Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya
Wanawake na Uzazi, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake,
Enid Chiwanga (kushoto) akiongea na ujumbe wa THBUB (mbele yake)
uliotembelea Hospitali ya rufaa jijini Dodoma mapema leo Machi 6, 2020.
Kamishna wa THBUB, Dkt. Fatma
Khalfan (kulia) na Kamishna Amina Talib Ali (kushoto) wakitoa mkono wa
pole kwa mmoja wa wazazi waliojifungua katika Hospitali ya rufaa jijini
Dodoma walipotembelea kuwaona wagonjwa mapema leo Machi 6, 2020.
Ujumbe wa THBUB ukiwa katika picha
ya pamoja na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, ambaye pia
ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Enid Chiwanga (katikati)
huku wakionyesha ishara ya “mwanamke hodari”muda mfupi mara baada ya
ujumbe wa THBUB kumaliza ziara yake katika hospitali hiyo.
…………………………………………………………………………………….
Na Mbaraka Kambona,Dodoma
Katika kuelekea kilele cha
kuadhimisha siku ya wanawake duniani, ujumbe wa wanawake kutoka Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) umetembelea Idara ya
Magonjwa
ya Wanawake na Uzazi iliyopo katika Hospitali ya rufaa jijini Dodoma
mapema leo Machi 6, 2020.
Ujumbe huo uliotembelea
hospitali hiyo uliongozwa na Makamishna wawili, Dkt. Fatma Khalfan na
Amina Talib Ali kwa lengo la kuwafariji wakina mama wagonjwa na wazazi
waliolazwa katika hospitali hiyo.
Kamishna wa THBUB, Dkt. Fatma
Khalfan akiongea wakati wa kukabidhi bidhaa mbalimbali walizopeleka kwa
ajili ya wagonjwa alisema kuwa lengo la ziara yao ni kwenda kuwafariji
wagonjwa kina mama katika hospitali hiyo kwa kuzingatia wiki hii ni ya
kuadhimisha siku ya mwanamke duniani.
Dkt. Fatma alisema kuwa Afya ni
muhimu sana kwa mwanadamu na kwamba jamii haitaweza kujenga uchumi wake
kama watu wake hawana afya nzuri.
Aliongeza kwa kusema kuwa kwa
niaba ya uongozi wa THBUB wanaipongeza serikali kwa jitihada zake za
makusudi katika kuboresha sekta ya afya nchini hususani matibabu mazuri
kwa kina mama na watoto.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya
tano chini ya Rais John Pombe Magufuli imeendelea kutekeleza utoaji wa
haki ya afya kwa vitendo kwa kuendelea kuboresha na kujenga miundo mbinu
mbalimbali ya zahanati na vituo vya afya ikiwemo kuongeza bajeti ya
ununuzi wa dawa nchini.
Aidha, Dkt. Fatma alisema kuwa
pamoja na jitihada kubwa za serikali katika kuboresha sekta ya afya bado
kuna changamoto ambazo zinaikabili sekta hiyo na hivyo kutoa wito kwa
wadau kushirikiana pamoja na serikali katika kutatua changamoto hizo.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya
Wanawake na Uzazi, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake,
Enid Chiwanga wakati akiupokea ujumbe huo alitoa shukrani kwa uongozi
wa THBUB kwa uamuzi wao wa kutembelea wagonjwa katika hospitali hiyo na
kusema kuwa wamefarijika kwani ziara hiyo itatoa tumaini jipya kwa
wagonjwa waliopo katika hospitali hiyo.
Kilele
cha maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani mwaka huu ni Machi 8, 2020
na kwa mwaka huu maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kumbukizi ya
miaka 25 tangu wanawake wakutane katika mkutano wa Beijing nchini China
mwaka 1995.
No comments :
Post a Comment