)
………………………………………………………………………………………………..
Tabora
Vijana wameiomba serikali ianzishe vijiji maalum kwa ajili ya shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi endelevu ili kuongeza upatikanji wa malighafi za viwanda nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Mjini Tabora na Mwenyekiti wa Wajasiliamali  Vijana mkoa wa
Tabora Mfaume Juma Mfaume kwenye kongamano la vijana katika kilimo  na kuongeza kuwa uwepo wa eneo maalum la kilimo kwa vijana kutasaidia vijana kuwa na uhakika wa ardhi
“Sisi vijana wa Tabora tunaomba tupatiwe mashamba ekari angalau kumi kwa ajili ya kuzalisha ili tuwe na kijiji cha wajasiliamali wazalishaji mazao ya kilimo na uvuvi ili kuondoa tatizo la ardhi “ alisema Mfaume
Aliongeza kusema kuwa vijana wengi wanashindwa kufanya kazi za kilimo kwa kuwa halmashauri nyingi hazitenga mashamba na maeneo ya ufugaji kibiashara na tatizo la ukosefu wa mitaji na elimu ya ujasiliamali 
Mfaume alitumia fursa ya kongamno hilo kupongeza jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri  za kuwafundisha vijana kuacha kukaa vijiweni na sasa wamehamasika kujiunga katika vikundi vya upandaji miti na kilimo kama sehemu ya ajira.
“Tabora yetu imebadilika  tangu Mkuu huyu wa Mkoa afike,vijana tulianza kwa shida lakini alitutia moyo sasa tumefanikiwa kukopeshwa trekta mbili kwa ajili ya kilimo “ alisema Mfaume
Kwa upande wake,Imanuel Sotta wa shirika la Compassion Tabora ameipongeza serikali kwa utashi na maono yake ya kuwezesha vijana kupitia mikopo ya uwezeshaji vijana kiuchumi  toka mapato ya ndani ya halmshauri.
Kijana John Kipingu toka Nzega ameeleza kuwa anaiomba serikali iwasimamie maafisa ugani kuweza kuwafundisha vijana kutumia rasilimali maji kulima kilimo cha bustani na mboga mboga kwani zinahitajika sana sokoni.
Nae Beatrice Bilanda toka wilaya ya Kibondo mkoa wa Kigoma alisema vijana wanahitaji taarifa za fursa ya kilimo mapema ili ziwasaidie kufanya mabadiliko na ushiriki katika kilimo utaongezeka.
“ Kilimo cha mazao kwa kutumia jembe la mkono  na bei ya kubwa ya pembejeo na mbegu zinaendelea kuwa changamoto kwa vijana walio katika kilimo  na ufugaji” alisema Beatrice na kuiomba serikali kutoa mikopo ya pembejeo kwa vijana.
 Naye Raphael Malongo toka Singida amewashauri vijana wenzake kujisomea vitabu na kutumia mitandao ya kijamii kupata elimu na mafunzo yatakayo saidia kuongeza tija katika uzalishaji mazao ya kilimo na mifugo na kutatua changamoto za soko na visumbufu vya mazao
“ Naishukuru Wizara ya Kilimo na FAO kwa kunifadhili kwenda masomoni nchini Benin kujifunza kwa vitendo shughuli za kilimo hata sasa nimeweza kuanzisha kilimo biashara Singida na kuajili vijana wenzagu kupitia kampuni ya Malongo Poulty Farm  kufugaji nyuki kisasa” alisema Malongo 
Malongo amesema kwa sasa amefanikiwa kutengeneza mtambo wa kuzalisha nishati ya bio gesi baada ya kufuga ng’ombe mmoja tu anawezesha kupata samadi anayotumia kuzalisha mazao ya bustani na chakula,hivyo vijana wajitokeze kutumia fursa za kilimo kwa kushiriki kwenye makongamano na mafunzo
Akijibu hoja za vijana ,Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewataka vijana kutumia ardhi nzuri iliyopo nchini na uwepo wa wataalam wa kilimo na mifugo  kujiunga katika vikundi vya ushirika ili wapate nguvu ya kuanzisha kazi za kilimo na kufikiwa na fursa za mitaji na utaalam
Mwanri amewashauri vijana nchini kujituma na kubadili fikra kuwa kilimo na ufugaji ni ajira ya uhakika kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa na malighafi za viwandani  kuongezeka.
“ Leo vijana mmekutana hapa  serikali inataka kuwajengea matumaini mapya ili mbadilike na kutumia fursa za kilimo,mifugo na uvuvi kuongeza uchumi wenu na kuzalisha ajira “ alisema Mwanri
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kaliua Abel Busalama amewataka vijana kujiamanini  kuwa sekta ya kilimo ni chaguo sahihi kwa wakati huu ambapo serikali inajielekeza kuhamasisha vijana kujiajili 
Busalala aliongeza kuwa fahamisha vijana kuwa uchumi wan chi unategemea kilimo ndio maana jitihada kubwa kupitia halmashauri zinafanyika kwa kutenga maeneo kwa vijana wanaojitokeza kama ilivyo kwa halmashauri ya wilaya ya Kaliua.
Kongamano la vijana katika kilimo limefanyika katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini Tabora na kuhusisha vijana zaidi ya 340 toka mikoa ya Tabora ,Singida,Dodoma na Kogoma chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri 

No comments :

Post a Comment