Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha (wa kwanza
kulia), akiwasilisha taarifa fupi ya Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kwa Bodi ya
Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
ilipotembelea jengo hilo leo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Mshauri Julius Ndyamukama
(aliyenyanyua mikono) akielezea jambo mbele ya Bodi ya Ushauri (MAB)
iliyotembelea jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA-TB3) katika ziara ya kikazi.
Kaimu Meneja wa Jengo la Tatu la
Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3),
Mhandisi Barton Komba (kulia), akitoa maelezo mbalimbali kwa Bodi ya
Ushauri (MAB) iliyotembelea jengo hilo leo. Aliyevaa tai ni Mwenyekiti
wa Bodi hiyo Dkt. Masatu Chiguma.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB)
ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiangalia ramani ya
jengo hilo wakati wakilitembelea katika ziara ya kikazi iliyofanyika
leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri
(MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Dkt Masatu Chiguma
akipimwa joto la mwili na Afisa Afya, Yusta Malisa wakati bodi hiyo
ilipotembelea Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kwa ziara ya kikazi.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB)
ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiangalia moja ya begi
likipita kwenye mkanda ikiwa ni hatua ya tatu kwa ukaguzi kabla
halijafika hatua ya mwisho tayari kupelekwa kwenye ndege, walipotembelea
jengo hilo leo katika ziatra ya kikazi.
…………………………………………………………………………………
Na Bahati Mollel,TAA
BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeridhishwa na ukaguzi wa abiria
wanaotoka nje ya nchi wanaotumia Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja
cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3).
Mwenyekiti wa MAB, Dkt Masatu
Chiguma amesema leo mara baada ya kumalizika kwa ziara yao ya kwanza ya
kikazi tangu kuteuliwa kwao hivi karibuni ya wametembelea jengo hilo
kuwa maafisa afya waliopo kwenye Jengo hilo wanafanya ukaguzi kulingana
na taratibu zilizowekwa, ili kuzuia maambukizi ya Homa Kali ya mapafu
inayoambukizwa na virusi aina ya Corona, isiingie nchini.
Dkt Chiguma amesema tahadhari
ya kuzuia ugonjwa huo ulioanzia nchini China na kusambaa kwenye nchi
mbalimbali Duniani, imefanyika ipasavyo kwenye Jengo hilo, baada ya
kulitembelea na kuona, vifaa na utendaji wa watumishi hao wa afya.
“Matayarisho ya kujihadhari na
huu ugonjwa wa Corona yamefanyika kwa hali ya juu na wajumbe wa Bodi
tumeridhika baada ya kuona vifaa vinavyohitajika kuvaliwa na watendaji
wa kitengo cha afya na pia watumishi wa TAA waliopo maeneo ya kuwasili
na maeneo mengine,” amesema.
Akizungumzia jengo hilo, Dkt
Chiguma amesema anaipongeza serikali kwa ujenzi wa jengo hili la kisasa
lenye vifaa vya kimataifa, ambapo uendeshaji wake ni wa hali ya juu.
“Tumepita kuanzia mwanzo wa
jengo hadi mwisho wa jengo na tumejionea namna lilivyo bora na zuri,
hata vifaa vyake ni vya kitaalam sana, ukiangalia eneo la mizigo ni
mashine tu zinafanyakazi pamoja na kuwa na Watumishi wachache lakini
kila kitu kinaongozwa na mashine za kisasa,” amesema.
Hatahivyo, amesema Bodi
imebaini bado katika jengo hili kuna upungufu mkubwa wa watumishi,
ambapo sasa waliopo wengi ni wanaofanya kazi kwa mikataba mifupi na wale
wanaendelea kujifunza (Internship), ambapo ni hatari kwa kuwa sio
wakutegemewa zaidi kutokana kuweza kuondoka wakati wowote watakapopata
ajira ya kudumu.
Pia ameitaka menejimenti ya
TAA kuhakikisha inaboresha maslahi ya watumishi ili waendelee kulitunza
jengo hilo kwa kufanya kazi kwa bidii.
Halikadhalika amesema ulinzi
na usalama wa abiria na mizigo yao kwenye Jengo hilo ni wa hali ya juu
na uliopangiliwa vyema, kwa kuanzia abiria anapoingia wakati akisafiri
hadi kufika kwenye ndege, hata mizigo inavyokaguliwa kwa kupitia hatua
tano napo panaridhisha.
Katika hatua nyingine, Dkt
Chiguma amewaita Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye jengo
hilo, pale TAA itakapotangaza zabuni mbalimbali, maana bado yapo maeneo
mengi ya uwekezaji.
Awali akiwasilisha ripoti ya
ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha amesema
wanakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za uendeshaji, ambapo jengo
zima kwa asilimia 100 linatumia umeme wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), na ukikatika hutumika jenereta ambazo zinatumia mafuta mengi.
Pia amesema wanakabiliwa na
upungufu wa watumishi, ambapo wanalazimika kutumia zamu fupifupi na
wengine waliotoka asubuhi kurudi jioni kuongeza nguvu (supporting).
No comments :
Post a Comment