Na.Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Jitihada za makusudi za Serikali
ya Awamu ya Tano katika kusimamia na kutekeleza sera madhubuti za fedha
na uchumi hasa katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi,
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, pamoja na usimamizi wa Benki,
zimeelezwa kuwa ni miongoni mwa vitu vilivyoifanya Tanzania kukua
kiuchumi na kunakoisaidia kue ndelea na ukuaji wa kasi katika siku
zijazo.
Kwa mujibu wa ripoti ndogo
iliyotolewa Jijini Dar es Salaam na wataalam wa Shirika la Fedha
Ulimwenguni (IMF), waliomaliza muda wao wa kufanya utafiti hapa nchini
kuanzia tarehe 20 Februari hadi Machi 4 Mwaka huu, Tanzania ni miongoni
mwa nchi chache za Afrika zinazofanya vizuri katika ukuaji wa Uchumi.
Kiongozi wa timu hiyo ya IMF
iliyotembelea Tanzania Enrique Gelbard amesema kiwango cha ukuaji wa
uchumi katika kipindi cha miezi michache iliyopita kinaonyesha ukuaji wa
kasi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali , kuongezeka
kwa mauzo ya nje ya nchi, pamoja na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta
binafsi.
Amesema viashiria hivyo
vitaifanya Tanzania kuendelea kukua kiuchumi katika siku zijazo katika
sekta za Ujenzi na madini, unaosaidiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei
kwa kiwango cha asilimia 3.7 pamoja na kuimarika kwa viwango vya
kubadilisha fedha za kigeni ,kadhalika na uwepo wa akiba ya kutosha ya
fedha za kigeni inayoweza kufanya manunuzi kwa kipindi cha takribani
miezi mitano.
Aidha mtaalam huyo amezungumzia
kuimarika kwa uchumi hapa nchini kuwa kumesababishwa na sera madhubuti
za usimamizi wa fedha ambazo zimeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi hapa
nchini, pia amezipongeza mamlaka husika kwa kuendelea kusimamia
ukusanyaji wa mapato.
No comments :
Post a Comment